Kama mama, lengo kuu ni mtoto wako kuzaliwa akiwa mwenye afya na salama. Hata kama, inabidi upasuaji kufanyika, ili kumleta kiumbe wako mzuri duniani.
Wakati huohuo, ni jitihada zinazoeleweka kujaribu kila kitu ili kuhakikisha mshono unapona vizuri na kovu linaonekana kwa mbali sana.
Nini cha kufanya ili mshono upone vizuri?
- Usafi. Jitahidi kuhakikisha sehemu ya mshono inasafishwa vizuri mara moja kwa siku kwa maji na sabuni. Hakuna haja ya kuumwagia mshono maji kila mara na epuka kusugua kwa nguvu. Unapomaliza kusafisha, kausha taratibu kwa taulo.
- Tumia mafuta. Baadhi ya madaktari wanasema ni vizuri kupaka mafuta ya mgando kisha kukifunika kidonda na kitambaa safi au bandeji bila kukaza; madaktari wengine wanasema ni vizuri kutopaka chochote na kuacha mshono wazi. Ni vizuri ukiongea na daktari wako au mkunga aliyehusika katika upasuaji wako kuhusu njia ipi ni nzuri kwa mshono wako.
- Ruhusu hewa kwenye eneo la mshono. Wakati wa usiku vaa gauni linaloachia itasaidia sana hewa kuzunguka, kwasababu hewa inahamasisha uponaji wa majeraha katika ngozi.
- Hudhuria miadi yako na daktari. Hakikisha nyuzi zinatolewa kwa wakati ili kuepusha kovu baya kutokea. Hivyo kabla ya kuondoka hospitali hakikisha unakumbuka kumuuliza mkunga wako au daktari tarehe ya kurudi kutolewa nyuzi.
- Epuka mazoezi kwa muda. Itakubidi kupunguza mazoezi ili kuruhusu majeraha katika uterasi na tumbo kupona. Hivyo epuka kuinama au kugeuza mwili ghafla, vilevile usinyanyue kitu chochote kizito zaidi ya mtoto wako. Inashauriwa kusubiri daktari akuruhusu kama ni salama kuanza mazoezi.
- Tembea kila uwezapo. Jitahidi kutembea, inasaidia kuongeza mzunguko wa damu, inasaidia pia kuponya jeraha na kupunguza nafasi ya damu kuganda kwenye mishipa ya miguu au ogani za nyonga, hali ambayo inawapata wamama waliotoka kujifungua. Pale unapoona unaweza kutembea mbebe mwanao kwenye kigari chake (kama unacho) au mfunge mtoto mbeleko kwa mbele kisha fanya matembezi jioni karibu na nyumbani kwako au kuzunguka nyumba yako.
Ishara kuwa mshono wako umepata maambukizi.
Maambukizi haya husababishwa bakteria katika eneo la mshono baada ya upasuaji. Ikiwa unapitia dalili zifuatazo, wasiliana na daktari wako mara moja:
- Uwekundu au kuvimba eneo la mshono au ngozi kuzunguka eneo hilo.
- Homa kali zaidi ya (100.4˚F)
- Harufu mbaya kutoka kwenye mshono
- Kuvuja au majimji kuzunguka mshono
- Usaha kutungika katika mshono
- Kidonda kuwa kigumu au kusikia ongezeko la maumivu kuzunguka kidonda.
- Maumivu katika sehemu moja ya mshono (kumbuka kuwa wiki za awali baada ya upasuaji maumivu ni kawaida, lakini pia usipuuzie kama eneo moja tu la mshono linakupa maumivu makali)
- Mshono kuachia.
- Maumivu wakati wa kukojoa
- Uchafu wenye harufu mbaya kutoka ukeni
- Miguu kuvimba au kuuma
- Kutokwa damu inayojaza pedi ndani ya lisaa. Wakati mwingine damu inayotoka inakuwa mapande ya damu (damu iliyoganda).
Hali Hatari Zinazosababisha Maambukizi Katika Mshono Baada ya Upasuaji.
Baadhi ya wanawake wako katika nafasi ya kupata maambukizi ya bakteria katika eneo la mshono kwa sababu zifuatazo:
- Unene uliopitiliza
- Ugonjwa wa kisukari au dosari yeyote katika kinga ya mwili, (mfano HIV)
- Matumizi ya mda mrefu ya steroidi
- “Chorioamnionitis”- maambukizo ya bakteria ya papo kwa hapo yanayoathiri utando wa nje, amnion na maji ya amniotic. Hutokea wakati wa ujauzito au uchungu, bila kutibiwa mapema husababisha maambukizo mazito kwa mama na mtoto.
- Kutohudhuria miadi ya kliniki (mara chache)
- Kujifungua kwa upasuaji ujauzito zilizopita
- Ukosefu wa dawa ya tahadhari kabla ya kuchanwa
- Uchungu au upasuaji uliochukua wa mda mrefu
- Upotevu mkubwa wa damu wakati wa uchungu, kuzaa au upasuaji
Maambukizi katika eneo la mshono baada ya upasuaji hutibiwa kwa antibaotiki zinazotolewa hospitali, daktari atakuandikia nyingine upate kurudi nazo nyumbani. Daktari atafungua mshono wako kama ulianza kutoa usaha, kisha atatoa usaha wote. Baada ya kusafisha vizuri daktari ataepusha usaha kujikusanya kwa kuweka kitambaa safi chenye antiseptiki ili kuzuia ukuaji wa bakteria katika mshono. Kidonda kinahitajika kuangaliwa mara kwa mara ili kuhakikisha kinapoa vizuri.
Baada ya siku kadhaa za matibabu ya antibaotiki na daktari kuangalia mshono mara kwa mara, kidonda kitaanza kujifunga vizuri au kupona chenyewe.
Jinsi Gani ya Kuzuia Maambukizi ya Mshono Baada ya Upasuaji
Baadhi ya maambukizi katika mshono hayaepukiki. Lakini ikiwa ulifanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua, unaweza chukua hatua kupunguza nafasi ya kupata maambukizi tena, baadhi ya hatua hizo ni pamoja na:
- Tumia dawa ulizoandikiwa na fuata maelekezo ya kuangalia kidonda yaliyotolewa na daktari au mkunga, ikiwa una swali usisite kuwasiliana na daktari.
- Kama umepewa dawa za kutumia kutibu au kuzuia maambukizi, hakikisha unatumia dozi nzima bila kuruka au kuacha kuzitumia kipindi kizima cha matibabu.
- Safisha kidonda chako na badili vitambaa vinavyofunga kidonda mara kwa mara.
- Usivae nguo zinazobana au kupaka losheni juu ya kidonda.
- Omba ushauri jinsi gani ya kumpakata mtoto wakati wa kumnyonyesha ili kuepuka mgandamizo mbaya katika kidonda.
- Angalia joto la mwili wako mara kwa mara, tafuta msaada wa kitiba ikiwa jotoridi lako ni zaidi ya 100˚F (37.7˚C)
KUMBUKA
Kama bado haujajifungua kwa upasuaji, hizi ni hatua unazotakiwa kuchukua:
- Dumisha uzito wenye afya. Kama wewe sio mjamzito, fanya mazoezi na kula mlo wenye afya ili kuepuka uzito uliopitiliza (kiribatumbo) ukiwa mjamzito.
- Chagua kujifungua kwa njia ya kawaida kama inawezekana. Wanawake wanaojifungua kwa njia ya kawaida hawana nafasi ya kupata maambukizi baada ya kujifungua.
- Jitahidi kutibu hali yeyote inayoleta dosari katika kinga ya mwili kabla ya kushika mimba. Ni salama kwako na mtoto ikiwa utatibu aina yeyote ya maambukizi au ugonjwa kabla ya kushika ujauzito.
Maambukizi katika eneo la mshono yanayosababishwa na bakteria baada ya upasuaji yanaweza sababisha matatizo makubwa kama: uharibifu wa tishu zenye afya katika ngozi, mshono kuachia na utokaji wa kinyesi baada ya mshono kuachia. Ikiwa mama atapata matatizo haya, upasuaji wa kurekebisha utafanyika. Inaweza kuchukua mda mrefu kupona, kwa wachache inaweza kusababisha kifo.
IMEPITIWA: AGUSTI, 2021.