Kujifungua kwa Njia ya Upasuaji

Kujifungua kwa njia ya upasuaji, kwa lugha ya kigeni “C-section” ni njia ya kujifungua mtoto kwa kuchana kuta za sehemu ya chini ya tumbo na mji wa mimba (uterasi) ili kutoa mtoto aliye kwenye mji wa mimba.

Katika kipindi fulani kabla uchungu kutokea mama anajua kwa uhakika atajifungua kwa njia fulani, lakini hali tofauti za kiafya zinaweza kubadilisha mpango huo.

Daktari au mkunga anaweza kuamua utajifungua kwa njia ya upasuaji mara moja ukiwa katika uchungu au ukiwa katika chumba cha kujifungua. Mabadiliko haya ya haraka yanaweza kutokea ikiwa afya yako au mtoto aliyeko tumboni imebadilika ghafla na kuwa mbaya, hivyo kufanya kujifungua kwa njia ya kawaida kuwe hatari kwa afya ya mama.

Ni busara kujifunza anachopitia mama wakati wa kujifungua kwa njia ya upasuaji hata kama sio mpango wako wa kujifungua, itakusaidia ikiwa mabadiliko yatatokea katika chumba cha kujifungulia na kuhitajika upasuaji ili kuokoa maisha yako na mtoto wako.

Kujifungua kwa njia ya upasuaji ni salama kwa mama na mtoto. Lakini ni upasuaji mkubwa, inashauriwa isichukuliwe kimzaha.

Aina za Kujifungua kwa Njia ya Upasuaji

Upasuaji Uliopangwa

Ikiwa unajua mapema utajifungua kwa njia ya upasuaji, unapata nafasi ya kujua tarehe ya kujifungua na kutopitia uchungu wa kuzaa. Kabla ya utaratibu huu kufanyika utapata dripu ili mwili wako uwe na dawa na majimaji. Utawekewa pia mpira wa mkojo kusaidia kukusanya mkojo katika kibofu chako kipindi cha upasuaji na wakati ukiendelea kupona wodini.

Kama utajua mapema kuwa utajifungua kwa upasuaji, utapata muda kwa kutosha kujitayarisha, lakini kama ni upasuaji wa dharura inaweza kukushtua. Utachomwa sindano ya kaputi kisha kulazwa kwenye kitanda cha upasuaji. Wakati mwingine inaweza ikahitajika kuchomwa sindano ya kaputi ambapo utakuwa hutambui kinachoendelea mpaka utakapoamka. Faida nyingine ni kwamba utaweza kumuona mtoto wako mara tu anapotolewa tumboni. Daktari atakuruhusu umbebe mara baada ya upasuaji kumalizika. Kama una mpango wa kumnyonyesha mtoto wako, unaweza kujaribu kumlisha mtoto. Lakini sio kila mama anapata nafasi ya kumbeba mtoto wake mara baada ya upasuaji.

Wakati mwingine watoto waliozaliwa kwa njia ya upasuaji wanapata shida ya upumuaji, hali hii inawafanya kuhitaji msaada kutoka kwa madaktari. Usiwe na wasiwasi utaweza kumbeba mtoto wako mara baada ya daktari kuamua kuwa ana afya nzuri na hali yake iko salama.

Baada ya mtoto kuzaliwa, daktari atatoa plasenta yako na kukushona. Utaratibu wote huu utachukua dakika 45 mpaka lisaa limoja tu.

Sababu za Upasuaji Uliopangwa

Daktari au mkunga wako anaweza kukupangia kujifungua kwa upasuaji siku ya kujifungua ikiwa una:

  • Aina fulani ya matatizo ya kiafya. Magonjwa makubwa kama magonjwa ya moyo, kusukari, shinikizo kubwa la damu au tatizo la kibofu cha mkojo ni baadhi ya matatizo yatakayofanya kujifungua kwa kawaida kuwe hatari kwa mwili wa mjamzito.
  • Maambukizi. Ikiwa wewe ni muathirika wa ugonjwa wa Ukimwi au una ugonjwa wa zinaa ambao haujapona, upasuaji wakati wa kujifungua ni jambo lisilo epukika. Hii ni kwasababu virusi vinavyosababisha magonjwa haya vinaweza ambukizwa kwa mtoto kipindi cha kujifungua.
  • Afya ya mtoto. Ugonjwa kurithi unaweza fanya safari ya mtoto kupita ukeni kuwa changamoto kwa mtoto wako.
  • Mtoto mkubwa.
  • Uzito wa mjamzito. Kuwa na uzito mkubwa au uzito uliopitiliza kunaongeza nafasi ya mjamzito kujifungua kwa njia ya upasuaji kwa sababu ya shida mbalimbali zinazoambatana na uzito mkubwa kama vile kisukari wakati wa ujauzito, lakini pia kwasababu wanawake wenye uzito mkubwa wa mwili wanapitia uchungu wa kuzaa unaochukua muda mrefu.
  • Mtoto akikaa mkao wa tofauti tumboni (breech position). Mtoto anapotanguliza miguu kwanza na ikashindikana kumgeuza, mkunga wako ataamua upasuaji ni lazima.
  • Ujauzito wa mapacha au zaidi.
  • Tatizo ya kondo la nyuma kujishikiza karibu na mlango wa kizazi. Pale kondo la nyuma limejishikiza karibu na shingo ya uzazi, sio rahisi kujifungua kwa njia ya kawaida kwasababu mtoto hatapita vizuri. Kawaida plasenta ina kazi ya kuingiza virutubisho kwa mtoto, kumpa hewa safi na kuondoa hewa chafu. Ikiwa plasenta imezuia kidogo au sana mlango wa uzazi (placenta previa) upasuaji ni njia pekee salama kwako na mtoto wako.
  • Kondo la nyuma kuachia kabla ya muda wa kujifungua (placenta abruption). Endapo kondo la nyuma limenyofoka au sehemu ndogo kuachana na ukuta wa kizazi, upasuaji wa haraka hauna budi kufanyika ili kuokoa maisha ya mtoto. Upasuaji ukichelewa kufanyika mtoto atazaliwa amechoka au wakati mwingine kufia tumboni kwasababu ya ukosefu wa virutubisho na hewa safi.
  • Matatizo mengine hatari ya kiafya. Matatizo kama ujauzito unaosababisha shinikizo kubwa la damu au shinikizo la damu linalokua taratibu na kuathiri mfumo wa kati wa fahamu na kusababisha mama kupoteza fahamu na wakati huohuo hakuna tiba inayofanya kazi. Mkunga wako atashauri upasuaji ili kulinda afya za wote.
  • Ombi la mama. Mjamzito anaweza kuomba kufanyiwa upasuaji kwasababu za kibinafsi. Mkunga anaweza kumzikiliza mama na kumshauri njia salama kulingana na ombi la mama.
  • Ikiwa ulijifungua kwa upasuaji ujauzito wa awali. Mama aliyejifungua kwa upasuaji ujauzito wake wa awali anaweza kujaribu kujifungua kwa njia ya kawaida endapo kovu limepona vizuri, afya yako iko salama na sababu iliyokufanya ukafanyiwa upasuaji katika ujauzito wako wa awali hazipo.
  • Upasuaji unafanyika ikiwa mtoto ni wa kipekee. Kwa wanandoa ambao wamepata shida katika kutafuta mtoto kwa muda mrefu, wanaweza kuamua upasuaji ufanyike wakati wa kujifungua ili kuhakikisha mama na mtoto hawapati madhara wakati wa kujifungua. Wanawake waliopata mimba ya kwanza kwenye umri mkubwa sana kwa mfano miaka zaidi ya 35, wanawake waliopata shida ya mimba kuharibika sana au mtoto kufariki wakati wa kujifungua huchagua upasuaji wakati wa kujifungua.

Upasuaji wa Dharura

Wakati wa upasuaji wa dharura, mambo machache yatabadilika ikiwa ni pamoja na kasi na uharaka wa operesheni. Daktari anaweza kumzalisha mtoto wako kwa dakika mbili baada ya kuchana uterasi yako (inachuka dakika 10 mpaka 15 kwa upasuaji uliopangwa).

Ikiwa mtoto wako anashida katika upumuaji au mapigo ya moyo hayako sawa, madaktari watahitaji kumtoa haraka ndani ya mji wa mimba na kumuwahisha hosspitali kwaajili ya huduma za kitabibu haraka ili aweze kuwa salama.

Katika upasuaji wa dharura kwa kawaida utachomwa sindano ya uti wa mgongo, itakayokufanya usisikie maumivu kuanzia kwenye nyonga kwenda chini. Au ukapigwa kaputi na kulala upasuaji mzima. Kwa bahati mbaya hutasikia au kumuona mtoto wako akiwa anazaliwa, ila hautasikia maumivu au mkandamizo wowote katika tumbo lako la uzazi. Habari njema ni kwamba, baada ya kuzinduka utaweza kumbeba, kumuona na kumlisha kichanga wako.

Upasuaji wa dharura unafanyika pale:

  • Ikiwa kitovu kitatoka nje kabla mtoto, hali hii itasababisha usambazaji wa hewa ya oksijeni kukatishwa.
  • Uterasi ikichanika.
  • Uchungu umechelewa kuanza au hauendi kama inavyotakiwa. Kutoendelea au kusimama kwa uchungu ni moja ya sababu kubwa inayopelekea wajawazito wengi kujifungua kwa upasuaji. Hali hii inapelekea shingo ya uzazi kutofunguka na kupelekea mtoto kushindwa kutoka. Kwa kawaida mkunga au daktari huangalia hali ya shingo ya kizazi mara kwa mara kwa kuingiza vidole viwili kupitia uke, kwa kufanya hivi atagundua kwa kiasi gani (sentimita) ngapi shingo ya uzazi imetanuka. Hii ni njia mojawapo ya kuangalia maendeleo ya uchungu.
  • Mjamzito kuchoka au mtoto kuchoka. Ikiwa daktari atakuona umechoka au kipimo maalum kinachowekwa kwenye tumbo kuangalia mapigo ya moyo ya mtoto kuonyesha dalili za mtoto kuchoka daktari ataamua upasuaji wa haraka ufanyike.

 Upasuaji wakati wa kujifungua unachukua muda gani?

Upasuaji ni haraka, procedure yenyewe inachukua dakika 10 au pungufu, ikifuatiwa na dakika nyingine 30 za kushona.

Nini hutokea wakati wa upasuaji?

Iwe ni upasuaji uliopangwa tangu awali au wa dharura, upasuaji wa kawaida unafuata mpango maalum.

Maandalizi na sindano ya nusu kaputi

Utafanyiwa vipimo vya damu ili kuangalia wingi wa dam una kundi la damu ili pale itakapotokea shida baada ya upasuaji damu iongozwe kiurahisi. Upasuaji unaanza kwa utaratibu wa dripu na sindano ya kaputi ili sehemu ya chini ya mwili ili usiweze kusikia maumivu na mgandamizo wowote lakini utakua macho na utafanikiwa kushuhudia pale mwanao anapotolewa ndani ya mji wa mimba. Kisha sehemu cha chini ya tumbo la uzazi litanyolewa (kama inahitajika) na kusafishwa kwa dawa maalum ya kuua vijidudu. Utawekwa mpira wa kukusanya mkojo kipindi cha upasuaji na wakati ukiendelea kupona wodini.

Ikiwa unahitajika kufanyiwa upasuaji wa dharura, utachomwa dawa ya kukufanya ulale kipindi kizima cha upasuaji ambayo mara nyingi huchukua dakika chache. Ukiamka utasikia kusinzia kwasababu ya dawa ya usingizi, utajisikia kichefuchefu na kuchoka sana. Unaweza pia kuwa na koo kavu iliyosababishwa na mrija wa kupeleka hewa kwenye mapafu unaowekwa wakati wa upasuaji.

Kuchanwa na kuzaa

Mara baada ya sehemu ya chini ya mwili kufa ganzi au kulala, daktari atachana kidogo kwenye sehemu ya chini ya tumbo-juu kidogo ya uke. Kovu la mchano huu hupotea kadiri mda unavyoenda ikiwa kazi ilifanyika kwa umakini. Daktari atachana tena ndani sehemu ya chini ya uterasi. Zipo aina mbili za michano:

Mchano mlalo. Unatumika kwa asilimia 95 wakati wa upasuaji, kwasababu misuli chini ya uterasi ni mwembamba hivyo damu kutoka kidogo. Pia sio rahisi kuachia wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida hapo baadae.

Mchano wima. Aina hii ya mchano inafanyika pale mtoto amekaa sehemu ya chini ya uterasi au amekaa katika mkao usio kawaida.

Baada ya hapo maji yanayopatikana tumboni mwa mama mjamzito yanayomzunguka mtoto kwenye hatua zake zote za ukuaji hufyonzwa nje, kisha mtoto wako atatolewa nje. Kwasababu uteute wa ziada haukutolewa vizuri nje ya njia ya hewa ya mtoto wako, ufyonzwaji wa ziada utahitajika ili kuhakikisha mapafu ya mwanao ni safi kabla ya kumsikia mtoto wako akilia kwa mara ya kwanza.

Kumbeba mtoto wako kwa mara ya kwanza

Baada ya kitovu kukatwa, daktari ataondoa placenta, kisha kukagua haraka ogani zako za uzazi kabla ya kuanza kukushona. Kisha ushonaji wa sehemu uliochanwa utafanyika, ambao unachukua dakika 30 au zaidi.

Utapokea dawa ya kupunguza nafasi ya kidonda kupata maambukizi na “oxytocin” ya kudhibiti damu kutoka na kusaidia uterasi kubana na kurudi katika hali yake ya awali katika dripu. Shinikizo lako la damu, mapigo ya moyo na kasi yako ya upumuaji na wingi wa damu inayotoka utaangaliwa mara kwa mara.

Kama utakuwa umejifungua kwa upasuaji utahitaji kuendelea kukaa hospitali kwa siku kadhaa uanze kupona. Kupona baada ya upasuaji ni sawa tu na kupona kwa upasuaji mwingine wa eneo la tumbo. Tofauti kubwa ni kwamba badala ya kupoteza kiungo kimoja kama figo au “appendix” unapata mtoto.

Mojawapo ya matatizo unayoweza kuyaona baada ya kujifungua ambayo ni ya kawaida ni kama hali ya kusikia maumivu kwenye uke, kutokwa na damu nzito nyeusi, matiti kuvimba, nywele kudondoka, uchovu na kutokwa jasho jingi.

Tegemea Yafuatayo Baada ya Kutoka Chumba cha Upasuaji.

Daktari wako atakuchunguza kwa karibu mpaka pale dalili zote za dawa za kuondoa maumivu zimeisha. Kumbukumbu zako zinaweza zikawa zinasumbua kama ulitumia dawa ya usingizi au nusu kaputi. Madhara ya sindano ya nusu kaputi inayochomwa kwenye uti wa mgongo huchukua muda mrefu zaidi kuliko madhara ya dawa za usingizi.

Baada ya dawa ya kuondoa maumivu kuisha utaanza kusikia kidonda kinauma. Ukali wa maumivu unategemea sababu tofauti, ikiwemo uwezo wako wa kusikia maumivu na kama una historia ya kujifungua kwa upasuaji hapo awali, kwani maumivu ya upasuaji wa pili na kuendelea huwa yanaonekana sio makubwa sana kama yale uliyoyasikia kwenye upasuaji wa kwanza. Utapewa dawa za maumivu kupambana na hali hii.

Unaweza ukasikia kichefuchefu, ambapo daktari atakupatia dawa itakayokuzuia kupata kichefuchefu au kutapika.

Nesi atakuwa anakuchunguza mara kwa mara. Atakuwa anachukua vipimo vyako muhimu (joto, shinikizo la damu (BP), na upumuaji). Atakuwa pia anaupima mkojo wako na chochote kinachotoka ukeni. Pia atakuwa anaangalia mfungo wa kidonga chako cha upasuaji, sehemu mfuko wako wa uzazi ulipo na ugumu wake na wakati huo huo akihakikisha mirija ya dripu na mpira wa mkojo ipo sehemu yake.

Kama hali yako itaendelea vizuri, utapelekwa kwenye wodi ndani ya masaa kadhaa baada ya upasuaji kufanyika. Uchunguzi wa vipimo vyako muhimu utafanyika kwa mara nyingine. Kama una uwezo wa kukojoa mwenyewe basi mpira wa mkojo utatolewa masaa 24 baada ya upasuaji.

Unaweza ukawa unasikia maumivu kwenye uke kama mwanamke aliyejifungua kwa njia ya kawaida. Hii isikupe wasiwasi maumivu haya ni kutokana na kukaza kwa misuli ya mfuko wako wa uzazi ukiwa unajirudia kwenye hali yake kabla ya ujauzito.

Dripu za maji zitatolewa na utaruhusuwa kuanza kutumia vinywaji kwa kunywa mwenyewe masaa 24 baada ya upasuaji (Huu ndio muda ambao utumbo wako utakuwa umeshaanza kusogeza chakula kawaida na kufanikiwa kutoa hewa chafu nje kwa njia ya kujamba). Taratibu utaruhusiwa kurudia mlo wako wa kawaida kadiri siku zinavyosogea. Mama wanaonyonyesha inabidi wapate maji ya kutosha mwilini.

Utategemea kutolewa nyuzi zako (Kama sio zile zinazoyeyuka zenyewe) ndani ya siku 4 hadi 6 baada ya upasuaji.

Mwishoni kabisa kama kila kitu kitakuwa kimeenda sawa kwako na mtoto, utaruhusiwa kurudi nyumbani ndani ya siku 3 hadi 7 baada ya upasuaji.

Hali gani hatari za kiafya zinazoweza kutokea baada ya kujifungua kwa upasuaji?

Kujifungua kwa njia ya upasuaji ni salama kabisa, lakini mara chache matatizo ya kiafya yanatokea kwa mama na mtoto baada ya upasuaji kufanyika.

Kwa mama, matatizo haya ni pamoja:

  • Kupoteza damu,
  • Mama kupata maambukizi eneo la mshono.
  • Muitikio mbaya wa dawa zinazotumika kipindi cha upasuaji (dawa za nusu kaputi, dawa za kupunguza maumivu n.k).
  • Kujeruhiwa wakati wa upasuaji,
  • Damu kuganda kwenye mishipa ya damu haswa miguuni,viungo ndani ya nyonga na mapafu. Huku madaktari wakifanya kila namna kuhakikisha hali hii haitokei, ni vizuri ukatembea baada ya upasuaji kama unaweza.
  • Mara chache sana, uterasi inaweza kuvimba au kuwasha.
  • Maambukizi katika kuta za kizazi
  • Mama kupata hatari ya kujifungua kwa upasuaji upasuaji unaofuata.

Hatari za kiafya za muda mrefu ni pamoja na: kupata kovu baya kwenye eneo la mshono na kuchanika kizazi kwenye ujauzito unaofuata.

Mtoto aliyezaliwa kwa njia ya upasuaji anaweza:

  • Kupitia kipindi cha mpito cha kupumua haraka haraka, kitakachodumu kwa siku chache baada ya kujifungua, hali hii inasababishwa na mabaki ya maji (yanayopatikana ndani ya mji wa mimba kumzunguka mtoto kipindi chote cha ujauzito) ndani ya mapafu ya mtoto.
  • Kama upasuaji umefanyika kabala ya wiki ya 39 ya ujauzito, mtoto atakuwa katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya kupumua ikiwa mapafu yake hayajakua vizuri-lakini kumbuka daktari atakua karibu nawe kumuangalia kwa ukaribu zaidi na kutibu aina yoyote ya tatizo litakalozuka ukiwa bado hospitalini.

Kumbuka

Ukishuhudia ongezeko la maumivu ya nyonga, kutokwa uchafu usio wa kawaida au homa baada ya mtoto kuzaliwa, wasiliana na daktari wako mara moja.

IMEPITIWA: AGUSTI, 2021.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.