Ujauzito Wiki ya 20

Jinsi mtoto wako anavyokua katika wiki ya ishirini
Wiki hii, ute ute mweupe unaoitwa “vermix caseosa” umeanza kumfunika mtoto wako. Hii itatumika kutunza ngozi ya mtoto wako kwa kipindi chote atakachokuwa anaelea kwenye maji ya uzazi “amniotic fluid”.

Dalili za ujauzito katika wiki ya ishirini
Je unaishiwa na nguvu baada ya kutembea umbali mdogo au kupanda ngazi? Kuhema juu juu “breathlessness” ni kawaida kipindi cha ujauzito. Inatokea kwa sababu ukuta wako wa kifua unatanuka zaidi kuweza kuyapa mapafu yako uwezo mkubwa wa kubeba hewa, hivyo kuufanya mwili wako kuipata na kuitumia oksigeni kwa urahisi. Hii inamaanisha kila pumzi unayovuta inakuwa ni ya ujazo mkubwa kuliko ulivyokuwa kabla ya ujauzito. Ni hali hii ndio inakufanya ujisikie kuishiwa pumzi au kuhema juu juu. Kama hali hii itaambatana na kusikia kizunguzungu au kuona marue rue ni vyema kumuona daktari mara moja.

Unachotakiwa kufahamu kwenye ujauzito wiki ya ishirini
Utakuwa umeshafanya kipimo cha ultrasound mpaka kufikia sasa. Umuhimu wa skani hii ni kuangalia kwamba mtoto anakua na kuendelea vizuri kadiri inavyotegemewa. Mtaalamu wa skani atampima mtoto wako na kuangalia ukuaji na ufanyaji kazi wa viungo vyake upo sawasawa. Pia ataangalia kama mtoto wako ana magonjwa ya tangu tumboni kama mdomo sungura na matatizo ya moyo.

Mtaalamu ataweza kukuonesha uso, mikono, miguu na hata moyo wa mtoto wako kwenye skani. Inawezekana akakupatia pia picha ya kuondoka nayo nyumbani. Hii inategemea na kituo cha afya unachohudhuria. Kama ungependa kujua utapata mtoto wa kiume au wa kike mtaalamu anaweza akakuambia baada ya skani kumalizika.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.