Tumefanikiwa kuona picha mbalimbali, rafiki zetu na watoto wao wadogo walio umri mkubwa kidogo wakituma picha kwenye mitandao ya kijamii, watoto wao wakianza kula vyakula vigumu. Maranyingi kuna tabasamu za furaha na saa nyingine kuna sura za kukasrishwa au kutofurahishwa. Lakini kwa pamoja picha hizi zina ujumbe mmoja ambao ni chakula kingi juu ya mtoto kuliko chakula anachokula.
Muda unapita kwa kasi, na siku si nyingi utaanza suala zima la kumuanzisha chakula kigumu mtoto wako. Ikiwa ulifurahishwa na kumyonyesha mtoto wako miezi yote iliyopita, muda utakuja wa kumkalisha mtoto wako na kumuonjesha chakula kigumu. Habari njema ni kwamba wewe na mwenzi wako mna miezi kadhaa ya kumlisha mtoto maziwa au kumnyonyesha.
Ila swali kuu kwa wazazi wengi ni nini na lini, waanze kumlisha vyakula vigumu?
Mashirika makubwa ya afya duniani kama UNICEF na WHO yalikubaliana kuwa kumuanzisha mtoto vyakula vigumu kuanzishwe rasmi kuanzia mtoto akiwa na umri wa miezi sita huku ukiendelea kumnyonyesha.
Wakati wa mwanzoni ni vyema kuanza kumpa vyakula laini ukiwa unamjengea tabia ya kula vitu vigumu taratibu.
Baadhi ya watoto wako tayari kuanzishwa vyakula vigumu wakiwa na miezi mitano na nusu, wakati wengine wanaanza mwezi wa saba, kwa nini yote haya?
Sababu ni rahisi. Kwanza, kusubiri mpaka mtoto wako akiwa na miezi sita ina maana mtoto wako ana ongezeko la mfumo wa kinga tayari kwa kulinda mwili wake kutoka kwenye magonjwa yaletwayo na vyakula. Huu ni umri ambao mfumo wao wa mmeng’enyo unaanza kukua na kushughulikia mmeng’enyo wa fati, protini na kabohaidreti tata bila kuhitaji msaada wa dutu zinazotolewa na maziwa kusaidia mmeng’enyo ndani ya miezi hiyo michache ya kwanza. Kwa sababu hii ndio maana kumuanzisha mtoto vyakula vigumu kabla ya miezi sita hupelekea mtoto kuwa mnene (kiribatumbo) kipindi cha ujana na utu uzima.
Hata baada ya vyakula vigumu kuanzishwa, weka akilini mtoto wako bado atapata virutubisho vingi na kwa wingi kutoka kwenye maziwa ya kunyonya, kwa hiyo usipange kupunguza kumnyonyesha.