Moja ya njia muhimu ya kutunza mfumo wa uzazi wa mwanamke ni kupitia uchafu unaotoka ukeni. Uchafu huu huweka uke wa mwanamke kuwa na afya nzuri ingawa wakati mwingine huweza kuleta shida. Maji yaliyotengenezwa na tezi ndani ya uke na mlango wa uzazi hubeba seli zilizokufa na bakteria nje ya mwili. Tendo hili linaweka uke safi na kusaidia kuukinga na maambukizi.
Wanawake wote hutokwa na uchafu ukeni, ingawa kiwango hutofautiana. Mara nyingi uchafu unaotoka ukeni ni kawaida kabisa. Unatofautiana kwa harufu,uzito, na rangi kulingana na mzunguko wako wa hedhi. Kwa mfano unaweza kutoka uchafu mwingi ukeni kama uko kwenye siku za yai lako kupevushwa, unanyonyesha au ashiki (hamu ya kujamiana). Uchafu huu unaweza kutoa harufu ya tofauti ukiwa mjamzito au unaposhindwa kujisafisha vizuri. Wanawake waliokomaa (menopause women) hupata uchafu huu kwa kiwango kidogo sana.
Mabadiliko haya yasikupe wasiwasi ni kawaida. Isipokuwa kama una dalili zifuatazo unaweza kuwa na tatizo la maambukizi ya vijidudu vya maradhi katika uke wako, ni vema kuwahi kituo cha afya kupatiwa uchunguzi zaidi na tiba sahihi:
- Kutokwa uchafu ukeni kunakoambatana na kuwashwa au vipele.
- Kutokwa uchafu ukeni ambako ni endelevu na kiwango kinaongezeka kila siku.
- Maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo.
- Kutoka uchafu mweupe, mzito kama jibini.
- Kutoka uchafu wa kijivu/mweupe au njano/kijani unaotoa harufu mbaya.
- Unajikuna, kuchomwa au hata uvimbe kwenye uke.
- Maumivu wakati wa tendo la ndoa.
Nini chanzo cha uchafu ukeni usio wa kawaida kwa mwanamke?
Badiliko lolote katika uwiano sawa wa bakteria wa asili wanaopatikana ukeni linaweza kuathiri harufu, rangi na muonekano wa uchafu unaotoka ukeni. Hizi ni baadhi ya sababu zinazopelekea uchafu ukeni kwa mwanamke yeyote:
- Matumizi ya antibaotiki au virutubisho vya kikemikali (steroid)
- Maambukizi yanayosababishwa na bakteria “bacterial vaginosis” – yanawapata wajawazito sana au wanawake walio na wapenzi zaidi ya mmoja.
- Njia za mpango wa uzazi-vidonge
- Kansa ya kizazi
- Magonjwa ya zinaa kama klamedia au kisonono
- Kutumia sabuni zenye marashi makali kusafishia uke/kutumia mafuta yenye harufu kali ukeni
- Maambukizi katika mfumo wa uzazi baada ya upasuaji wakati wa kujifungua.
- Maambukizi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke (PID)
- Ugonjwa wa malengelenge sehemu za siri (trichomoniasis), unaosababishwa baada ya kufanya ngono zembe.
- Uke kuwa mkavu kwa wanawake waliofikia ukomo wa kuzaa
- Ugonjwa wa fangasi ukeni (yeast infection)
Aina ya uchafu unaotoka ukeni na chanzo chake
Aina ya uchafu | Maana yake ni nini? | Dalili nyingine |
Rangi ya damu au kahawai(hudhurungi) | Ishara ya mzunguko wa hedhi uliovurugika (irregular menstrual cycle), kansa ya kizazi au kansa katika mfuko wa uzazi. | Utokaji wa damu ukeni usio wa kawaida, maumivu ya nyonga. |
Rangi yenye mawingu au njano (cloudy or yellow) | Kisonono | Damu kabla na baada ya siku yako ya hedhi, maumivu ya nyonga,kushindwa kuzuia mkojo. |
Uchafu wenye rangi njano au kijani unaotoka kama povu na wenye harufu mbaya. | ugonjwa wa trichominiasis | Maumivu na muwasho kila unapokojoa. |
Uchafu wenye rangi ya pinki. | Tabaka lililojishika ndani ya ukuta wa mfuko wa uzazi linatoka nje ya mwili baada ya kujifungua (lochia-kutokwa damu baada ya kujifungua) | |
Uchafu mzito, mweupe, unaofanania jibini | Ugonjwa wa fangasi ukeni. | Maumivu na kuvimba kuzunguka uke (vulva), muwasho, maumivu wakati wa kujamiana. |
Uchafu mweupe, rangi ya kijivu, au njano wenye harufu ya shombo ya samaki. | Bakteria ukeni | Muwasho au kuungua, wekundu na kuvimba uke au ndani ya uke (vagina au vulva) |
Chanzo cha uchafu kutoka ukeni kipindi cha ujauzito ni nini?
Ujauzito unaweza kukuchanganya kadiri unavyoendelea kukua, sio rahisi kujua mabadiliko yapi ni kawaida na yapi yanahitaji uharaka wa kuwasiliana na mkunga wako au kutembelea kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi. Mojawapo ya mabadiliko haya ni kutokwa uchafu ukeni, ambao unabadilika katika muda wa kutokea,mara ngapi unatokea,muonekano, kiasi,na uzito wake kipindi cha ujauzito.
Moja ya ishara za awali za ujauzito ni ongezeko la uchafu unaotoka ukeni, hali hii inaendelea kipindi chote cha ujauzito. Kwa kawaida uchafu unaotoka ukeni (leukorrhea) ni mwembamba, unaonekana vizuri (clear) au una rangi ya maziwa meupe na unatoa harufu kidogo.
Mabadiliko ya viwango vya homoni mara baada ya kuwa mjamzito yanasababisha mabadiliko ya uchafu unaotoka ukeni. Mabadiliko ya mlango wa uzazi kipindi cha ujauzito yanachangia kuathiri uchafu unaotoka ukeni. Kulainika kwa mlango wa uzazi na ukuta ndani ya uke, kunasababisha mwili kutoa uchafu zaidi ili kujikinga na maambukizi. Unapokaribia mwisho wa ujauzito kichwa cha mwanao kinaweza kuleta mgandamizo katika mlango wa uzazi na kupelekea ongezeko la uchafu unaotoka ukeni.
Kipindi chote cha ujauzito inategemewa mama mjamzito kupitia dalili kama mkojo kuvuja, kutoka uchafu, kuwashwa, na kuona damu katika nguo za ndani.
Katika makala hii utaweza kujua aina gani ya uchafu unaotoka ukeni ni kawaida na upi una ashiria tatizo linalohitaji kumuona daktari. Ili kujua aina gani ya uchafu unaotoka ukeni wakati wa ujauzito ni kawaida, tujifunze zaidi kuhusu vyanzo vyake:
Uchafu wa kawaida ukeni
Matone ya damu katika nguo zako za ndani
Hakuna kitu kinacho ogopesha kama kutokwa damu bila kutarajia. Wanawake wengi wanaona damu kidogo katika nguo zao za ndani katika kipindi cha miezi mitatu ya awali baada ya kufanya tendo la ndoa au uchunguzi wa mfumo wa uzazi katika miadi. Mara nyingi hali hii inaashiria yai lililo rutubishwa limefanikiwa kupandikizwa kwenye ukuta wa mfuko wa mimba (implantation) au muwasho katika mlango wa kizazi.
Kuona damu katika nguo zako za ndani kipindi cha mwisho cha ujauzito inahusiana na kuwa na kiasi cha ziada cha damu na homoni zinazopelekea mishipa iliyopo kwenye mlango wa uzazi kutoa damu. Wakati mwingine ina ashiria kujifungua kuna karibia, lakini pia inaweza kuashiria tatizo kubwa la kiafya kama- kondo la nyuma kuachia kabla mtoto kuzaliwa. Kila unapoona matone ya damu kwenye nguo zako za ndani yasio kawaida (rangi nyekundu inayong’aa) mjulishe mkunga wako.
Unyevu katika nguo za ndani(chupi)
Je, unyevu kwenye nguo za ndani ni ishara chupa yako imepasuka? Inawezekana ni mkojo, ikiwa unavuja kila unapo cheka, piga chafya au kukohoa. Kuvuja mkojo ni kawaida kipindi cha ujauzito, inatokea kwasababu ya mgandamizo wa uterasi inayoendelea kukua. Mazoezi maalumu- “kegel” yanasaidia wanawake wengi kuweza kudhibiti vibofu vyao. Unaweza kufanya utaratibu wa kuwahi chooni dakika chache kabla ya kubanwa mkojo vizuri. Kumbuka usiache kunywa maji ya kutosha hata kama unavuja mkojo bila kutarajia. Ikiwa unahisi maji yanayovuja sio mkojo bali chupa ya uchungu imepasuka, fanya utaratibu wa kuwasiliana na mkunga wako au wahi kituo cha afya.
Uchafu usio kawaida ukeni.
Ugonjwa wa fangasi ukeni
Maambukizi haya yana ambatanana muwasho, wekundu na kuvimba kuzunguka uke, baadhi ya wanawake wanapata maumivu wakati wa tendo la ndoa na kuungua wakati wa kukojoa. Uchafu huu una rangi ya njano au nyeupe inayofanana na jibini. Fangasi wanaishi ndani ya mwili na kwenye uke muda wote, lakini ujauzito unatengeneza mazingira ya fangasi kuzaliana.
Muone daktari akupatie ushauri wa dawa sahihi kwaajili ya maambukizi haya. Punguza sukari kwenye mlo wako (fangasi wanapenda sukari) na hakikisha unabadilisha nguo yako ya ndani (chupi) mara kwa mara.
Bakteria ukeni (Bacterial vaginosis-BV)
Maambukizi haya yanasababishwa na kukosekana kwa uwiano sawa wa bakteria asili wanaopatikana ukeni. Uchafu huu unaonekana zaidi baada ya kufanya tendo la ndoa,unaambatana na muwasho au kuungua kila unapojisaidia. Vile vile unakua na harufu ya shombo ya samaki ukiwa mjamzito. Maambukizi haya yasipotibiwa vizuri yanaweza kusababisha matitizo makubwa kwenye ujauzito. Kawaida maambukizi haya yanaanza katika uke, lakini baadae yanapanda kwenye uterasi na kusababisha kuraruka membreni mapema na kujifungua kabla ya wiki ya 37.
Ikiwa unahisi una dalili za maambukizi haya, muone daktari haraka. Dawa sahihi zinaweza tokomeza dalili zote bila kuhatarisha mtoto tumboni na kupunguza nafasi ya kujifungua kabla ya wiki 37.
Magonjwa ya zinaa
Wakati mwingine uchafu wenye rangi ya njano wakati wa ujauzito unaashiria kisonono, na uchafu unaotoka kama povu wenye rangi ya kijani au njano wakati wa ujauzito unaonyesha ugonjwa wa “trichomoniasis” zaidi ya hayo, uchafu ulio na harufu unasababishwa na klamedia. Maambukizi haya matatu ya zinaa yanaweza sababisha maumivu wakati wa tendo la ndoa au kujisaidia. Kuwa na magonjwa ya zinaa wakati wa ujauzito inapelekea kujifungua kabla ya wiki 37 na maambukizi ya mfuko wa mimba baada ya kujifungua.
Baadhi ya vijidudu vinavyosababisha magonjwa haya ya zinaa vinaweza penya kupitia plasenta na kuathiri kijusi, mengine yanaweza kusambazwa kwa mtoto wakati wa kujifungua.
Ikiwa unahisi una maambukizi ya magonjwa ya zinaa wahi kituo cha afya mara moja, ukapimwe na daktari na kupatiwa antibaotiki sahihi. Habari njema ni kuwa magonjwa haya mengi yanaweza kutibika kwa antibaotiki sahihi.
Jinsi gani uchafu unaotoka ukeni unatibiwa?
Aina ya matibabu yatategemea na nini chanzo cha uchafu. Kwa mfano maambukizi ya fangasi ukeni yanatibiwa na dawa za antifungal zinazowekwa ndani ya uke. BV inatibiwa na antibaotiki. Ugonjwa wa malengelenge sehemu za siri unatibiwa na madawa kama “metronidazole(Flagyl) au tinidazole (Tindamax).
Vifuatavyo ni vidokezo kwa wanawake wote(wajawazito na wasio wajawaazito) vya kuzuia maambukizi ukeni ambayo yanapelekea uchafu usio kawaida ukeni:
- Weka uke wako safi kwa kusafisha taratibu, sabuni kidogo na maji vuguvugu kwa nje. Hakuna haja ya kutumia sabuni moja kwa moja kwenye uke.
- Epuka kuosha uke kwa kutumia sabuni zenye manukato au mbinu yoyote ile kwa sababu huongeza kujikuna. Uke wenye afya hauhitaji marashi au manukato.
- Baada ya kutoka bafuni, siku zote jifute kuanzia mbele kurudi nyuma kuepuka bakteria kuingia ukeni na kusababisha maambukizi.
- Ongeza mtindi katika mlo wako ili kukuza bakteia wenye afya.
- Tumia chupi iliyotengenezwa kwa pamba au chupi ambayo haitakuchoma na badilisha chupi kila siku.
- Usivalie nguo za kukubana kwa sababu zinafanya mwili kuwa na unyevu na kisha husababisha vidudu kusambaa kwa haraka.
- Osha chupi kwa maji moto na sabuni kisha ukamue chupi hizo kwa maji masafi kabla ya kuanikwa.
- Badilisha nguo zenye unyevunyevu baada ya kuogelea au nguo za michezo baada ya mchezo bila kukawia.
Kumbuka
Ni muhimu kuwasiliana na daktari au mkunga anayesimamia ujauzito wako kama unatokwa uchafu usio wa kawaida ukeni, maana inaweza kuwa ishara ya maambukizi au tatizo kwenye ujauzito wako.
CDC (Centre for diseases control and prevention) wanashauri wajawazito wote kuchunguzwa magonjwa ya zinaa katika miadi ya kwanza ya kliniki.
Uchafu usio wa kawaida unaweza kuwa ishara ya tatizo kubwa kwenye ujauzito wako. Wasiliana na mkunga anayesimamia ujauzito wako ikiwa utaona uchafu ukeni wenye rangi nyekundu inayong’aa. Inaweza kuwa ishara ya tatizo la kondo la nyuma kuachia kabla mtoto kuzaliwa au placenta previa (kondo la nyuma hujipachika katika sehemu ya chini ya mfuko wa uzazi)
IMEPITIWA: MEI,2021.