Kwikwi kwa Mtoto Mchanga Baada ya Kumnyonyesha.

Unaweza kushuhudia mtoto wako ana kwikwi mara nyingi- wanaweza kupata kwikwi hata walipokuwa bado tumboni. Kwikwi ni kawaida kwa watoto wachanga na wenye umri chini ya mwaka mmoja kwasababu mfumo wao wa umeng’enyaji haujajengeka vizuri.

Nini Husababisha Kwikwi?

Kwikwi ni moja ya tabia ya kwanza mtoto wako kupata. Katika utafiti uliofanya 2019 ulionyesha kwikwi inaweza kuwa muhimu katika ukuaji wa ubongo wa mtoto wako na maendeleo katika upumuaji. Kwiki ni kama hatua nyingine ya ukuaji kwa mtoto- ni ya kwanza kukua tangu wakiwa tumboni.

Kwikwi husababishwa na kubana ghafla kwa msuli wa kiwambo (diaphragm) kinachotenganisha sehemu ya tumbo na mapafu, kiwambo hicho hushtuliwa kwa watoto hasa wanapopaliwa na maziwa na wakati mwingine hutokea tu yenyewe.

Kwikwi ni kitendo cha kawaida kwa watoto. Mara nyingi kwikwi inawapata watoto wachanga wengi, hii pia ni ishara kuwa mtoto wako ana afya na anakua vizuri.

 Nifanye Nini Kama Mtoto Wangu Amepata Kwikwi.

Kwa kawaida watoto hawasumbuliwi na kwikwi wanaweza kula na kulala wakiwa nayo. Kawaida kwikwi inaisha yenyewe ndani ya dakika 5 mpaka 10, hali hii kufanya matibabu yasiwe lazima.

Kama una wasiwasi na kwikwi anazozipata mtoto wako, kuna baadhi ya mbinu zinazoweza kusaidia kumaliza kwikwi mapema zaidi au kuzuia kabisa:

  • Mcheulishe mtoto baada ya kumnyonyesha. Watoto wanaweza kuanza kwikwi wakati wananyonya kwasababu ya hewa iliyozidi tumboni inayosumbua tumbo lao. Kumbeba mtoto kwenye bega kisha kumpiga piga mgongoni taratibu inaweza kumsaidia.
  • Mnyonyeshe mtoto polepole. Kama utaona mtoto wako anapata kwikwi wakati wa kunyonya, itakuwa imesababishwa na kumnyonyesha harakaharaka. Jaribu kumnyonyesha polepole huku ukimpa wakati wa kupumua kila unapombadilishia titi, hii itasaidia kupunguza nafasi za mtoto kupata kwikwi wakati wa kunyonya.
  • Mnyonyeshe mtoto anapokua ametulia. Jaribu kunyonyesha mtoto kabla hajapatwa na njaa kali na kuanza kulia. Kama mtoto wako atakuwa analia wakati wa kunyonya, maziwa hayatashuka kama inavyotarajiwa katika koo lake.
  • Mbebe mtoto kwa wima baada ya kumnyonyesha. Mkao huu kwa dakika 20 mpaka 30 utasidia chakula kutulia tumboni na kuhakikisha mmeng’enyo wa mtoto wako unaenda vizuri. Itasaidia pia hewa kutoka tumboni mwake.
  • Kama unamnyonyesha mtoto kwa kutumia chupa hakikisha kwenye chuchu ya chupa imejaa maziwa kabla ya kumuwekea mdomoni, kupunguza hewa kwenye chuchu ya chupa kunapunguza hewa ziada kuingia tumboni kwa mtoto na kusababisha kwikwi mbaya.
  • Hakikisha midomo ya mtoto wako imefunguka vizuri kwenye chuchu yako. Msikilize mtoto anaponyonya iwapo utasikia sauti ya kugugumia inamaanisha mtoto wako hajanyonya vizuri chuchu yako na hali hii itapelekea kuingiza hewa ziada tumboni itakayosababisha kwikwi kutokea.
  • Nunua chupa yenye chuchu sahihi kwa mtoto wako. Kama unanyonyesha kwa kutumia chupa hakikisha mtiririko wa maziwa katika chuchu ya chupa sio wa haraka sana au taratibu sana kwa mtoto wako. Kama chuchu ya chupa inatoa maziwa kwa kasi sana itasababisha tumbo la mtoto kujaa haraka na kusababisha maumivu. Chuchu ya chupa ikiruhusu maziwa kutiririka polepole sana inaweza kumfanya mtoto aliye na njaa kufadhaika na kunyonya kwa nguvu huku akiingiza hewa kwa wingi. Mtiririko sahihi katika chuchu ya maziwa unategemea na umri wa mwanao, hivyo unaweza kuhitajika kubadili chuchu za chupa kila miezi michache.
  • Mara baada ya mtoto kunyonya, epuka kazi nzito kwa mtoto kama vile kumrusha juu na chini au mchezo wa kutumia nguvu nyingi.
  • Acha kwikwi iache yenyewe. Kwa watoto wenye umri zaidi ya mwaka mmoja wanaopata kwikwi mara kadhaa huwa inaacha yenyewe. Mara nyingi sana kwikwi ya mwanao itaacha yenyewe, hivyo kama haimsumbui mtoto subiri iache yenyewe. Ikiwa tofauti na hapo pata ushauri wa dakatri au mkunga. Mara chache sana, kwikwi inaweza kuwa ishara ya tatizo kubwa la kiafya.

KUMBUKA

Utahitaji kumuona daktari ikiwa mtoto wako hajaacha kwikwi kwa kipindi kirefu sana baada ya kunyonya au anaonekana kuteseka akiwa na kwikwi.

Kuwa makini na njia za nyumbani zinazotumika kukomesha kwikwi. Usitumie njia za kumaliza kwikwi kwa watu wazima kwa mtoto wako mchanga. Kumbuka mwanao bado mdogo koo lake la chakula na tumbo bado havijakomaa, hivyo tumia njia salama kwa mtoto.

Kwikwi ni kawaida na mara nyingi hazimdhuru mtoto wako. Kwa watoto wadogo, kwikwi ni ishara kuwa: wanawekwa mikao mibaya wakati au baada ya kunyonyeshwa, wanatakiwa kunyonyeshwa polepole, au wanahitaji mda wa kupumzika wakati au baada ya kunyonya. Tafuta msaada wa kitabibu ikiwa mtoto wako anaonekana kuwa kwenye maumivu au kwikwi hajakoma kwa masaa mengi.

Kwikwi za mara kwa mara zinategemea kupotea mtoto akifika mwaka mmoja.

IMEPITIWA: OKTOBA,2021.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.