Kutungwa kwa mimba – Conception

Jinsi mimba inavyotungwa (Conception)

Kutungwa kwa mimba (conception) ni ule wakati yai na mbegu (manii) hukutana. Inaweza kuchukua muda kati ya dakika 45 hadi masaa 12 kwa manii kufika kwenye mirija yako ya uzazi, sehemu ambayo mara nyingi kutungwa kwa mimba hutokea. Japokuwa manii huweza kuishi ndani ya mwili wako hadi siku saba, hivyo kutungwa kwa mimba kunaweza kutokea muda wowote kwenye wiki baada ya kufanya mapenzi kama upo kwenye ovulation.
Jifunze zaidi kuhusu safari hii ya kushangaza, na namna maisha huanza!

Ndani ya mwili wa mwanamke: jinsi yai linavyotolewa

Kwa wanawake, uwezekano wa kupata ujauzito huanza kwenye mifuko ya mayai (ovaries). Hivi ni viungo kama mifuko miwili yenye umbo la yai, vinavyounganika kila upande wa mfuko wako wa uzazi (uterus). Mifuko hiiya mayai imejaa mayai, ambayo hutengenezwa hata kabla ya kuzaliwa kwako. Kila mtoto wa kike huzaliwa na mayai kati ya milioni 1 hadi 2 kwenye mifuko yake ya mayai. Mayai mengi huanza kufa mara moja na yaliyobakia huanza kupungua idadi taratibu kadiri unavyoongezeka umri. Unaweza kutoa mayai 400 katika miaka yako unayoweza kupata mimba, hiki ni kipindi tangu ulipoona hedhi kwa mara ya kwanza mpaka utakapofikia “menopause”. Kwa kawaida wastani wa umri wa kufikia “menopause” ni kati ya miaka 50.
Katika kila mzunguko wako wa hedhi, wakati fulani baada ya kuona siku zako, mayai 1 hadi 3 huanza kufikia kukomaa ndani ya moja ya mifuko yako ya uzazi. Yai lililokomaa zaidi huachiliwa, hatua inayojulikana kama ovulation (kutolewa kwa yai)

Yai la kawaida kwa wastani huishi kwa masaa 24 tangu liachiliwe. Litahitaji kuchavushwa ndani ya muda huu kwa mbegu Ili mimba iweze kutungwa. Kama yai lako litakutana na mbegu hai na yenye afya ikiwa inasafiri kwenye mji wa mimba, hatua za kutengeneza maisha mapya huanza. Kama sivyo, yai humaliza safari yake kwenye mfuko wa uzazi na kuyeyuka.

Kama mimba haikutungwa, mifuko ya mayai huacha kutoka homoni za “oestrogen” na “progesterone”. Hizi ni homoni mbili ambazo husaidia kuushikilia ujauzito. Pale homoni hizi zinapopungua, ukuta uliokuwa umekua kwenye mji wako wa mimba humomomonyoka ukiwa kwenye hedhi. Mabaki ya yai ambalo halikuchavushwa hutoka wakati wa hedhi pia.

Ndani ya mwili wa mwanaume: jinsi manii zinavyotengenezwa

Miili ya wanawake hukuza yai moja kila mwezi. Miili ya wanaume kwa upande mwingine huwa mar azote kazini, kutengeneza mamilioni ya mbegu za uzazi (manii). Lengo kuu la kila mbegu ni kuogelea kuelekea kwenye yai na kufanikiwa kupenyeza na kuingia ndani.
Kuanzia mwanzo hadi mwisho inachukua miezi mitatu kutengeneza mbegu mpya. Kwa wastani mbegu huishi kwa wiki chache tuu ndani ya mwili wa mwanaume, na kadirio la karibu milioni 40 huachiliwa huru kila mwanaume anapofika kileleni na kukojoa. Hii inamaanisha wanaume lazima watengeneze mbegu za uzazi (manii) mara kwa mara katika maisha yao ya utu uzima.
Homoni zilezile zinazoongoza ovulation kwa wanawake ndio zinaanzisha utoaji wa homoni ya “testosterone” kwa wanaume. “Testosterone” ndio homoni inayohusika na uzalishaji wa mbegu (manii). Uzalishaji wa manii huanza kwenye korodani, glandi mbili zilizofunikwa ndani ya “pumbu” chini ya uume. Korodani zinaning`inia nje ya mwili kwa sababu zinaathiriwa na joto. Kutengeneza mbegu zenye afya korodani inabidi zikae kwenye mazingira yaliyo kati ya digrii 34c. Hii ni kama digrii 4c baridi kuliko mwili. Baada ya manii kutengenezwa, huhifadhiwa kwenye kila korodani kwenye mrija wa mbegu (epididymis). Muda mchache kabla ya kufika kileleni na kukojoa, manii husafiri juu na kuchanganywa na shahawa kutoka kwenye tezi dume (prostate).

Pamoja na mamilioni ya manii kutengenezwa na kuachiliwa kipindi cha kufika kileleni, mbegu moja tuu ndio inaweza kulichavusha yai. Jinsia ya mtoto wako inategemea na aina gani ya mbegu imeingia kwenye yai ya kwanza. Mbegu zenge kromosomu Y hutengeneza mtoto wa kiume, na mbegu zenye kromosomu X hutengeneza mtoto wa kike. Kuna uvumi mwingi kuhusu namna ya kupata mtoto wa kiume au wa kike, baadhi kuna ushahidi wa kisayansi lakini ki uhalisia jinsia ya mtoto hutokea bila mpangilio maalumu.

Nini hutokea wakati unafanya ngono

Ukijumlisha na raha ya ngono, miili yenu hutengeneza mvutano ambao mnategemea utaishia kwenye kufika kileleni. Kufika kileleni pia kuna umuhimu mkubwa kibaiolojia. Kwa wanaume, kufika kileleni husukuma shahawa zilizojaa manii kwenye uke na ndani zaidi kuelekea kwenye mlango wa mfuko wa uzazi kwa spidi ya kadiri km 15 kwa saa. Nguvu ya kufika kileleni na kukojoa huzipa shahawa mchepuko wa kwanza kuelekea kwenye yai. Mwanamke haitaji kufika kileleni kwa mimba kutungwa. Mikazo michache ya mfuko wake wa uzazi inatosha kuzisaidia shahawa kusafiri, lakini hii hutokea bila hata mwanamke kufika kileleni.
Wenza wengi huwaza kama kuna aina fulani ya mikao wakati wa ngono inayoweza kusaidia kutungwa kwa mimba. Haijulikani kwa uhakika. La muhimu zaidi kuhusu ngono ni kuwa wote mnafurahia na mnafanya mara kwa mara iwezekanavyo. Kwa wewe kutunga mimba, mbegu hai inabidi iwepo kwenye mfumo wako wa uzazi kipindi chako unachoweza kutunga mimba (ovulation).

Sio wanawake wote kipindi chao cha kuweza kushika mimba (ovulation) kipo katikati ya mzunguko wao wa hedhi. Kuongeza uwezekano wa kupata ujauzito jitahidi kufanya ngono kila baada ya siku moja kwenye mzunguko wako wote.

Wakati unapumzika, kazi ya manii ndio kwanza inaanza

Katika wakati huu huwezi kufanya chochote zaidi ya kukunja vidole vyako ukitegemea mimba itajitunga. Wakati wewena mwenza wako mnafurahia na kukumbatiana baada ya mapenzi, mengi yanaendelea ndani ya mwili wako. Mamilioni ya zile mbegu zimeanza safari kabambe kulitafuta yai lako, na hii sio safari rahisi. Kipingamizi cha kwanza kinawezakuwa ute ute kwa kwenye mlango wa mfuko wa uzazi (cervical mucus), ambao kipindi haupo kwenye ovulation ni vigumu chochote kupenya. Ukiwa kwenye siku za kuweza kupata mimba hali huwa tofauti na kulegea kidogo, hivyo mbegu zitakazokuwa na nguvu ya kuogelea zaidi zinaweza zikapenya.
Mbegu iliyofanikiwa kupenya bado itakuwa na safari ndefu mbeleni. Kuanzia hapa mpaka mbegu zikutane na yai zitaweza kusafiri wastani wa sentimeta 18. Kwa kawaida husafiri kila sentimeta 2 na nusu kwa robo saa. Mbegu itakayokuwa na spidi zaidi inaweza kulifikia yai ndani ya dakika 45, wakati iliyo na spidi ndogo itaweza ikachukua hadi masaa 12. Kama mbegu zisipokutana na yai baada ya ngono, zinaweza kuishi ndani ya mwili wako kwa hadi siku saba. Hii inamaanisha kama utafikia kipindi chako cha ovulation ndani ya muda huu mimba inaweza ikatungwa.

Asilimia kubwa ya mbegu hufa kabla ya kulifikia yai. Mbegu chache sana hulifikia yai. Mbegu nyingine hukwama njiani, nyingine hupotea na nyingine hufa njiani. Kwa zile zenye bahati kufika karibu na yai, mapambano hayajaisha. Kila mbegu hupigana kufa na kupona kulipenyeza yai na kuingia ndani kabla ya wenzake. Yai huhitaji kuchavushwa ndani ya masaa 24 tangu liachiwe. Pale ambapo mbegu ngumu kuliko zote kwenye mapambano inapopenya, yai hubadilika ghafla na kuzuia mbegu nyingine kuingia ndani. Hii ni kama kinga ambayo hukifunika yai katika wakati ule ule ambao mbegu ya kwanza imefanikiwa kuingia salama.

Sasa maisha mapya yamezaliwa

Katika kipindi cha kutungwa kwa mimba, taarifa mpya ya genetiki kwenye manii na kwenye yai huungana na kutengeneza seli ambayo huanza kugawanyika haraka sana. Huu mkusanyiko mpya wa seli utakaotokea huitwa “blastocyst”. Huendelea kusafiri chini kwenye mirija ya uzazi kuelekea kwenye mfuko wa mimba, safari inayoweza kuchukia siku tatu zaidi.
Utakuwa bado si mjamzito mpaka pale mkusanyiko wa seli “blastocyst” utakapojipachika kwenye ukuta wako wa mimba, hapa itatengeneza “embryo” na “placenta” – mrija unaounganisha mwili wa mama na mtoto hapo baadae. Wakati mwingine mkusanyiko huu wa seli unaweza ukajipachika sehemu nyingine ambayo sio kwenye ukuta wa mimba, kama kwenye mirija ya uzazi (fallopian tube). Hii ikitokea ujauzito unakuwa umejitunga nje ya mfuko wa mimba (ectopic pregnancy) ambayo ni dharura kwa afya. Mimba haiwezi kukua nje ya mfuko wa uzazi na hutakiwa kutolea moja kwa moja kuepuka kupasuka na kuharibu mijija ya uzazi.

Itakuwa baadhi ya wiki mpaka utakapozikosa siku zako za hedhi na kuhisi unaweza ukawa mjamzito. Pale utakapozikosa siku zako na kuziona baadhi ya dalili za ujauzito nyingine, kipimo cha mimba kinaweza kukupa uhakika. Kama umehakikisha na unategemea kuanza kuitwa Mama Kijacho, hongera na karibu kwenye mwanzo wa safari nzuri ya ujauzito wako.

Imepitiwa: April 2017

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.