Kwanini chunusi hutokea na namna ya kupambana nazo

Chunusi ni nini?

Chunusi ni ugonjwa wa ngozi unaowaathiri watu wengi katika kipindi fulani cha maisha yao. Ugonjwa huu husababisha vipele vidogo vidogo vya mafuta kwenye ngozi na wakati mwingine hufanya ngozi kuwa na maumivu au kuhisi kuungua. Viupele hivi hutokea wakati vishimo vya kupitisha jasho katika ngozi vinapozibwa kwa mafuta na seli za ngozi zilizokufa au wadudu yaani bakteria. Mara nyingi chunusi hutokea usoni, mgongoni, kifuani na shingoni. Chunusi huwaathiri takribani asilimia 80% ya watu wenye umri kati ya miaka 11-30. Ugonjwa huu hutokea zaidi wasichana kuanzia miaka 14-17 na wavulana kuanzia miaka 16-19.

Jinsi gani chunusi hutokea?

Kawaida ngozi ina vishimo vidogo vidogo vya kutolea jasho,mafuta na seli zilizozeeka kutoka ndani ya mwili. Katika ngozi pia kuna tezi ya mafuta iitwayo ‘sebacous gland’ inayotoa mafuta yaitwayo sebum. Uzalishaji wa sebum nyingi na seli za ngozi zilizokufa husababisha kuziba kwa vishimo vidogo vidogo vya ngozi vinapitisha jasho katika ngozi na kusababisha kuvimba na mara nyingine kujaa kwa usaa na kusababisha chunusi. Licha ya hayo chunusi pia huchangiwa na sababu nyinginezo kama:

  • Mabadiliko ya homoni
  • Bakteria
  • Matibabu
  • Kizazi(genetics)

Jinsi gani ya kupambana na chunusi?

Kuna njia nyingi za matibabu za kupunguza chunusi zikijumuisha kubadili hali ya maisha, taratibu na dawa. Kula kabohidrati chache na zinazomeng’enywa kwa urahisi, kama vile sukari, kunaweza kusaidia. Usijaribu kuviminya au kuvisugua kwa nguvu viupele kwasababu hufanya ngozi kuuma na kutengeneza makovu ya kudumu. Jiepushe kutumia manukato au vipodozi kwenye ngozi yenye chunusi. Tumia bidhaa za urembo zisizoziba matundu madogo madogo ya ngozi yako.

Chunusi pia huweza kutibiwa kwa matumizi ya tiba asili kama matumizi ya matunda na viungo kama vitunguu swaumu, mdalasini na vingine. Hii ni njia nzuri ya kupatia ngozi unafuu na tiba mbadala na rafiki kwa ngozi yako. Zifuatazo ni baadhi ya tiba asili za chunusi na salama kwa ngozi yako:

Mdalasini wa unga na asali.

Kwa wale ambao wanasumbuliwa sana na chunusi iwe, usoni, kifuani, mgongoni n.k wanaweza tumia mchanganyiko mzuri wa asali na mdalasini wa unga kwa kupaka angalau mara moja kwa siku. AsaliI na mdalasini  zinasaidia kuponyesha kwasababu zina tabia za ANTI-BACTERIAL (zinaua na kuzuia mazalia ya bacteria) Jinsi ya kufanya:

  1. Chukua vijiko vitatu (3) vya chai vya asali
  2. Chukua nusu kijiko cha chai cha mdalasini wa unga safi
  3. Changanya pamoja kupata uji uji mzuri
  4. Paka sehemu yenye chunusi na kisha kaa nayo kwa angalau dakika 10-30 kisha osha kwa maji ya uvuguvugu.

ANGALIZO: MDALASINI unaweza kuwasha kwenye ngozi hivyo unashauriwa ujaribu kupaka kidogo kwenye kiganja cha mkono kwanza ili kupata uhakika kua haitakusumbua.

Matango:

Unaweza kutumia tango kwa kuondoa chunusi na hata kuondoa mabaka mabaka katika ngozi na kuifanya ngozi yako kuonekana yenye afya na yenye kuvutia. Matango ni mazuri sana kwa kusafishia uso na haswa ukiwa na chunusi. Kata tango na kisha liponde ponde (unaweza kutumia blenda) kisha paka au kandika usoni. Acha likae kwa muda wa dakika 15 hadi 20 hivi, kisha suuza kwa maji baridi. Unaweza kurudia kwa siku mara mbili mpaka mara tatu hadi utakapopona.

Asali:

Matumizi ya asali kutibu chunusi huwezesha ngozi, iwe na afya na nyororo. Kwa sababu kwenye asali kuna virutubisho vingi vyenye kazi ya kuua vimelea (bacteria) na kuzuia uchafu na kusinyaa kwa ngozi. Weka asali kidogo sehemu ilio athirika na iache kwa muda mrefu kadri uwezavyo. Vilevile unaweza kupaka uso mzima au hata mwili mzima ukitaka. Sababu asali inarutubisha ngozi ya mwili na kuifanya iwe na afya na mwonekano mzuri. Ukisha ridhika na muda wa asali kwenye ngozi yako unaweza kusafisha kwa kutumia maji ya vuguvugu.

Papai:

Unaweza kushangaa, lakini matumizi ya papai yameonyesha matokeo mazuri sana katika kuondoa chunusi usoni na kusafisha sehemu zingine za mwili. Ponda ponda kiasi kidogo cha papai na upakae sehemu yenye chunusi, kisha liache kwa muda mrefu kadri uwezavyo. Ukisha ridhika na muda unaweza kujisafisha kwa kutumia maji ya kawaida. Unaweza kurudia mara kadhaa kila siku kama unataka.

 

Imepitiwa: Feb 2018

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.