Mpaka sasa utakuwa umeshaandaa begi lako la uzazi utakalokwenda nalo kujifungua. Kuzijua dalili za uchungu ni hatua nyingine muhimu kwa matayarisho, kwani utajua ni wakati gani kuwasiliana na daktari au ni wakati gani uelekee hospitali.
Utahitaji kuwa na mpangilio wa nani atabaki na watoto wengine wakubwa kama unaishi nao nyumbani. Mfanyakazi wa ndani au ndugu yako anaweza akaitwa haraka na kuja kukaa na watoto wako wakati wewe umeenda kujifungua.
Usisahau kubeba pia begi la mtoto ambalo inatakiwa uwe umeshaliandaa pia. Kwenye begi hili utaweka nguo atakazovaa mtoto wako wakati wa kurudi nyumbani, nepi, kanga kadhaa, taulo laini la kumfuta akishazaliwa, chupa kadhaa za kumlishia mtoto kama umeamua hautamnyonyesha mtoto wako.
Pamoja na begi lako la uzazi, utahitaji pia kubeba pedi kadhaa za uzazi, nguo kadhaa za kubadilisha (kumbuka kuchukua nguo kubwa kubwa kwani hautarudi kwenye uzito wako wa kawaida ghafla tu baada ya kujifungua)
Kadiri utakavyojitayarisha vizuri, ndio utakavyokuwa na amani pale uchungu utakapoanza.