Uchungu ni mwendelezo wa mchakato wa mimba tangu ilipotungwa. Uchungu wa mjamzito ni wa kipekee na hubadilika kutokana na mambo mengi ikiwemo: maumbile yako (fiziolojia), ukubwa na mkao wa mtoto wako, afya na historia ya maradhi yako, matarajio na hisia zako, watu unaoishi nao na wanaokusaidia, mtaalam atakayekuhudumia, na mahali utakapojifungulia mtoto wako. Hatua za uchungu hutofautiana kati ya mwanamke mmoja hadi mwingine.
Kuelekea mwishoni mwa ujauzito au hata mapema zaidi kwa baadhi ya wanawake-wanaweza kuhisi mji wa mimba ukikaza mara chache bila kuhisi maumivu yoyote, kitendo hiki huitwa “Braxton-Hicks contractions” au (leba ya uongo). Kukaza kwa mji wa mimba ni hali ya kawaida ambayo haitokei katika mpangilio maalum, na wala haisababishi mlango wa kizazi kufunguka. Mikazo hii ni njia ya asili ya mwili kujiandaa kwa ujio wa uchungu halisi wa kuzaa.Utahisi kuongezeka kwa msukumo kwenye nyonga na kibofu cha mkojo kadiri mtoto anavyozidi kusogea chini zaidi.
Mkazo wa aina hii katika mji wa mimba ni maarufu sana kwa wajawazito katika kipindi cha mwisho cha miezi mitatu ya ujauzito, lakini inaweza kuanza mapema zaidi muda wowote baada ya wiki ya 20 ya ujauzito.
Mjamzito Anayepitia Leba ya Uongo (Braxton Hicks Contractions) Anahisije?
Kwa ujumla wanawake wengi waliopitia uchungu huu wameripoti mikazo hii kutokuwa na maumivu ila inasababisha mikazo ya tumbo inayodumu kati ya sekunde 30 mpaka 60 na kwenda mpaka dakika 2 kwa muda. Mikazo hii inaweza kuleta wasiwasi kwa wajawazito lakini ikumbukwe haisababishi uchungu halisi kuanza au kufunguka kwa mlango wa uzazi (cervix). Ukilinganisha na uchungu halisi wa kujifungua, aina hii ya uchungu:
- Hausababishi maumivu.
- Unatofautiana, hutokea kawaida au bila mpangilio.
- Unaachana sana kati ya mkazo mmoja na mwingine.
- Unadumu kwa muda mfupi.
- Kwa kawaida hutokea kwa saa chache na baadaye kuacha- wakati mwingine hata siku kadhaa.
- Unaacha ukibadilisha mkao au shughuli unayoifanya.
- Mikazo yake inasikika katika tumbo.
Nini Husababisha Leba ya Uongo?
Chanzo halisi cha mikazo hii hakijulikani. Watafiti wa kuaminika wa afya wameafiki kuwa kuna baadhi ya shughuli na hali zinazoweza kumsumbua mtoto ndani ya mji wa mimba. Mikazo hii katika mji wa mimba inaweza kusaidia kuongeza mtiririko wa damu kwenye plasenta na kumpatia mtoto hewa ya oksijeni zaidi.
Vyanzo vya hali hii ni pamoja na:
- Upungufu wa maji mwilini. Wajawazito wanahitaji vikombe 10 mpaka 12 vya maji na vinywaji vingine kama maziwa au juisi ya matunda safi kila siku, jitahidi kunywa maji ya kutosha.
- Unaweza kushuhudia mikazo katika mji wa mimba baada ya kusimama muda mrefu au kufanya shughuli nyingi za nyumbani au kufanya kuupa mwili zoezi kidogo.
- Tendo la ndoa. Kufika kilele wakati wa tendo la ndoa (orgasm), inaweza kusababisha misuli ya uterasi kukaza. Hii ni kwasababu mwili unaachia “oxytocin” baada ya kufika kileleni. Kichocheo hichi husababisha mkazo wa mawimbi wa mara kwa mara.
- Kibofu cha mkojo kilichojaa. Kibofu cha mkojo kilichojaa kinapeleka mgandamizo katika uterasi na kusababisha mikazo au maumivu ya misuli ya tumbo.
Unawezaje Kutofautisha Leba ya uongo na Leba ya ukweli?
Wakati
Leba ya uongo
- Hutokea baada ya wiki ya 20 ya ujauzito.
Leba ya ukweli
- kawaida hutokea kati ya wiki ya 37 na 40 ya ujauzito.
Marudio ya mikazo
Leba ya uongo
- Yanatofautiana, hutokea kawaida au bila mpangilio.
- Unaachana sana kati ya mkazo mmoja na mwingine.
Leba ya ukweli
- Inakuwa na mpangilio maalumu
- Uchungu unakuwa mkali, kuongezeka kadiri mda unavyoendelea.
Muda
Leba ya uongo
- Sekunde 30-60 mpaka dakika
- Kila mkazo unabadilika kwa muda.
Leba ya ukweli
- Maumivu yanayopanda na kushuka yanayoachana kwa muda wa dakika tano na kudumu kwa sekunde 45 mpaka 60 na huwa ni makali sana.
Ukali
Leba ya uongo
- Hausababishi maumivu lakini inakufanya ujisikie vibaya tu.
- Makali ya mikazo ya mji wa mimba hayaongezeki.
- Yanapotea ukibadilisha mkao.
Leba ya ukweli
- Maumivu yanayopanda na kushuka huwa ni makali sana kiasi kwamba hushindwa hata kuongea kadiri muda unavyoenda.
- Makali hayapungui hata ukibadilisha mkao.
Eneo
Leba ya uongo
- Hutokea sehemu ya chini ya fumbatio na ukeni.
Leba ya ukweli
- Huanza mgongoni na kusogea sehemu ya mbele.
Je, Kuna Tiba Zozote za Leba ya Uongo “Braxton Hicks Contractions”?
Baada ya kuthibitisha na daktari unapitia leba ya uongo na sio leba halisi, unaweza kupumzika bila wasiwasi.
Hakuna haja ya matibabu ya kidaktari kwaajili ya aina hii ya uchungu. Jaribu kujikita katika kupumzika, kunywa maji ya kutosha na kubadilisha mkao-hata ikibidi kusogea kutoka kitandani kwenda kwenye kochi.
Jitahidi:
- Kwenda maliwatoni kujisaidia haja ndogo (ikiwa haufanyi hivyo kila baada ya saa moja).
- Kunywa glasi tatu mpaka nne za maji au kinywaji kingine kama maziwa, au juisi ya matunda safi.
- Lala kwa ubavu wa kushoto, ulalaji huu unaimarisha mtiririko mzuri wa damu kwenye uterasi, figo na plasenta.
- Mara nyingi uchungu huanza usiku. Wakati mwingine kuoga kwa maji ya moto ya bomba la mvua husaidia kupunguza maumivu, na kukufanya upate usingizi.
- Hakikisha unakula na kupumzika.
- Ili kupunguza maumivu, wajawazito wengine hupenda kutembea kunasaidia kupunguza uchungu.
- “Massage” inasaidia pia.
Ikiwa mbinu hizi hazifanyi kazi kupunguza uchungu wa mapema unaopitia, usisite kumuuliza daktari au mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako matibabu mengineyo yanayofaa. Ijapokuwa utatuaji wa hali za kila siku za maisha zinashauriwa kutumika, ila kuna baadhi ya dawa zinazoweza kusaidia kupunguza mikazo na mibano katika mji wa mimba.
KUMBUKA
Wasiliana na mkunga wako au daktari anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako mara moja ikiwa una dalili kama:
- Unatokwa damu ukeni
- Unavuja maji maji au kama chupa yako ya maji ya uchungu imevunjika.
- Mikazo ya nguvu kila dakika tano ndani ya saa moja.
- Maumivu yasiyovumilika.
- Mtoto kucheza tumboni tofauti kuliko kawaida, au kama mtoto hachezi mara 6-10 ndani ya saa moja.
- Maumivu ya mgongo yanayoendelea.
- Dalili zozote za uchungu halisi kabla ya wiki ya 37 ya ujauzito.
IMEPITIWA: JULAI,2021.