Maambukizi Katika Mshono Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.

Ijapokuwa nafasi ya kupata maambukizi ni ndogo sana siku hizi kwasababu ya maendeleo katika sekta ya matibabu na dawa, zipo sababu zinazoweza kuongeza hatari ya hali hii kutokea. Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na:

  • Kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua, wakati upasuaji unaendelea au hata wakati wa uchungu.
  • Kujifungua kwa upasuaji na uchungu kuchukua mda mrefu zaidi ya kawaida.
  • Kutokea kwa maambukizi katika utando wa fetasi (kijusi) na maji yanayopatikana katika mji wa mimba yanayomlinda mtoto kipindi chote cha ujauzito (amniotic fluid) kupelekea mambukizi ya bakteria yanayojulikana kama “chorioamnionitis” wakati uchungu unaendelea.
  • Mjamzito akiwa na ugonjwa wa kisukari au ugonjwa unaodhohofisha kinga ya mwili kama virusi vya Ukimwi (HIV).
  • Mjamzito akiwa na mafuta yaliyozidi yanayosababisha kiribatumbo.

Ishara na Dalili za Maambukizi Katika Mshono Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.

Kuelewa kama kidonda kimepata maambukizi kunawea kujulikana kwa kuchunguza eneo la mshono. Ikiwa huwezi kuona kidonda mwenyewe, ruhusu mtu mwingine akaguwe eneo la mshono. Baadhi ya dalili kubwa zinaashiria maambukizi kuwepo katika kidonda ni pamoja na:

  • Wekundu au kuvimba kwenye eneo la mshono, ikiambatana na maumivu.
  • Maumivu katika tumbo la chini baada ya kujifungua yanaongezeka badala ya kupungua.
  • Kidonda kinaanza kutoa usaha.
  • Mama anapata homa kali (100.5˚F)
  • Mama anashindwa kukojoa kwasababu ya hali ya kuungua inayoambatana na maumivu wakati wa kukojoa.
  • Utokaji wa uchafu wenye harufu kali ukeni.
  • Utokaji wa damu ukeni kuongezeka, hali hii itamsababisha mama kubadilisha pedi daima.
  • Utokaji wa damu ukeni yenye matone au madonge madonge.
  • Miguu itaanza kuvimba tena na kuanza kuuma.

Utambuzi wa Maambukizi Katika Kidonda Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.

Madaktari wengi wanachunguza eneo la mshono na kidonda kabla ya kuruhusiwa ili kuhakikisha hakuna maambukizi yeyote. Lakini, wanawake wengi wanapata maambukizi wiki moja baada ya kurudi nyumbani.

Kwa kuanzia madaktari huchunguza eneo la nje la mshono bila kutoa nyuzi au bandeji, mara nyingi uwekundu na kuvimba katika eneo la mshono utamfahamisha vizuri daktari kama kuna maambukizi yeyote.

Muda mwingine, mshono utachunguzwa kwa ukaribu zaidi au kutoa bandeji ili kujua zaidi kwa jinsi gani kidonda kinaendelea kupona. Maambukizi yanaweza kusababisha mshono kuachia mapema zaidi ya ilivotarajiwa.

Kama kuna usaha katika eneo la mshono, daktari atatumia sindao kufyonza usaha wote polepole na kupunguza muwasho. Wakati huohuo sampuli itachukuliwa kutoka kwenye kidonda na kupelekwa maabara kwaajili ya kuchunguzwa zaidi.

Daktari atakuuliza utaratibu wako wa kuangalia kidonda mar azote ulivyokuwa nyumbani na kitu gani kilipita juu ya kidonda kwa wiki moja iliyopita. Hii itamsaidia kupata wazo zuri la chanzo cha maambukizi katika mshono.

Aina za Maambukizi Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.

Baadhi ya maambukizi yanayoweza kutokea baada ya kujifungua kwa upasuaji ni pamoja na:

“Cellulitis”-tishu kuzunguka eneo la mshono zinapoanza kuwa nyekundu na kuvimba. Haya ni matokeo ya kwanza yanayosababishwa na aina fulani ya bakteria (staphylococcal au streptococcal). Usaha unatokea mara chache katika aina hii ya maambukizi.

“Abdominal abscess”-aina hii ya maambukizi inatokea pale eneo la mshono linapoanza kuwasha na kuuma, pembezoni kunaanza kuvimba vilevile. Inapelekea bakteria kushambulia uvungu wa tishu na kusababisaha usaha kutengenezwa. Pia usaha unaanza kutoka nje ya mshono.

“Endometritis”-wakati mwingine maambukizi yanafika kwenye mji wa mimba (uterasi) na kuanza kushambulia ukuta wa ndani ya uterasi. Hali hii inasababisha maumivu makali ya tumbo la uzazi na utokaji uchafu ukeni kunakoambatana na homa kali. Maambukizi haya yanasababishwa na bakteria pia.

Maambukizi katika mfumo wa mkojo (UTI)- kuna baadhi ya wanawake wanaweza hitaji mpira maalumu wa kutoa mkojo wakati wa kujifungua. Matumizi ya mpira huu yanaongeza nafasi ya kupata UTI kwasababu ya bakteria ajulikanae kama “e-coli”.

Maambukizi yanayosababishwa na fangasi anayepatikana mwilini aitwaye candida (thrush)- maambukizi haya yanawashambuliwa wanawake walio na kinga hafifu ya mwili, husababisha fangasi ukeni au hata vidonda mdomoni.

Matatizo Yanayosababishwa na Maambukizi Katika Mshono Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.

  • Ushambuliaji wa tishu zenye afya mwilini “necrotizing fasciitis”
  • Tishu zenye afya za mwili kuwa wazi kupata kidonda
  • Kuachia kwa mshono na sehemu ya ndani ya mshono iliyoanza kupona “dehiscence of the wound”.
  • Kidonda kufunguka kabisa na kinyesi kuanza kutoka kupitia kwenye kidonda “wound evisceration”

 Matibabu ya Maambukizi katika Mshono Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji.

  • Chunguza kidonda mara kwa mara kuhakikisha kinapona vizuri au kama kuna chochote kinachotoka kwenye eneo la mshono.
  • Usaha wowote unatakiwa kufyonza ili kurahisisha uponaji.
  • Dawa maalum itumike kusafisha kidonda vizuri na kuondoa aina yeyote ya bakteria.
  • Kusafisha na kubadilisha bandeji katika kidonda kufanyike mara kwa mara.

Njia Mbalimbali za Kuzuia Maambukizi Katika Mshono Baada ya Kujifungua kwa Upasuaji

  • Angalia vizuri kidonda baada ya upasuaji na mjulishe daktari mara moja ikiwa kuna dalili zisizo sawa utaziona.
  • Tumia na maliza dozi ya antibaiotiki ulizoandikiwa na daktari kipindi chote isipokuwa kama umeshauriwa vinginevyo na daktari.
  • Safisha kidonda mara kwa mara na badilisha bandeji kama ilivyoshauriwa na daktari.
  • Vaa nguo zilizolegea juu ya eneo la mshono, epuka kutumia kipodozi chochote.
  • Chagua njia tofauti za kumbeba mtoto wako wakati wa kunyonyesha kuepusha mgandamizo katika kidonda.
  • Usishike eneo la mshono.
  • Mjuze daktari au mkunga ikiwa mwili wako utaanza kupata joto juu ya 100˚F
  • Wasiliana na dakatari wako au mkunga ikiwa dalili za usaha, maumivu au kuvimba zikionekana.

Vidokezo Vitakavyokusaidia Katika Uponaji wa Mshono

  • Hakikisha unatumia dawa mara kwa mara kutibu maumivu na kuvimba eneo la mshono
  • Shika tumbo lako kila unapopiga chafya, tembea wima usipinde mgongo ili kuepusha maumivu ya mgongo hapo baadae.
  • Kunywa maji na vimiminika vya kutosha
  • Usinyanyue kitu chochote kizito.
  • Pumzika kadiri uwezavyo.

IMEPITIWA: OKTOBA, 2021.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.