Virusi Vya Corona COVID19 na Ujauzito

 

Je, wajawazito na kina mama wanaonyonyesha wanahitaji kujua nini kuhusu virusi vya corona?

Kuna mengi yasiyofahamika kuhusu madhara ya virusi vya corona kwa wajawazito na kina mama wanaonyonyesha. Lakini uelewa wa madhara ya virusi hivi utaongezeka kadiri muda unavyoenda.

Kuwa mjamzito huleta wasiwasi na hali ya sintofahamu kwa wamama wengi watarajiwa, hata kama kila kitu kinaenda sawa.

Wanahitaji kuepuka aina fulani ya vyakula mfano samaki wasiopikwa vizuri na jibini laini. Hii ni kwasababu miili yao inabadilika kwa kiasi kikubwa kila siku na utaratibu wake wa kawaida unaweza kuvurugika.

Taifa la Uingereza ni moja ya nchi ambazo hivi karibuni zimewahusisha wanawake wajawazito katika kundi la watu walio katika hatari za kupata maambukizi haya. Inashauriwa wanawake wajawazito kukaa mbali na mikusanyiko ya watu ili kupunguza nafasi za kushika virusi vya Corona. Inaeleweka, wajawazito wengi na familia zao wana wasiwasi na wamechaganyikiwa kwasababu ya ujio huu wa Virusi vya Corona.

Pamoja yote hayo, ukweli unabaki kuwa hatuna ufahamu wa kutosha kuhusu madhara ya virusi hivi vya Corona COVID-19 kwa wajauzito. Kuwepo kwa ufahamu wa kutosha husaidia kuchukua hatua za uhakika. Uwepo mdogo wa wanawake wajawazito waliopata maambukizi haya pamoja na ufahamu wa kutosha wa Virusi hivi vya Corona kwa ujumla utatusaidia kutoa ushauri wa ziada kwa wanawake wajawazito kuchukua tahadhari mapema.

Mfumo Dhaifu wa Kinga ya Mwili

Mwanzoni ilidhaniwa kipindi cha ujauzito kinga ya mwili ya mwanamke inadhoofika na kumfanya kuwa katika hatari ya kupata maambukizo. Hata hivyo, kama ilivyo vitu vingi vinavyohusiana na mwili wa binadamu ushahidi mpya unaonesha kuwa kinga mwili ya mjamzito hupanda kipindi cha ujauzito, na wakati mwingine huwa ni ya kubadilika badilika.

Mabadiliko haya ya kinga ya mwili kipindi cha ujauzito ni muhimu kwa ajili ya kumpa nafasi mtoto anayeendelea kukua katika hatua tofauti za ujauzito. Kwa mfano katika hatua za kwanza za ujauzito kinga ya mwili inabadilika ili kuruhusu upandikizaji katika mwili. Wakati mwingine mfumo wa kinga unahitaji kujirekebisha katika njia tofauti, mfano mzuri ni wakati mwili wa mwanamke unajiandaa kupata uchungu wa kujifungua.

Jambo la muhimu katika maelezo yote haya ni kwamba kuwa na mfumo wa kinga wenye kubadilika badilika inakuweka katika hatari kubwa ya matatizo ya Virusi vya Corona kama vile shida katika upumuaji na hata homa ya mapafu (pneumonia).

Kitu cha kwanza cha kutiliwa mkazo ni wanawake wajawazito waendelee kuhudhuria miadi yao ya kliniki katika hospitali isipokuwa kama wameambiwa vinginevyo na mkunga au daktari wao.

Kwa sasa hakuna sababu ya kubadilisha mpango wako wa kujifungua, kama uliandaa hapo awali. Mpango wa kujifungua unahusisha mahali unapotarajia kujifungulia (hospitali, zahanati, kituo cha afya, au nyumbani) na aina gani ya dawa za maumivu unatarajia kupata.

Walakini, ikiwa umeonekana na dalili zinazoashiria maambukizi ya Virusi vya Corona, kama kikohozi kikavu au joto kubwa la mwili, kubanwa kifua na kupumua kwa shida,  ni lazima ujitenge (self-isolation) na wasiliana na daktari au mkunga wako haraka.

Vilevile, kwa wanawake wajawazito wenye matatizo mengine ya kiafya wanahitaji kuwa makini zaidi na kukaa mbali na mikusanyiko ya watu ikiwezekana kufikiria kujitenga (self-isolation) kipindi cha ujauzito. Wanawake waliopata ugonjwa wa kisukari, aina ya ugonjwa wa kisukari ambayo ni matokeo ya ujauzito ijulikanayo “Ugonjwa wa Kisukari kipindi cha Ujauzito” (gestational diabetes), wanatakiwa kuchukua tahadhari na kupunguza migusano na watu.

Kuwa mgonjwa wa kisukari wakati wa ujauzito ni kundi la hatari hata bila kupata Virusi vya Corona, kwasababu ugonjwa huu wa kisukari unaongeza ugumu wakati wa ujauzito na kujifungua. Zaidi ya hapo, viwango vikubwa vya sukari katika damu kwa mda mrefu bila kutibiwa na kuangaliwa vizuri vinaweza kudhoofisha mfumo wa kinga zaidi.

Kutokana na mfumo wa kinga unaobadilika kila hatua wakati wa ujauzito ni vizuri wanawake wasio na matatizo ya kiafya kuchukua tahadhari na kukaa mbali na watu pale inapobidi.

Kama ilivyo wajawazito wengi wanaishi na wenzi wao au mara nyingine mtoto/watoto wao wengine, ushauri huu ni vizuri kufuatwa ili kupunguza nafasi ya kuweka afya ya mama mjamzito katika hatari ya kupata maambukizi ya Virusi vya Corona.

Tahadhari hizo ni pamoja na kufanya kazi ukiwa nyumbani kwa wale wanaoweza, kataa mgusano wa aina yeyote na watu na epuka sehemu za mikusanyiko.

Mwisho kabisa, ili kuwasaidia wajawazito kuwa na ujauzito wenye afya na kinga ya mwili nzuri katika kipindi hiki, ni vizuri kuzingatia mlo bora wenye madini chuma kwa wingi (kama mboga za majani zenye kijani kilichokolea, samaki na mayai) na madini ya foliki ambayo yanapatikana kwenye maharage, kunde, maharage ya kijani n.k. Bila kusahau vidonge vya vitamini vya kila siku ulivyoandikiwa na daktari wako vinasaidia pia.

Je, ninaweza kumpatia mtoto wangu Virusi vya Corona?

Je, kuna uwezekano wa mama mjamzito aliyepata maambukizi ya Virusi vya Corona kumpatia mtoto anayeendelea kukua ndani ya mwili wake?  Hili ni moja ya swali linalowaumiza wajawazito wengi na familia zao.

Ukweli ni kwamba kuna maambukizi mengi ya virusi, bakteria na fangasi ambayo yanaweza kupatiwa mtoto kipindi cha ujauzito, kama vile Virusi vya Ukimwi, Homa ya Manjano, Tetekuwanga, Rubela na Toxoplasmosis (maambukizi yanayosababishwa kwa kula nyama isiyopikwa vizuri na iliyogusana na kinyesi cha paka).

Hakuna ushahidi unaoonyesha Virusi vya Corona vinaweza kumpata mtoto aliye tumboni kama mama mjamzito anayo maambukizi. Ila kwa sababu virusi hivi ni vipya wanasayansi wanaendelea kuusoma ugonjwa huu taratibu na tutegemee taarifa zaidi hapo mbeleni.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la kujitegemea la Kidaktari liitwalo “The Lancet” ambalo liliwafuatilia wanawake 9 waliopatikana na maambukizi ya virusi hivi baada ya kufanyiwa vipimo nchini China, waligundua hakuna mtoto hata mmoja aliyezaliwa na maambukizi haya (ikumbukwe wanawake hawa wote walijifungua kwa njia ya upasuaji). Ijapokuwa idadi ni ndogo ila inatia matumaini.

Pia hakuna ushahidi ulioonyesha kulikuwa na virusi ndani ya kimiminika cha amnion “Amniotic fluid” hichi ni kimiminika kinachomzunguka na kumlinda mtoto wakati wa ujauzito. Pia hakuna ushaidi uliopatikana ndani ya sampuli za damu zilizochukuliwa kutoka katika kitovu cha kila mtoto. Hali hii inaweza kupendekeza kujifungua kwa njia ya kawaida kwa mjamzito aliye na maambukizi ni njia salama, lakini hatuna majibu ya uhakika kuhusu hili kwasababu idadi ya tafiti zilizofanywa ni ndogo sana.

Kwa tafiti zote hizi inaonyesha kuna ushahidi kidogo kuwa watoto wanaweza kupata maambukizi ya virusi hivi kutoka kwa mama zao wakati wa ujauzito.

Je, ninaweza kumpatia mtoto wangu maambukizi kwa njia ya kunyonyesha?

Hakuna uwazi wa kutosha katika suala la maziwa ya mama, hata hivyo hatuwezi fanya hitimisho kama maziwa ya mama yanabeba virusi au la!

Baadhi ya virusi, kama virusi vya UKIMWI vinajulikana kuenezwa kwa njia ya maziwa ya mama, lakini mpaka tulipofikia hakuna ushahidi kuwa Virusi vya Corona COVID-19 vinaweza kuenezwa kwa njia hii pia.

Ushauri uliopo ni kuwa wamama ambao hawana maambukizi haya waendelee kuwanyonyesha watoto wao ila wakumbuke kunawa mikono yao vizuri kabla na baada ya kuwanyonyesha.

Ikiwa mama ataonekana na dalili za kukohoa au joto kubwa la mwili, ni vizuri atumie njia mbadala ya kunyonyesha (mf: vifaa maalumu vya kukamua maziwa) na kumpatia mtu mwingine asiye na maambukizi kumlisha mtoto mpaka atakapo pona.

Kuna ushahidi wa kutosha kuwa maziwa ya mama ni mazuri kwa kuongeza kinga mwili ya mtoto, hivyo kusitisha moja kwa moja kumnyonyesha mtoto wako kunaweza kumuweka katika  hatari ya kupata maambukizi kwa urahisi.

Kadiri muda unavyokwenda, haitaepukika na tutarajie kushuhudia wanawake wengi wajawazito wakipata virusi vya corona COVID-19, hii itapelekea wanasayansi kuweza kutambua zaidi jinsi kirusi hiki kinafanya kazi na ni kwa namna gani kinamuathiri mjamzito. Kwa sasa kuchukua hatua za kujikinga ni muhimu – kuosha mikono kwa maji tiririka, kuepuka kukaa karibu karibu sana ikiwemo kuepuka maeneo yenye mikusanyiko ya watoto, kukaa nyumbani, kuepuka wageni ni njia zinazohitaji kufuatwa kuweza kuwa salama.

 

IMEPITIWA: 19 MARCH 2020

 

 

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.