Uhitaji na Utaratibu wa Kuanzishiwa Uchungu

Kuna sababu kadhaa zinazoweza kusababisha kuanzishiwa uchungu kuwa lazima. Uchungu utatakiwa kuanzishwa iwapo:

  1. Umepitiliza siku yako ya kujifungua, mara nyingi utaanzishiwa uchungu kati ya wiki ya 41 na 42
  2. Chupa imevunjika lakini uchungu haujaanza
  3. Una kisukari; mara nyingi huanzishiwa uchungu mara tu baada ya wiki 38
  4. Umepata shinikizo la damu la mimba (pre-eclampsia)
  5. Una utokaji wa damu usio wa kawaida
  6. Mtoto wako ametambulika kuwa amechoka tayari
  7. Mrija wa chakula wa uzazi (placenta) kushindwa kupeleka chakula na oksigeni kwa mtoto
  8. Unategemea kujifungua mapacha na daktari wako ameshauri uanzishiwe uchungu

 

Kama unafikiria ni kwa namna gani utafanikiwa kujifungua kwa kawaida, basi kuna vidokezo kadhaa vya kuzingatia:

  1. Achana kabisa na sigara, pombe na madawa yoyote kipindi chote cha ujauzito wako
  2. Mara zote wasiliana na daktari wako kabla ya kutumia dawa ya aina yoyote
  3. Hudhuria kliniki mara kwa mara
  4. Kula mlo bora na kamili
  5. Fanya mazoezi mara kwa mara
  6. Muone daktari mara moja pale unapopata dalili hatarishi au usiyoielewa

Kumbuka msaada wa kitaalamu wa kukupa uchungu ukihitajika haimaanishi kwamba kuna kitu ulikosea katika ujauzito wako. Wanawake wengi wanakuwa na ujauzito wenye afya kabisa lakini wanakuja kuhitaji kuanzishiwa uchungu wakati wa kujifungua. Kwa makadirio mwanamke mmoja kati ya watatu atahitaji msaada wa kitaalamu wakati wa kujifungua.

 

Kuanzishiwa uchungu kunaweza kufanyika kwa njia mbali mbali, ikiwemo:

 

  1. Kutenganisha nyavunyavu (membrane sweep): Moja ya njia maarufu za kuanzishiwa uchungu. Wakati wa tukio hili daktari au mkunga wako atatenganisha nyavunyavu nyembamba zilizozunguka kichwa cha mtoto wako kutoka kwenye mlango wa uzazi. Ni kawaida kwa kitendo hiki kurudiwa mara kwa mara.
  2. Prostaglandini: Homoni hii ya kutengeneza maabara inayopatikana kama kimiminika laini au kidonge huingizwa ukeni. Homoni hii husaidia kuivisha mlango wako wa uzazi ili uweze kufunguka na kutanuka kiurahisi. Inaweza ikahitajika kuwekewa dozi kadhaa mpaka ianze kufanya kazi sawasawa.
  3. AROM (Artificial rupture of membranes) – Kupasua chupa: Njia hii inahusisha kupasua chupa yako kwa kukusudia. Njia hii ilikuwa ndio njia maarufu zamani lakini kwa sasa inatumika zaidi kuharakisha uchungu kuliko kuanzisha uchungu.
  4. Syntocinon: Hii ni kama homoni ya oksitosini iliyotengenezwa maabara. Husaidia kukuharakishia kupata uchungu. Hutumiwa zaidi pale njia ya kutenganisha nyavunyavu (membrane sweep) pamoja na kutumia homoni ya Prostaglandini zote zimeshindwa kufanya kazi. Dawa hii hutolewa kwa dripu.
  5. Kuanzishiwa uchungu kwa njia ya kawaida: Oksitosini ni homoni ambayo inahusishwa moja kwa moja na uchungu. Homoni hii pia huwa inatolewa pale matiti yanapoguswa guswa, kunyonywa n.k. Hivyo basi kwa miaka mingi inafahamika kwamba kufanya mapenzi pia ni njia ya kawaida kabisa inayoweza kukuanzishia uchungu.

 

Kama taratibu za kukuanzishia uchungu zote hazitafanikiwa, basi itabidi ujifungue kwa upasuaji kadiri itakavyoonekana ni muhimu kiafya. Lakini, wanawake wengi wameanzishiwa uchungu na wakaweza kupata uchungu na kujifungua kawaida.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.