Ukurutu mweupe kichwani ni dalili ya kawaida kwa watoto wachanga. Mtoto wako anaweza akawa ana tatizo dogo tu la ngozi kavu iliyobabuka na kuonekana kama ukurutu au mba au akawa na tatizo kubwa akionekana kuwa na uteute wa njano, mzito, wenye mafuta mafuta na kukatika katika.
Ukurutu huu huweza kutokea wiki mbili hadi miezi mitatu baada ya kuzaliwa na hupotea wenyewe baada ya miezi kadhaa. Mara nyingi huwa sio tatizo baada ya miezi 6 hadi 7. Hakikisha mtaalamu wa afya anamuangalia mtoto wako kama ana tatizo hili. Ukurutu kichwani hutokea pale tezi zinazotengeneza mafuta (sebaceous glands) zinatengeneza mafuta mengi zaidi ambayo baadae hukauka na kubabuka babuka. Wataalamu wengi wanaamini kwamba zile homoni za ziada ambazo mama mjamzito alikuwa anazitoa zilisafiri hadi kwa mtoto wake wakati wa kujifungua na kuziamsha tezi za mtoto kutengeneza mafuta zaidi. Miezi michache baada ya homoni za mtoto wako kuwiana tatizo hili litatoweka.
Njia rahisi kuondoa ukurutu huu ni kwa kuosha nywele za mtoto wako kila siku kwa sabuni zinazoshauriwa kuosha nywele za mtoto. Jaribu kusugua ukurutu huu kwa mikono yako au nguo laini ya kuogeshea watoto kuulainisha ukurutu huu. Kabla ya kuzisuuza nywele zake, mchane kwa kitana laini kuondoa ukurutu uliozidi ndio umsuuze.