Chanjo ni nini?
Chanjo huokoa maisha ya hadi watoto milioni 3 kila mwaka. Chanjo hukinga maradhi, ulemavu na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwa ni pamoja na surua, homa ya ini (hepatitisi B), dondakoo, kifaduro, nimonia, polio, kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota, rubela na pepopunda.
Kisayansi chanjo ni kitendo cha kupewa kinga mwili kwa njia ya kuamsha vitoa kinga viwe tayari kupambana na adui ambaye wanamjua tayari.
Umuhimu wa chanjo
Watoto waliopata chanjo huwa wamekingwa dhidi ya magonjwa hatari, ambayo kwa kawaida huweza kusababisha ulemavu au kifo. Watoto wote wana haki ya kupata kinga hii. Kinga ya utotoni ni muhimu sana hasa kwa ukuaji wa baadae. Hivyo basi, chanjo kwa mtoto katika mwaka wake wa kwanza na katika mwaka wa pili ni muhimu sana.
Ni muhimu pia, kina mama wajawazito kupata chanjo ya pepopunda ili kujikinga wao wenyewe na watoto wao wanaozaliwa. Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu sababu za umuhimu wa chanjo, ratiba ya chanjo inayotumika na mahali chanjo inakotolewa kwa watoto.
Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu kuwa kutoa chanjo kwa mtoto mgonjwa kidogo au mwenye ulemavu au mwenye upungufu wa lishe ni salama.
Ukweli kwa ajili ya familia na jamii kuhusu chanjo
1. Chanjo ni jambo la lazima. Kila mtoto ni lazima apate chanjo zote zilizopendekezwa. Kinga ya utotoni ni muhimu sana; chanjo katika mwaka wa kwanza na wa pili zina umuhimu wa pekee. Wazazi wote au walezi wengine wanapaswa kuzingatia ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu muda wa kukamilisha chanjo zinazohitajika.
2. Chanjo hutoa kinga dhidi ya magonjwa mengi hatarishi. Mtoto ambaye hajapata chanjo yuko katika hatari kubwa ya kupatwa na maradhi, ulemavu wa kudumu au hata kupoteza maisha.
3. Mama wote wajawazito pamoja na watoto wao wanapaswa kukingwa dhidi ya pepopunda. Hata kama mama aliwahi kupata chanjo kabla , anapaswa kupata ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu kama bado anahitaji kupewa chanjo ya pepopunda.
4. Sindano mpya hazina budi kutumika kwa kila mtu anayepata chanjo. Kila mtu anapaswa kudai sindano mpya kwa kila chanjo anayopewa.
5. Ugonjwa huweza kuenea haraka watu wengi wanapokuwa wamekusanyika pamoja. Watoto wote wanaoishi katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa , hasa katika mazingira ya wakimbizi au ya watu waliojikusanya kutokana na janga fulani, wanapaswa kupewa chanjo haraka.
6. Kadi ya chanjo ya mtoto (au ya mtu mzima) haina budi kuwasilishwa kwa mtoa chanjo kabla ya kutolewa kwa chanjo.
Aina za chanjo
BCG (Bacile Calmette-Guérin)
Watoto wote wanastahili kupokea chanjo itwayo BCG (Bacile Calmette-Guérin) vaccine. Hii huumpa mtoto kinga dhidi ya aina zingine za kifua kikuu na ukoma.
DTP au DPT (Dondakoo, Pepopunda na Kifaduro)
Watoto wote wanastahili chanjo dhidi ya dondakoo, pepopunda na kifaduro kupitia aina ya chanjo iitwayo DTP au DPT vaccine. Viini vya dondakoo husababisha maambukizi ya njia ya kuingizia hewa na huenda ikasababisha shida za kupumua na hata kifo. Pepopunda nayo husababisha kukauka kwa misuli na maumivu makali yanayo sababishwa na mkazo wa misuli. Mkazo huo wa misuli unaweza sababisha kifo. Kifaduro huathiri njia ya kuigizia hewa na kusababisha kikohozi kinachoweza dumu wiki nne hadi nane na ni hatari sana kwa watoto wachanga.
Wanawake wote waja wazito na watoto wachanga wanahitaji chanjo ya pepopunda.
Surua
Watoto wote wanastahili kupokea chanjo dhidi ya surua. Maradhi ya surua husababisha utapiamlo, udhaifu wa maendeleo ya ubongo na huweza kufanya mtoto kiziwi au kipofu. Ishara zinazoelekeza kuwa mtoto anaweza kuwa anaugua surua ni pamoja na kuongezeka kwa joto mwilini, upele, kikohozi, kumwaga kamasi na macho kubadilika na kuwa mekundu. Tahadhari, mtoto anaweza kufa kutokana na surua.
Polio
Watoto wote wanastahili chanjo dhidi ya polio. Dalili za polio ni utepe kwenye mguu au mkono na udhaifu wa kukitumia kiungo kilicho athirika. Kwa kila watoto mia mbili wanaoambukizwa maradhi ya polio, mmoja atapata ulemavu wa maisha.
Ratiba za chanjo hutofautiana kulingana na nchi au sehemu ya nchi unayoishi. Ni muhimu kufuatilia ratiba ya chanjo kwa mujibu wa mwongozo wa taifa. Watoto wanastahili kupokea chanjo kwa umri unaostahili na kwa muda unaostahili.
Pamoja na kutofautiana huku kwa ratiba za chanjo kati ya nchi na nchi, unaweza kufuatilia utaratibu uliopendekezwa na CDC (Centre for Disease Control) hapa chini.
Ufuatao ni mtiririko wa chanjo husika na wakati muafaka ambao mtoto wako anatakiwa awe ameshapatiwa.
UMRI | AINA YA CHANJO | INATOLEWAJE | MUHIMU KUJUA |
0 – Anapozaliwa | Kifua Kikuu (BCG) | Sindano bega la kulia | Ni lazima kovu lotokee kwenye bega la kulia baada ya muda |
Polio (OPV 0) | Matone mdomoni | Chanjo ya ugonjwa wa kupooza ya kuanzia | |
Wiki ya 6 | Polio (OPV 1) | Matone mdomoni | Chanjo ya kwanza ya ugonjwa wa kupooza |
DTB-HepB-Hib1 (Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B) | Sindano paja la kushoto | Chanjo ya kwanza ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B kwa pamoja. | |
PCV 1 | Sindano paja la kulia | Chanjo ya Nimonia ya kwanza | |
Rota 1 | Matone mdomoni | Chanjo ya Kuhara ya kwanza | |
Wiki ya 10 | Polio (OPV 2) | Matone mdomoni | Chanjo ya pili ya ugonjwa wa kupooza |
DTB-HepB-Hib2 (Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B) | Sindano paja la kushoto | Chanjo ya pili ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B kwa pamoja. | |
PCV 2 | Sindano paja la kulia | Chanjo ya Nimonia ya pili | |
Rota 2 | Matone mdomoni | Chanjo ya kuhara ya pili | |
Wiki ya 14 | Polio (OPV 3) | Matone mdomoni | Chanjo ya mwisho ya ugonjwa wa kupooza |
DTB-HepB-Hib3 (Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B) | Sindano paja la kushoto | Chanjo ya tatu ya Dondakoo, Kifaduro, Pepopunda na Hepatiti B kwa pamoja. | |
PCV 3 | Sindano paja la kulia | Chanjo ya Nimonia ya tatu | |
Miezi 9 | Measles (MR 1) | Sindano bega la kushoto | Chanjo ya kwanza ya surua |
Miezi 15 | Measles (MR 2) | Sindano bega la kushoto | Chanjo ya pili ya surua |
IMEPITIWA: 26 MAY 2020