Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito.

Ikiwa wewe ni mjamzito na unapata maumivu ya kichwa mara kwa mara, hauko pekee yako. Ripoti moja ya matibabu iliyotathiminiwa ilionyesha asilimia 39 ya wanawake wajawazito na waliotoka kujifungua hupata maumivu ya kichwa.

Ijapokuwa kipindi cha ujauzito utakuwa na maumivu ya kichwa tofauti na yale uliyozoea, ikumbukwe maumivu haya wakati wa ujauzito hayana madhara.

Maumivu ya kichwa wakati wa kipindi cha kwanza cha ujauizto yanaweza kutokea kwa sababu tofauti ukilinganisha na maumivu katika kipidni cha pili cha ujauzito. Kwa baadhi ya kesi, maumivu ya kichwa yanaweza kuwa ishara ya matatizo mengine ya kiafya wakati wa ujauzito.

Mwambie daktari au mkunga wako kuhusu maumivu haya ya kichwa kabla,wakati na baada ya ujauzito. Ni busara pia kuweka kumbukumbu ya mara ngapi unapata maumivu haya na kwa kiasi gani maumivu yanakuwa makali. Kwa kuongezea, weka kumbukumbu ya aina ya dalili nyingine unazopita.

Aina za Maumivu ya Kichwa.

Maumivu mengi ya kichwa yanayowapata wajawazito hutokea yenyewe. Hii sio dalili au ishara ya tatizo au hitilafu nyingine katika ujauzito. Haina budi kujifunza baadhi ya aina kuu za maumivu haya ya kichwa ili kukusaidia kujua aina gani ya maumivu ya kichwa inakutokea, aina hizo ni pamoja na:

Maumivu ya kichwa ya kuvuta “tension headache”. Ikiwa una msongo wa mawazo, njaa au maumivu ya shingo au mabega unaweza kupata aina hii ya maumivu ya kichwa. Ni moja ya aina kuu ya maumivu ya kichwa.

Maumivu ya kichwa kama kinagongwa gongwa “migraine attacks”. Aina hii ya maumivu unaweza pitia maumivu wastani na kuwa makali yanayogonga gonga na kudumu kwa masaa au hata siku. Wanawake wenye aina hii ya maumivu hupitia dalili kama kushindwa kuona vizuri, kufa ganzi na kichefuchefu.

“Sinus headache”. Mkandamizo kuzunguka macho, mashavu na kichwa pamoja na kubanwa mafua ni ishara za aina hii ya maumivu ya kichwa. Aina hii huchanganywa na “migraines”, maumivu haya huongezeka kila unapoinama au kulala.

“Cluster headache”. Unaweza kusikia kama maumivu juu ya maumivu yanayoanza haraka na kuwa makali sana yanayodumu kwa siku au zaidi. Maumivu haya yanajikita katika jicho moja au kuathiri upande mmoja wa kichwa. Habari njema ni kwamba, aina hii ya maumivu huwapata wanaume sana kuliko wanawake, hivyo ni nadra sana kuwapata wanawake.

Maumivu ya kichwa ya kudumu “chronic headaches”. Ikiwa unapata maumivu ya kichwa zaidi ya siku 15 ndani ya mwezi, maumivu haya yanaweza kuchukuliwa kama ya kudumu.

Je, Dalili na Ishara za Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito ni Zipi?

Maumivu ya kichwa yanatofautiana kutoka kwa mtu mmojaa na mwingine. Unaweza kupata dalili kama:

  • Maumivu kidogo/yasiyo makali
  • Kichwa kugonga gonga au maumivu ya kubana na kuachia kwa nguvu katika kichwa
  • Maumivu makali upande mmoja au pande zote mbili za kichwa
  • Maumivu ya makali nyuma ya jicho moja au yote
  • Kichefuchefu
  • Kutapika
  • Kushindwa kuona vizuri

Kwa baadhi ya wanawake wanapata shida wakiwa katika mwanga na sauti kubwa “light and sound sensitivity” wanapopata maumivu ya kichwa aina ya “migraine”. Maumivu yanakuwa makali zaidi wakisogea sehemu moja kwenda nyingine.

Nini Chanzo cha Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito?

Vichocheo (homoni) ni sababu kuu ya maumivu ya kichwa, japo zipo sababu nyingine nyingi za maumivu ya kichwa kila hatua ya ujauzito.

Kipindi cha kwanza cha ujauzito (first trimester)

Maumivu ya kichwa ya kuvuta hutokea sana kipindi hichi. Hii hutokea kwasababu mwili wa mjamzito unapitia mabadiliko mbalimbali. Mabadiliko yafuatayo yanapelekea maumivu ya kichwa:

  • Mabadiliko ya homoni
  • Kiwango kikubwa cha damu
  • Mabadiliko ya uzito wa mwili

Vilevile maumivu ya kichwa kipindi hichi yanasababishwa na: ukosefu wa maji ya kutosha mwilini, kichefuchefu na kutapika, msongo wa mawazo, ukosefu wa usingizi, kuacha kutumia kahawa, lishe duni, viwango vidogo vya damu, kiasi kidogo cha mazoezi au kazi za mwili na unyeti wa mwanga na sauti (sound and light sensitivity).

Vipo baadhi ya vyakula vinasababisha maumivu ya kichwa. Vyakula hivi vinabadilika kipindi cha ujauzito, baadhi ya vyakula hivi vinavyoweza kusababisha maumivu ya kichwa kwa baadhi ya watu ni pamoja na:

  • Maziwa
  • Chokoleti
  • Jibini
  • Mikate iliyotengenezwa na hamira
  • Nyanya
  • Nyama iliyosindikwa
  • Pombe
  • Karanga

Kipindi cha pili na cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito (second and third trimester)

Maumivu ya kichwa katika vipindi hivi yanaweza sababishwa na:

  • Uzito ziada wa mwili
  • Mkao (jinsi mjamzito anavyobeba mwili wake)
  • Kiasi kidogo cha usingizi
  • Mlo
  • Misuli kukaza na kubana
  • Shinikizo kubwa la damu: baada ya wiki ya 20 ya ujauzito, maumivu makali ya kichwa yanahusishwa na shinikizo kubwa la damu. Hali hii inaongeza nafasi ya kupata baadhi ya matatizo katika ujauzito wako kama vile kujifungua kabla ya wiki 37 ya ujauzito, kifafa cha mimba (pre-elampsia,eclampsia), tatizo la kondo la nyuma kuachia kabla mtoto hajazaliwa, kiasi kidogo cha oksijeni inayoenda kwa mtoto, mtoto kuzaliwa na uzito duni na kiharusi
  • Kisukari

Sababu nyingine za maumivu ya kichwa wakati wa ujauzito ni pamoja na maambukizi ya kawaida na magonjwa makubwa zaidi kama vile:

  • Kuvimba kwa mizizi ya hewa kwenye mifupa karibu na pua na macho “sinus infection”
  • Shinikizo dogo la damu
  • Tatizo la “blood clot” linalosababishwa na unene, kukaa mda mrefu, ujauzito, kuvuta sigara, njia za uzazi wa mpango n.k. “Blood clot” inatokea pale damu inapobadilika kutoka hali ya ukimiminika na kuwa katika hali yabisi (bonge la damu).
  • Kutoka damu
  • Ugonjwa wa selimundu (sickle cell anemia)
  • Tatizo la uvimbe kwenye ubongo (brain tumor)
  • Uvimbe (aneurysm)
  • Kiharusi
  • Matatizo ya moyo
  • Ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo.

Matibabu ya Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito.

Wakati wa ujauzito, inasahuriwa kutuliza maumivu haya kwa kutumia njia za asili kama inawezekana, ingawa mkunga au daktari wako anaweza kukushauri dawa sahihi kutumia. Ongea na daktari kabla ya kutumia dawa zako za kutuliza maumivu wakati wa ujauzito. Usitumie asprin na ibuprofen (Advil, motrin,mitishamba), Acetaminophen (tylenol) inaweza kutumika kuleta unafuu na pia inaaminika kuwa salama kwa ujauzito.

CDC (Centre for Disease Control and Prevention) wameonya kuwa matumizi ya dawa za kupunguza maumivu zinaweza kuwa na madhara kwa mtoto anayekua, haswa kama zitatumika kipindi cha kwanza cha miezi mitatu ya ujauzito. Daktari anaweza kukushauri njia mbadala za matibabu ya kutibu maumivu ya kichwa wakati wa ujauzito na dawa za asili za maumivu ya kichwa kama vile:

  • Kunywa maji na vimiminika vya kutosha
  • Ikiwa una maumivu yaliyosababishwa na “sinus infection” tumia taulo/kitambaa cha moto kukanda kuzunguka eneo la macho na pua.
  • Kama maumivu yako ya kichwa ni yakuvuta, chukua barafu zifunge kwenye kitambaa au taulo kisha weka kwenye shingo yako
  • Pumzika kwenye chumba kilicho na mwanga hafifu (giza) kisha jaribu kuvuta pumzi ndani na kuachia kuondoa msongo mwilini.
  • Oga kwa maji ya moto
  • Tafuta mkao mzuri wa kubeba mwili wako haswa kipindi cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito
  • Pumzika vya kutosha
  • Fanya zoezi la kutembea kisha kunywa maji ya kutosha
  • Pata masaji
  • Fanya mazoezi na kujinyoosha mara kwa mara.

Tafuta huduma ya haraka ikiwa una dalili zifuatazo:

  • Homa
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Kushindwa kuona vizuri
  • Maumivu makali
  • Maumivu ya kichwa yanayodumu zaidi ya masaa kadhaa
  • Maumivu ya kila mara ya kichwa
  • Kuzimia
  • Mshtuko wa moyo
  • Maumivu ya kichwa yanayoambatana na kuongezeka uzito ghafla, maumivu upande wa kulia juu ya fumbatio na kuvimba mikono na uso.

Daktari anaweza kukushauri kufanya vipimo na uchunguzi zaidi ili kujua chanzo cha maumivu ya kichwa. Vipimo hivi ni pamaoja na;

  • Shinikizo la damu
  • Kipimo cha damu
  • Kipimo cha kiwango cha sukari katika damu
  • Kipimo cha kuona
  • Ultrasound ya kichwa na shingo
  • Kipimo cha uchunguzi wa moyo na kichwa
  • Afya ya jicho kwa kutumia hadubini

Je, Ninaweza Kuzuia Maumivu ya Kichwa Wakati wa Ujauzito?

Ijapokuwa baadhi ya maumivu ya kichwa hayaepukiki, vidokezo sahihi na hatua chache zinaweza kuchukuliwa ili kuzuia kutokea hapo baadae. Baadhi ya vidokezo hivyo ni pamoja na:

  • Kula mara kwa mara. Kuruka milo kunapelekea kiwango kidogo cha sukari katika damu ambacho kinasababisha maumivu ya kichwa. Hakikisha unakula chakula kwa muda sahihi, ikiwezekana beba matunda au vitafunio vyenye afya kila uendapo ili kuufanya mwili upate virutubisho sahihi kwa wakati sahihi.
  • Lala vizuri. Pata mapumziko ya kutosha ni muhimu katika kipindi cha kwanza na cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito, lakini kumbuka usilale sana maana kufanya hivyo kutafanya kichwa kuuma.
  • Punguza matumizi ya kahawa
  • Pata hewa ya kutosha. Epuka maeneo yaliyo na joto sana, msongamano, harufu nzito. Ukiwa ndani kumbuka kufungua dirisha ili hewa safi ipenye ndani. Angalau mara chache pata hewa safi nje kwa kutembea jioni au asubuhi.
  • Tafuta eneo lenye amani na utulivu. Makelele yanapelekea maumivu ya kichwa, eneo tulivu linaweza kusaidia kuepuka maumivu ya kichwa sasa n ahata baadae.
  • Hakikisha mwili wako unadumu katika mkao ambao ni salama kwako. Jaribu kutojikunja au kuinama unapotembea au kukaa kazini.
  • Jaribu kufanya yoga, mazoezi ya kupumua kwa kuvuta pumzi ya nguvu kwa ndani na kuachia taratibu.

KUMBUKA

Maumivu ya kichwa ni kawaida wakati wa ujauzito. Unaweza ukapata maumivu ya kuvuta ya kichwa katika kipindi cha kwanza cha miezi mitatu ya ujauzito. Hali hii inaweza kutokea kwasababu ya mabadiliko yanayopitiwa na mwili kwa kipindi cha mda mfupi.

Maumivu haya ya kichwa yanaweza kutokea katika kipindi cha pili na cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito kwasababu nyinginezo. Baadhi ya sababu zinazosababisha maumivu ya kichwa katika kipindi cha katikati na mwisho wa ujauzito zinaweza kuwa kubwa na hatari kwa afya.

Shinikizo kubwa la damu ni sababu kubwa hatari ya maumivu ya kichwa wakati wa ujauzito. Wakati wowote katika ujauzito wako unaweza kupata tatizo hili. Unaweza usiwe na dalili zozote zile. Angalia shinikizo lako la damu angalau mara moja kwa siku ukiwa nyumbani kwa kutumia kifaa maaalum.

Mtaarifu daktari katika miadi yako ya kliniki ikiwa unapata maumivu haya mara kwa mara. Mjulishe daktari mara moja ikiwa kuna historia katika familia yenu ya watu kusumbuliwa na shinikizo kubwa la damu, kisukari, maumivu makali ya kichwa aumshtuko wa moyo.

Tumia dawa na matibabu kama ulivyoelekezwa na daktari wako. Fuata mlo mzuri na mazoezi salama kwa hali yako. Muone daktari kwaajili ya uchunguzi au ufuatiliaji wa matibabu kila unapopaswa kwenda. Sababu za maumivu ya kichwa wakati wa ujauzito zinatibika au kuzuilika kwa kuzingatia huduma sahihi.

IMEPITIWA: OKTOBA, 2021.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.