Fikiria hauna njia nyingine ya kuwasiliana na watu wa karibu yako. Uko katika ulimwengu mpya uliozungukwa na watu wanaoonekana wanakupenda na kukujali, ila hawazungumzi lugha yako na hawaelewi unachowaza au unachohisi. Na fikiria kuwa unawategemea hao watu kukutimizia haja zako,hauwezi kujilisha au kufanya chochote. Utafanya nini kujaribu kueleza unachohitaji? Kusema ukweli, unaweza ukalia.
Na hichi ndio kitu ambacho watoto wanafanya. Huwa wanalia kwa sababu mbalimbali zinazohusisha wao kutaka au kuhitaji kitu fulani. Kwa mfano mtoto wako anaweza kulia kwa sababu zifuatazo:
- Ana njaa
- Anataka kubebwa
- Anajisikia mchovu
- Amechoka (bored)
- Nepi yake ina mkojo
- Anasikia joto sana au baridi sana
- Anataka tu umkumbatie
Kwa kila sababu mojawapo inayosababisha mtoto wako alie, kuna jambo wewe na mwenza wako mnaweza kufanya. Ukichukua muda wa kutosha kuwa na mtoto wako, wewe kama mzazi utaanza kuwa na uwezo wa kugundua mahitaji mbali mbali ya mtoto wako yanayomfanya alie. Njaa inawezekana ikawa ndio sababu kubwa ya vilio vingi vya watoto. Kama mzazi unatakiwa kujua na mda gani mtoto amekula mara ya mwisho na alikula kiasi gani. Hii itakusaidia kutambua kama njaa ndio sababu ya kilio husika. Vile vile ni vyema kuangalia nepi ya mtoto kama bado ipo safi na kavu akianza kulia kwani wakati mwingine ni nepi yenye unyevu nyevu wa mkojo au choo cha mtoto ndio humfanya alie akiomba msaada kwani hali ile inamkera.
Ki ukweli kuna wakati mwingine watoto wanaweza wakalia na tukashindwa kujua sababu ya kulia kwao. Hii hutokea sana sana kwenye ile miezi minne toka kuzaliwa, akiwa na vipindi ambavyo hulia na kama mzazi huwa unakosa suluhisho. Unaweza ukajitahidi kila njia kumbembeleza bila mafanikio. Watoto wadogo pia wanaweza wakawa na siku mbaya kama wewe. Mtoto anaweza akawa na hisia za huzuni, anaweza akawa mpole, mwenye hasira, anaota meno au hajisikii vizuri, na wakati mwingine, mtoto anaweza tu akaamua kulia.
Jua kwamba, pamoja na kwamba huwezi kugundua sababu kwanini mtoto wako analia, haimaanishi kwamba kuna kitu unakosea. Wakati mwingine watoto hulia tuu.
Lakini, kama mtoto wako analia kuliko kawaida, au kama anatoa kilio cha sauti ya juu sana, muone daktari. Unajua utaratibu wa mtoto wako vizuri kuliko mtu mwingine, hivyo kama ukiona lolote la tofauti kama kilio hafifu, kunong`ona kama analia, kubadilika kwa muda na wakati wa kilio, au kama inaonekana kana kwamba mtoto wako yupo kwenye maumivu usisite kuwasiliana na daktari. Kilio cha ghafla kikifuatiwa na ukimya wa muda mfupi halafu kilio kikaendelea zaidi huashiria maumivu.