Mtoto wako anaweza kupendelea zaidi kuchezea maji, lakini kuna kanuni muhimu kufuatwa ili kufanya muda wa kuoga salama na vilevile wa kufurahisha. Kanuni ya kwanza na muhimu ni usimwache mtoto peke yake ndani ya beseni wakati wa kuoga.
Joto gani la maji lafaa kwaajili ya kumuogesha mtoto?
Hakikisha maji ya kuoga ya mtoto wako yana uvuguvugu wa kutosha kabla ya kumuweka mtoto wako. Weka maji ya baridi kwanza, kisha ongeza maji ya moto.
Changanya maji vizuri ili kuhakikisha hakuna maeneo yenye joto zaidi. Hii itapunguza hatari ya kumuunguza mtoto wako. Kamwe usimuweke mtoto ndani ya chombo cha kumuogeshea(beseni) ukiwa unamimina maji. Jotoridi la maji linaweza kubadilika haraka sana na mtoto kuungua ndani ya sekunde chache.
Unaweza kununua kipima joto kuhakikisha jotorii la maji ya kuoga ni sawa. Baadhi ya vipima joto ni midoli mizuri ya kuchezea wakati wa kuoga. Maji ya kuoga ya mtoto yanatakiwa kuwa na joto la digrii 37 za sentigredi mpaka 38, ambalo ni sawa na joto la mwili.
Ikiwa hautumii kipimajoto njia nzuri ya kupima joto la maji kwa haraka ni kwa kutumia kiwiko chako kuliko kiganja cha mkono kujua jotoridi la maji.
Japokua maji ya kuoga yana joto, mtoto anaweza hisi baridi mara umtoapo kwenye maji, hivyo ni vyema kuweka mazingira ya kumpa joto mara atokapo kwenye beseni la maji. Mara umwinuapo mtoto kutoka kwenye maji mfunike kwa taulo kavu na mfute akauke kabla ya kumvalisha nepi kavu na nguo.
Kina gani cha maji ni sawa kwa maji ya mtoto.
Kwa watoto wachanga mpaka miezi 6, jaza maji katika beseni karibu 8sm mpaka 10( inchi 3 mpaka 4). Kamwe usijaze maji kupitiliza na usimuweke mtoto ndani ya beseni kisha umimine maji, kwani joto la maji linaweza kubadilika haraka.
Jinsi gani naweza msaidia mtoto wangu pindi yuko ndani ya maji?
Unapomuweka mtoto ndani ya maji mshike kwa nguvu chini ya matako kwa mkono mmoja. Weka mkono mwingine chini ya shingo yake kwa nyuma karibu na mabega. Mara mtoto wako akikaa vizuri ndani ya beseni au chombo unachomuogeshea, tumia mkono wako uliomshikilia sehemu ya chini ya matako kumwagia maji kuzunguka mwili wake. Kaza mwili wako kwenye mwili wa mtoto na pia msaidie kuweka kichwa chake juu ya maji ili asizame.
Kamwe usimwache mtoto pekee yake ndani ya beseni. Hata kama mtoto wako mwingine mkubwa yupo nae bafuni au kwenye beseni, ni vema kukaa na kumshika au kumwangalia mwanao.
Watoto wadogo wanaweza kuzama ndani ya maji yenye kina cha chini ya 5 sm (2inch) na inachukua sekunde chache tu kwa mtoto kuteleza ndani ya maji au kujizungusha kwenye maji bila msaada. Kawaida watoto hawalii au kupambana mara wanapoingia ndani ya maji, hivyo inakua vigumu kugundua kama hatari imetokea kwa mwanao.
Je, nimwogeshe mwanangu mara ngapi?
Ni uamuzi wako. Kuoga knaweza kuwa wakati wa furaha na kupumzika kwako na mwanao. Lakini kama hupendi kumuogesha mwanao kila siku, ni sawa kumuogesha mara mbili au tatu kwa wiki.
Siku ambazo mtoto haogi unaweza kumfuta kwa kitambaa safi chenye unyevu na kumbadili nguo, pia kuosha uchafu uonekanao tu.
Pindi mtoto wako atakapokua na umri wamiezi michache, itakubidi kuoga kuwe moja ya ratiba yake ya kila siku, asubuhi( midaa ya saa nne mpaka saa tano) na kabla ya kulala. Lakini pia ratiba hii itegemee hali ya hewa ya eneo. Chagua sabuni nzuri na salama kwa mtoto, ili kusaidia kudumisha mng’ao mzuri wa ngozi ya mwanao.
Ikiwa mtoto wako ana ngozi kavu na yakuwasha, ongeza mafuta ya kuogea (bath emmolient) maalumu yanayosaidia kurudisha mng’ao wa mtoto kwenye maji. Kumbuka kukaza mikono maana mafuta haya maalumu ya kuogea hutelezakwenye ngozi ya mtoto.
Je, nimwoshe mwanangu nywele mara ngapi?
Huitaji kuosha nywele zake kila siku. Nywele zake hutengeneza mafuta kwa kiasikidogo, hivyo basi maramoja au mbili kwa wiki ni sawa.
Kama mtoto wako ana (cradle cap) – ngozi yenye rangi ya unjano au wekundu juu ya kichwa chake inayotokana na uzalishaji wa mafuta(sebum) na kufanya ukoko katika kichwa chake,ni vema kuosha nywele zake mara nyingi kwa sabuni au shampoo maalumu.
Epuka kutumia shampoo kama mtoto wako ana ukavu wa ngozi au muwasho badala yake tumia mafuta maalumu ya kuogea (emollient).
Je, naweza muacha mtoto wangu bafuni kwa dakika chache?
HAPANA. Kamwe usimuache mtoto pekee yake kwenye beseni.
Kabla ya kuanza kumogesha, hakikisha umeandaa kila utakachohitaji katika zoezi hili. Hakikisha taulo, sabuni, nepi safi na nguo ziko karibu na uwepo wako. Kipindi mtoto wako ni mchanga hakikisha una mahitaji ya kutosha maana watoto wanakojoa mara nyingi na kujisaidia haja kubwa wakati wowote na bila kutarajia.
Ikiwa simu yako itaita au mtu akagonga mlangoni, mnyanyue mwano kutoka kwenye maji na mfunike kwa taulo kisha mchukue pamoja na wewe.