Habari njema ni kuwa mtoto wako anaendelea kukua. Maumivu makali katika mgongo kipindi hichi yanasababishwa na ukuaji wa mtoto tumboni.
Kumbuka sio wewe tu unayepitia hali hii,wajawazito wengi wanaanza kupatwa na hali hii mara nyingi kuanzia kipindi cha pili cha miezi mitatu ya ujauzito.
Makala hii itakupa nafasi ya kufahamu vidokezo vitakavyokusaidia kupunguza maumivu ya mgongo kipindi cha ujauzito.
Chanzo cha maumivu ya mgongo kwa mama wajawazito
Kawaida maumivu ya mgongo wakati wa ujauzito yanatokea sehemu ambayo nyonga na uti wa mgongo vinakutana (sacroiliac joint)
Maumivu ya mgongo yanachangiwa na mambo mengi. Zifuatazo ni sababu zinazoongeza nafasi ya maumivu ya mgongo kutokea kwa wajawazito:
- Kuongezeka uzito. Wakati wa ujauzito ambao ni salama, kawaida wanawake huongezeka uzito (kilo 11-16). Kazi ya kuhimili uzito huu inafanywa na uti wa mgongo. Hii inaweza kusababisha maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo. Uzito wa mtoto anayekua na uterasi vinasababisha mgandamizo kwenye mishipa na mirija ya damu inayopatikana katika nyonga na mgongo.
- Mabadiliko ya mkao. Uzani wa mtoto, uterasi na kiowevu cha amnioni hubadili mkao wak na kuweka mkazo kwenye mifupa na misuli ya mgongo wa mama mjamzito.Taratibu bila hata kujua utaanza kubadilisha mkao wako na jinsi unavyotembea,hali hii inaweza kusababisha maumivu ya mgongo.
- Mabadiliko ya homoni. Wakati wa ujauzito, mwili unatengeneza homoni iitwayo “relaxin” ambayo inaruhusu ligamenti katika nyonga kupumzika na viungo kulegea kwaajili ya maandalizi ya kujifungua. Homoni hii inasababisha ligamenti zinazosaidia uti wa mgongo kufanya kazi vizuri kulegea pia, hali hii inasababisha maumivu.
- Msongo wa mawazo. Msongo wa mawazo unaweza kusababisha mvutano wa misuli inayopatikana kwenye mgongo,hali hii inaweza kusababisha maumivu ya mgongo kwa mama mjamzito.
Matibabu kwaajili ya maumivu ya mgongo kwa mama mjamzito
Habari njema zaidi: maumivu ya mgongo yanaweza kupungua taratibu kabla ya kujifungua isipokuwa kama ulikuwa na matatizo ya kudumu ya mgongo kabla ya kubeba ujauzito.
Wakati huohuo, yapo mambo mengi unaweza kufanya kutibu sehemu ya chini ya mgongo wako au kupunguza maumivu haya:
- Kufanya mazoezi kila mara, mazoezi salama kwa mjamzito kama kutembea, kuogelea yanaweza kunyoosha misuli na kupunguza mvutano katika uti wa mgongo. Mkunga wako anaweza kukushauri mazoezi ya kunyoosha mgongo na fumbatio ambayo ni salama kwako na ujauzito wako.
- Tumia vitu vya baridi au joto kutuliza maumivu ya mgongo. Zungumza na mkunga au daktarin wako anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako kama ni salama kutumia njia hii. Unaweza kuanza kwa kuweka kitu cha baridi (mfuko wenye barafu au njegere zilizoganda) kwa dakika 20 eneo lenye maumivu. Baada ya siku mbili au tatu ukabadilisha na kuweka chupa ya plastiki au mpira maalumu wa maji ya moto eneo lenye maumivu. Kuwa makini usisababisha maumivu kwenye fumbatio wakati wa ujauzito.
- Imarisha mkao wako. Kuchechema kunaumiza uti wako wa mgongo. Hivyo basi, mkao mzuri wakati unafanya kazi, kaa kitako au kulala ni hatua nzuri. Kwa mfano, wakati wa kulala-lala kwa upande kwa msaada wa mto katikati ya magoti ili kutoa mkazo mgongoni. Ukiwa umekaa kwenye dawati ofisini, weka mto au taulo iliyoviringishwa vizuri nyuma ya mgongo wako kuupa msaada mgongo. Vilevile pumzisha miguu yako juu ya vitabu kadhaa ulivyovipanga au kigoda kisha kaa kwa kunyooka, mabega yako yakirudi nyuma. Ikiwezekana vaa mkanda maalumu unasaidia.
- Ushauri nasaha. Ikiwa maumivu yako ya mgongo yanahusiana na msongo wa mawazo, kuongea na rafiki yako unayemwamini au mshauri nasaha inaweza kukusaidia.
- Matibabu ya kutumia sindano(acupuncture) hii ni aina ya dawa kutoka China ambapo sindano nyembamba zinatumika kuchomwa kwenye ngozi katika maeneo fulani. Utafiti unaonyesha aina hii ya matibabu inaweza kutuliza maumivu ya mgongo wakati wa ujauzito. Ongea na daktari wako kama ni salama kwako na upatikanaje wake.
Vidokezo zaidi:
- Ikiwa unataka kuokota kitu chini, tumia miguu yako kuchuchumaa kuliko kuinama.
- Usivae viatu vyenye kisigino kirefu.
- Usilale kwa mgongo
Ikiwa maumivu yako yatazidi, ni busara zaidi kumuona dakatari, ili kuona kama kuna hatua nyingine inaweza kuchukuliwa. Hakikisha unapata maelekezo au ushauri kutoka kwa daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako kabla ya kutumia dawa yeyote kutumiza maumivu. Acetaminophen (Tylenol) ni salama kwa mama mjamzito. Dawa kama Asprin na dawa nyinginezo za maumivu kama ibuprofen (Advil,Motrin) au naproxen(Aleve) hazishauriwi kutumika kwa mama mjamzito.
Kwa baadhi ya wanawake, maumivu ya mgongo sio sababu pekee ya kuwasiliana au kumuona daktari. Lakini inakubidi umuone daktari haraka iwezekanavyo ikiwa utapata dalili zifuatazo:
- Maumivu makali sana
- Ongezeko la maumivu haya makali au maumivu yanayoanza ghafla.
- Shida kukojoa au kuhisi hali ya kuchomwa na pini au sindano kwenye mikono na miguu.
- Maumivu yanayofuatana katika fumbatio.
KUMBUKA
Katika hali nadra, maumivu makali ya mgongo yanaweza kuhusishwa na shida kama vile ugonjwa wa mifupa “osteoporosis”-hali ambayo mifupa inakua dhaifu na yenye kuvunjika kwa urahisi. Maumivu yanayofuatana inaweza kuwa ishara ya uchungu wa kujifungua kabla ya muda. Kwa hivyo ikiwa unapata shida hizi, ni muhimu kuchunguzwa na daktari wako hospitalini.
IMEPITIWA: APRILI, 2021.