Mtoto Miezi 6

Jinsi mtoto wako anavyokua

Miezi sita ni hatua nzuri kwani mtoto wako anaweza kuanza kula vyakula vigumu. Bado ataendelea kupata asilimia kubwa ya virutubisho vyake kwa kunyonya maziwa ya mama au kutumia maziwa ya formula, kwa hiyo usiwe na wasiwasi kama atakuwa hali sana mwanzoni. Jambo la kufurahia ni kujaribu vyakula mbali mbali tofauti kwa mtoto wako.

Unaweza ukaanza na vyakula laini laini na vyepesi, kama uji mwepesi na kumlisha kwa kijiko kidogo kisichoweza kumuumiza mdomo wake. Ni vyema ukamkalisha mtoto kwenye kiti cha kumlishia mtoto, ila kama kiti hakipo unaweza kumkalisha kwenye mapaja yako na kumlisha taratibu.

Kwa sasa mtoto wako ameshajifunza na kuitambua dunia karibia nusu mwaka sasa. Ameshapata ujuzi wa vitu mbalimbali. Inawezekana anaweza akakuiga ukisema au ukifanya kitu, kukutekenya, kujiviringisha kwenda mbele, ila anaweza asiweze kujirudisha kwa sasa.

Kama bado hajaanza, mtoto wako ataanza kusogea kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Unaweza kumuona anaanza kujivuta kwenda mbele kwa tumbo. Kujivuta huku ki komando komando inaashiria mtoto wako ataanza kutambaa karibuni.

Maisha yako: Lishe bora

Ni rahisi kujihusisha sana na nini anakula mtoto wako na kujisahau wewe mwenyewe. Lakini kula vizuri ni muhimu sana katika kipindi hiki kwani unahitaji nguvu za kutosha kuweza kumuhudumia mtoto wako.

Kuna sababu kwa nini mlo wa asubuhi unaonekana ni mlo muhimu kuliko yote katika siku. Mwili wako unahitaji kuamshwa vema asubuhi ili uweze kuzianza shughuli zako za siku. Mlo wa asubuhi ni muhimu sana kama ulipata usingizi wa kusuasua. Mlo wenye protini za kutosha kama mayai au uji wa ulezi utatosha kukupa nguvu inayohitajika kuzianza shughuli zako.

Unaweza ukawa unatamani kutokula mlo wa asubuhi ili upunguze uzito. Lakini tafiti zinasema kwamba watu wanaokula mlo wa asubuhi huwa wembamba kuliko wale wasiokula mlo wa asubuhi.

Jaribu kula mda sawasawa na mtoto wako. Hii inaweza ikawa ni ngumu mwanzoni, lakini mtoto kukuona wewe ukifurahia chakula chako kutamfanya na yeye ale zaidi.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.