Jinsi mtoto wako anavyokua
Uwezo wa mtoto wako kutumia lugha unaanza taratibu. Anaanza kuelewa sauti mbali mbali za lugha, na anaweza kuanza kusema “ma-ma” na “da-da” mwezi huu. Kujaribu kwake kuyatamka maneno haya ni juhudi sahihi za kuanza kujifunza kuongea. Usiwe mwenye huzuni kama mtoto wako ataanza kusema “da-da” kabla ya kuanza kusema “ma-ma”. Sauti za maneno haya hayana maana yoyote kwenye akili ya mtoto wako kwa sasa. Mtoto wako anaweza tu akawa anaona ni rahisi zaidi kusema “da-da” badala ya “ma-ma” au anaweza akawa amelisikia neon “da-da” mara kwa mara zaidi.
Unaweza ukawa na mawazo kama wakati umefika sasa kwa mtoto wako kuanza kutumia vyakula vigumu. Wataalamu wanasema bado ni mapema. Atapata kila kitu anachohitaji kutoka kwenye maziwa ya mama au maziwa ya formula mpaka atakapofikisha umri wa miezi sita. Hivyo hata kama ndugu, jamaa na marafiki wanaweza wakawa wanakushauri kuwa ni muda wa kumuanzishia vyakula vigumu mtoto wako, ni vyema kusubiri mpaka afikishe miezi sita kama muongozo wa kitaalamu unavyosema.
Mwezi huu hatua ya tatu ya chanjo kwa mtoto wako itahitajika kutolewa. Atachomwa sindano tatu kumlinda dhidi ya magonjwa hatari ambukizi kama dondakoo, tetanasi na maambukizi kwenye ubongo (meningitis).
Kama una wasi wasi kuhusu chanjo hizi na muda ambao mtoto wako anatakiwa azipate ni vyema kumuuliza mtaalamu wa afya akueleze zaidi.
Maisha yako: Kuanza kufanya mazoezi tena
Unaweza ukawa unajisikia kama upo tayari kuanza kuendelea na kufanya mazoezi. Inabidi uanze pole pole kwani haijapita muda mrefu tangu ujifungue. Mazoezi ya kujinyoosha (yoga) na kuogelea ni mazoezi mazuri kunyoosha na kuimarisha misuli yako muhimu.
Usifanye mazoezi ya kujitesa. Ijapokuwa ni vyema kiafya kufanya mazoezi, kurudia hali yako ya zamani itachukua muda pia. Fikiria mwili wako ulichukua muda gani kumtengeneza mtoto wako. Jiwekee muda sawa na huo huo kuweza kurudi katika umbo lako na uzito unaoutaka.