Kipindi hiki tofauti na zamani kumekuwa na njia mbali mbali za kujifungua. Hii intokana na maendeleo ya teknolojia na uwepo wa wataalamu mpaka kwenye vituo vya chini kabisa vya afya. Hali hii imesaidia kupunguza kwa kasi vifo vya mama na mtoto. Zifuatazo ni njia mbalimbali zinazotumika kujifungua. Ni vyema kuzitambua na kuzielewa mapema ili uweze kufahamu mapema ni njia gani ambayo itatumika wakati wa kujifungua kwako.
Ukweli Unaotakiwa Kujua Kuhusu Njia za Kujifungua
- Chaguo zilizopo wakati wa kujifungua ni pamoja na: kujifungua bila msaada (kawaida), kujifungua kwa msaada na kujifungua kwa upasuaji.
- Unaweza kujifungulia nyumbani, zahanati/kituo cha afya au hospitalini.
- Kujifungua kwa njia ya kawaida bila dawa hakuna maumivu, ni rahisi kama mama atajifunza mbinu za kupumua wakati wa kusukuma mtoto katika chumba cha kujifungulia.
- Katika kuhakikisha njia gani ni sahihi kwa mama wakati wa kujifungua upimaji wa faida na hasara za njia hiyo uende sambamba na pendekezo la mjamzito ambalo ni salama kwake.
- Kila mwanamke ana uzoefu wa kipekee wakati wa kujifungua, wnaawake wengi wanakiri wakati wa kuzaa mtoto kuna amabatana na maumivu. Hata hivyo, maumivu hay ani ya mada mfupi, zipo aina na njia madhubutu za kupunguza ukali wa maumivu wakati wa kujifungua.
Kujifungua kwa Njia ya Kawaida (Kujifungua Bila Msaada- Unassisted birth)
Kujifungua kwa njia ya kawaida
Wewe na familia yako mnaweza kubaini ishara za kawaida za uchungu. Mwanamke anaweza kujifungua siku kadhaa au hata wiki kadhaa kabla au baada ya tarehe iliyotarajiwa, kulingana na tarehe ya kipindi cha mwisho cha hedhi ya kawaida. Mwanamke anapofahamu maana ya uchungu, ataweza kufahamu kitakachotokea. Ufahamu huu humsaidia kutulia zaidi na kuwa na ujasiri katika siku au wiki za mwisho za ujauzito.
Yafahamu maagizo dhahiri ya jambo la kufanya pale uchungu unapoanza (kwa mfano ikiwa utakuwa na maumivu ya mkakamao wa misuli ya fumbatio ya tumbo la uzazi au kuvuja kwa kilowevu cha amniotiki, maarufu kama kupasuka chupa). Hakikisha kuwa kuna mtu atakaye mwita mkunga au mtaalamu mwingine ili kukuzalisha haraka iwezekanavyo.
Mkunga wako anafaa kuzingatia maandalizi ya kujifungua na:
- Kuheshimu chaguo la mama. Anapaswa kumpa mama habari zote zinazohitajika kuhusu uzalishaji safi na salama, lakini hatimaye anapaswa kuheshimu chaguo lake kuhusu mahali pa kujifungulia na mtu angelipenda kuandamana naye.
- Kukusaidia kutambua mahali pa kupata usaidizi wakati wa kujifungua na kipindi cha baada ya kujifungua kinachofuata punde.
- Kupangia gharama yoyote ya ziada inayohusiana na kujifungua kwako.
- Kutayarisha vifaa vya kumtunza mama na mtoto wake atakayezaliwa.
Faida za Kujifungua kwa Njia ya Kawaida
- Watoto wanaozaliwa kwa njia ya kawaida wanakuwa na matatizo madogo ya upumuaji.
- Mama anapona haraka na kuepuka aina yeyote ya matatizo yanayohusiana na upasuaji kama vile uchanwaji wa utumbo au ogani za eneo la tumbo wakati wa upasuaji.
- Njia hii ya kujifungua ina kiasi kidogo cha maambukizi na ukaaji mfupi hospitali au kituo cha afya.
Hasara za Kujifungua kwa Kawaida
- Kuchanwa eneo kati ya njia ya haja kubwa na uke.
Njia za kujifungua kwa Msaada (Assisted Births)
Kujifungua kwa njia ya kawaida kwa msaada wa vifaa maalumu
Vifaa hivi huwasaidia akina mama na watoto pale watoto wanapotakiwa kuzaliwa haraka. Ni zana muhimu sana kwa mtu mwenye ujuzi wa kuzitumia.
Kifaa cha kunyonyea cha utupu (vacuum extractor) ni kifuniko kidogo cha kunyonyea ambacho hutosha kwenye kichwa cha mtoto kinachotokeza angali akiwa ndani ya uke. Hewa hujazwa ndani ya kile kifuniko ili kiweze kushikilia vizuri ngozi ya kichwa cha mtoto wakati mtaalam anapokivuta. Utaratibu huu unaweza kusababisha damu kuganda kwenye kichwa cha mtoto, kitaalam inaitwa (cephalohematoma)
Koleo hufanana na mikasi mirefu yenye bawaba ambayo mwishoni imejikunja ili kutosha kwenye kichwa cha mtoto. Kifaa hiki kinaweza kuleta madhara makubwa sana kwa watoto na mama vikitumiwa vibaya au vkitumiwa na mtu asiye na ujuzi.
Matumizi ya kifaa cha kunyonyea (vacuum-cup) yameongezeka. Sababu tatu zilizosababisha ongezeko la matumizi ya vifaa hivi ni kwasababu ya:
- Ongezeko la matumizi ya dawa ya usingizi ya epidural, ambayo hurefusha hatua ya kusukuma
- Muda maalum wa kusukuma uliotengwa kwa wanawake katika baadhi ya hospitali
- Jitihada za hospitali kupunguza uwezekano wa kufanyiwa upasuaji.
Kifaa cha kunyonyea (vacuum-cup) mara nyingi hutumiwa pamoja na dawa ya ganzi ya mgongoni (epidural) kwa sababu ganzi huzuia hisia za kusukuma. Kama ulipewa dawa ya ganzi ya mgongoni (epidural), vuta subira mpaka mlango wa kizazi utakapokuwa umeshatanuka vya kutosha. Unaweza pia ukaongeza uwezekano wa kuepuka kujifungua kwa kutumia vifaa hivi au kwa upasuaji kwa kutoanza kusukuma haraka mpaka pale mlango wako wa kizazi unapokuwa umekamilika kutanuka. Kama utasubiri mpaka utakapohisi hali ya kusukuma, au kichwa cha mtoto wako kimezidi kutokeza,utakuwa na nguvu zaidi na unaweza kusukuma vizuri zaidi.
Kabla ya kutumia njia hii kama hakuna dharura yoyote, kaa mikao tofauti ambayo itasaidia kufungua nyonga zako. Jaribu kuchuchumaa au kutekenya chuchu ili kuongeza nguvu uchungu na kupata nguvu zaidi ya kusukuma.
Kuchanwa eneo kati ya uke na njia ya haja ndogo (Episiotomy). Hii ni aina nyingine ya kujifungua kwa njia ya kawaida kwa msaada ambapo madaktari watafanya utaratibu huu ikiwa wanataka kumtoa mtoto haraka.
Kitendo cha kupasua chupa ya maji ya uchungu (Amniotomy). Daktari kifaa maalum chenye muonekano wa ndoana (plastiki) kutengeneza uwazi katika “amniotic sac”.
Kuanzishiwa uchungu (Induced labor)-hali hii inatokea pale daktari anapokuanzishia uchungu kabla haujaanza wenyewe. Kitendo hichi kitapendekezwa ikiwa daktari ana wasiwasi na afya yako au mtoto wako.
Kujifungua kwa upasuaji mkubwa (Cesarean Section)
Kujifungua kwa njia ya upasuaji hutokea kwa sababu kadhaa. Kama mtoto ni mkubwa au mdogo sana, kama unajifungua mapema au baada ya muda wa kujifungua kupita, una umri mkubwa au ni mwoga sana, kuchoka sana kwa sababu ya ujauzito au kuchoka sana kwa sababu ya uchungu, kama una mapacha, kama mtoto alitanguliza makalio, au kama wakati uliopita alijifungua kwa upasuaji.
Kiwango cha watu wanaojifungua kwa njia ya upasuaji mkubwa kimeongezeka sana kwa kipindi cha miaka thelathini iliyopita. Kujifungua kwa upasuaji huhusisha upasuaji mkubwa wa tumbo. Lazima ufanyike hospitalini, mahali ambapo dawa ya nusu kaputi, dawa za kuua bakteria (antibiotiki), na damu ya akiba pia inapatikana. Kujifungua kwa upasuaji ni operesheni zinazookoa maisha wanapofanyiwa wanawake wenye matatizo fulani wakati wa kujifungua, ikiwa ni pamoja na matatizo ya kitovu (kamba ya kitovu kutangulia kichwa cha mtoto), kondo la nyuma linapoziba mlango wa uzazi (placenta previa), kondo la nyuma kushindwa kufanya kazi yake vizuri na kusababisha mtoto kushindwa kushuka kupitia kwenye fupa nyonga.
Kama unataka kujifungua kwa upasuaji mkubwa, utapelekwa kwenye chumba cha upasuaji, mahali ambapo utachomwa sindano ya dawa ya usingizi au utachomwa sindano ya ganzi kwenye uti wa mgongo (epidural) ili tumbo na miguu yako ife ganzi kabisa. Utaingiziwa Mpira wa kutolea mkojo ili kuhakikisha kibofu chako kinakuwa kitupu. Utaendelea kubaki macho. Kwa nadra sana wakati ambapo upasuaji unatakiwa ufanywe haraka sana, utachomwa sindano ya dawa ya nusu kaputi ili usinzie kwa sababu hufanya kazi kwa haraka zaidi kuliko ya uti wa mgongo (epidural).
Dawa ya nusu kaputi inapoanza kufanya kazi, daktari atakupasua kwa mlalo chini ya tumbo karibia kwenye kinena (Upasuaji wa wima hufanywa kwenye matukio ya dharura), upasuaji mwingine hufanyika tena kwenye misuli ya mlango wa kizazi ili kurahisisha mtoto kutoka. Halafu atamfyonza pua na mdomo mtoto wako, atakibana kitovu na kukikata na kuangalia upumuaji wa mtoto kama ni wa kawaida. Mambo yote yakienda vizuri, wewe na mwenzi wako mnaweza kumshikilia mtoto wenu wakati daktari akiendela kutoa kondo la nyuma na kushona kidonda. Utaratibu mzima huchukua muda wa saa moja. Kujifungua kwa upasuaji mkubwa kunaweza kuokoa maisha na kuboresha afya katika mazingira ya dharura, lakini sio kwamba ni njia ya kawaida tu ya kukimbilia kuchagua.
KUMBUKA
Vifaa vya kujifungua ambavyo mwanamke mjamzito na familia yake wanapaswa kushauriwa watayarishe kabla ya siku ya kujifungua ni:
- Nguo safi kabisa za mama kulalia na za kumpangusa mtoto mzawa na kumfunika
- Wembe mpya wa kukata kamba kitovu
- Uzi safi mpya wa kufungia kitovu au kibana kitovu maalumu
- Sabuni, kitambaa safi cha kusafishia na ikiwezekana, pombe tiba tiba ili kuepuka maambukizi
- Maji safi ya kunywa, kumwosha mama mikono na mikono yako.
- Ndoo tatu kubwa au bakuli.
- Vifaa vya kutengenezea vinywaji vya kuongeza maji mwilini au chai.
- Tochi ikiwa hakuna umeme katika eneo husika.
Kumbuka kuwa, matatizo yanayohusiana na ujauzito kama vile shinikizo la juu la damu na kuvuja damu yanaweza kutokea wakati wowote katika ujauzito, na ugonjwa wowote unaweza kutokea wakati wa ujauzito. Hali hizi zinapohisiwa katika awamu yoyote ya ujauzito, unapaswa kupatiwa rufaa mara moja na mkunga atakushauri kumuona au kutafuta huduma ya kitabibu haraka iwapo dalili za hatari zitaonekana.
Katika hali ya dharura
Hakikisha kuwa wewe na mwenza wako pamoja na watu wengine katika familia wanajua mahali pa kutafuta usaidizi.
- Fanya utaratibu wa usafiri
- Akiba ya pesa za usafiri, dawa na matibabu mengine.
- Nani ataandamana na wewe hadi kwenye kituo cha afya?
- Nani ataangalia familia wakati mama hayupo.
Mwanamke mjamzito anaweza kuvuja damu kwa wingi wakati wa kujifungua au baada ya kuzaa hivyo anaweza kuhitaji kuongezewa damu. Hakikisha kuwa wewe au mume wako mmewatambua watu wazima wawili wenye afya watakaokubali kukutolea damu ikiwa mama atahitaji. Na wasiliana na mtaalamu wa afya ili ahakikishe watu waliojitolea kutoa damu kuwa hawataathirika kwa kutoa damu, na kwamba afya yao kwa ujumla itakaguliwa kabla ya kutoa damu.
IMEPITIWA: SEPTEMBA, 2021.