Kumfundisha Mtoto Kujisaidia Mwenyewe

Kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe ni hatua moja uliyokua unaisubiria kwa hamu sana. Japo kuna baadhi ya watoto wanaelewa ndani ya siku chache, kumbuka inaweza kuchukua miezi michache mwanao kuzoea tabia hii, japo kuna changamoto  katika safari hii.

Angalia utayari wa mwanao kujifunza kujisaidia mwenyewe

Hakuna umri maalumu wa kuanza kumfundisha mtoto kujisaidia, kwasababu kila mtoto ni tofauti. Kwa kawaida wazazi wananza kuwafundisha watoto kujisaidia wenyewe kati ya miezi 18 na miaka mitatu. Watoto wengi wanaanza wakiwa kati ya miaka miwili na miaka miwili na nusu.

Usijisikie kumlazimisha mwanao mapema kwasababu ya maneno ya wazazi wengine au familia yako. Angalia ishara kutoka kwa mwanao kama yuko tayari na usianze kabla ya hapo.

Fanya maandalizi ya kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe

Nunua poti la mtoto na chupi mpya. Matumizi ya poti ni njia rahisi ya kuanzia kuliko kutumia choo. Ni rahisi kukaa na kunyanyuka na linaweza kusogezwa sehemu yeyote ndani ya nyumba. Unaweza kutumia picha za kufurahisha na DVD zinazoonyesha matumizi ya poti, ili kumuhamasisha mtoto kuwa tayari zaidi kutumia poti.

Andaa chupi na kaptula za kutosha ambazo zitakua rahisi kuvua na kuvaa. Uvaaji wa chupi una mpa moyo mtoto kutumia poti.

 

Kuwa na msimamo katika njia utakayotumia kumfundisha mwanao kujisaidia mwenyewe

Fanya mambo taratibu unapoanza. Mhamasishe mwanao kukaa kwenye poti mara moja kwa siku,baada ya kifungua kinywa au kabla ya kuoga au wakati anaopendelea kujisaidia.

Mkalishe mwanao kwenye poti baada ya kukojoa kwenye nepi. Hii itamsaidia kumhamasisha kuzoea poti na kukubali ni moja ya utaratibu wake.

Ikiwa hataki kukaa, ni sawa. Usimlazimishe kukaa,mvalishe nepi na weka poti pembeni kwa wiki kadhaa kabla hujajaribu tena.

Ikiwa atakubali kukaa kwenye poti baada ya wiki kadhaa ni vizuri. Ila usimlazimishe kukaa kwenye poti kama hataki. Msubiri mpaka atakapokua tayari na muelekeze anachotakiwa kufanya. Ukimlazimisha mtoto kama hataki atakasirika na kuwa mgumu kutaka kujifunza kutumia poti.

Unaweza kugundua wakati wa kiangazi ni muda mzuri wa kumfundisha mwanao kutumia poti, ikiwa unaishi mji wenye baridi kali na unyevu kipindi kirefu cha mwaka. Wakati huu wa kiangazi nguo zinaweza kufuliwa na kukauka mapema pale mtoto atakapojisaidia.

Wataarifu watu wote wanaobaki na mwanao wakati umeenda kazini juu ya mpango wako wa kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe, ili watumie mfumo huo.

Muonyeshe inavyofanyika

Watoto wanapenda kuiga. Mtoto akiona unatumia choo itamsaidia kuona umuhimu wa kutumia choo. Kama una mtoto wa kiume anza kumfundisha kukojoa kwa kukaa.

Muonyeshe jinsi ya kutumia poti, “toilet paper” au maji kutawaza na jinsi ya kupandisha chupi na suruali mara baada ya kumaliza, kisha kumwaga maji chooni/flash na mwisho kabisa kunawa mikono na kukausha kwenye kitamba kikavu.

Wakati mwingine utamsaidia mtoto kutawaza baada ya kujisaidia haja kubwa. Ila kukuona unafanya itamsaidia hatua kwa hatua kuzoea na kufanya mwenyewe hapo baadae.

Ikiwa mtoto wako ana kaka yake aua dada yake, au rafiki yake ambaye anaweza kujisaidia mwenyewe, akiona wanatumia choo, ataweza kukuza ujuzi wake wa kujisaidia mwenyewe kwasababu anaona jinsi inavyotakiwa kufanyika.

Mhamasishe zaidi, kama yuko tayari kukaa kwenye poti

Mtie moyo mwanao kutumia poti anaposikia haja.  Mpatie maji mengi na mkumbushe akae kwenye poti kila baada ya masaa machache. Lakini mkumbushe kuwa anaweza kukuambia anaposikia kujisaidia, na utamsindikiza kama anataka kujisaidia chooni.

Ukiweza  mruhusu kucheza bila nguo chini na weka poti karibu. Mwambie anaweza kutumia poti kila anapotaka.

Mtoto wako akifanikiwa kutumia poti vizuri mpatie pongezi nyingi, japo ataendelea kuwa na ajali nyingi katika safari hii, ataanza kuelewa kufanikiwa kujisaidia kwenye poti ni moja ya mafanikio.

Kukabiliana na ajali zinzotokea wakati wa kumfundisha mwanao kujisaidia mwenyewe kwa hali ya utulivu

Mtoto atapitia ajali tofauti kabla ya kufanikiwa kujisaidia mwenyewe usiku na mchana. Inaweza kuchosha na kukatisha tama lakini usimuadhibu au kumkasirikia. Kufuzu hatua hii itachukua mda. Akijisaidia pembeni, kwa hali ya utulivu safisha bila kumgombeza ila mkumbushe mara nyingine ajisaidie kwenye poti. Kisha mkalishe kwenye poti baada ya kusafisha na muonyeshe kuwa haja ndogo na kubwa “wee na poo” vinapaswa kuenda kwenye poti.
Ajali ni moja ya utaratibu mzima wa kumfundisha mtoto kujisaidia mwenyewe. Lakini ikiwa ajali zitakua nyingi zaidi ya mafanikio, rudi kwenye matumizi ya nepi na acha kumfundisha matumizi ya poti kwa mda. Mwanao anaweza asiwe tayari.

Mafunzo ya kujisaidia mtoto wakati wa usiku

Inaweza kuchukua miezi mingi zaidi hata mwaka mwanao kufuzu kukaa mkavu wakati wa usiku. Hivyo basi,usitupe nepi kwanza. Mwili wake bado haujakua vizuri kumfanya aamke wakati wa usiku mwenyewe na kwenda chooni kujisaidia.

Wazazi wengi wanaanza kuwafundisha watoto wakiwa na miaka mitatu na minne. Unaweza kujaribu kabla ya umri huo,lakini hakikisha unaweka mpira wa kuzuia mkojo chini ya shuka au juu ya shuka.

Usimruhusu mtoto kunywa sana kinywaji chochote wakati wa usiku ili kupunguza nafasi za mtoto kukojoa kitandani wakati wa usiku. Mpatie maji ya kutosha wakati wa mchana kila anapo omba. Unaweza msaidia kwa kumkumbusha anaweza kukuamsha usiku kama atahitaji kujisaidia.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.