Kipindi cha ujauzito mabadiliko mbalimbali hutokea katika mwili wa mjamzito ili kuruhusu ukuaji na maendeleo ya mtoto aliye tumboni, mabadiliko haya vilevile ni maandalizi ya mtoto kuzaliwa. Kiungulia ni miongoni mwa matatizo yanayowapata wanawake wengi wanapobeba mimba, tatizo hili huwapata wajawazito mara nyingi katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito na kwa wengine miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.
Kiungulia hutokea wakati kiwambo (valvu) kilichopo kati ya tumbo na koromeo la chakula (esophagus) kinapolegea na kushindwa kuzuia tindikali (acid) ya tumbo isipenye na kurudi katika koromeo la chakula na kusababisha maumivu makali kifuani. Ujauzito huongeza nafasi ya mama kupata kiungulia kwasababu homoni ya projesteroni hulegeza kiwambo hicho na kusababisha tindikali (acid) inayozalishwa tumboni hasa baada ya kula kurejea katika koromeo la chakula na kusababisha kiungulia.
Je, Kiungulia Kinasababishwa na Nini Wakati wa Ujauzito?
Ili kuelewa njia na mbinu za kuzuia kiungulia kisitokee ni vizuri kufahamu kiungulia kinasababishwa na ni nini wakati wa ujauzito.
Mabadiliko ya homoni
Wakati wa ujauzito kiwango cha homoni ya projesteroni huongezeka zaidi ili kuhakikisha mtoto tumboni anakua vizuri, lakini pia homoni hii inafanya misuli ilegee. Hali hii inaweza kupelekea misuli ya koo la juu kulegea zaidi na kuruhusu tindikali inayozalishwa tumboni kurudi kwenye koromeo la chakula na kusababisha maumivu makali kifuani.
Ukuaji wa mtoto tumboni/ Kuongezeka ukubwa tumbo la uzazi
Katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito kiungulia hutokea kwasababu ya ukubwa wa mfuko wa uzazi unaosababisha kubana utumbo mdogo na tumbo. Kadiri mtoto anavyoendelea kukua tumboni ndivyo mfuko wa uzazi unavyokua mkubwa na kusababisha kuongezeka kwa mkandamizo tumboni. Mbano huu hupeleka vilivyoko tumboni kusukumwa upande wa koromeo la chakula.
Baadhi ya mambo na hali zinazochangia kiungulia kutokea wakati wa ujauzito ni pamoja na:
- Kula chakula kingi na kunywa maji mengi wakati wa kula
- Ulaji wa vyakula vyenye mafuta, pilipili na viungo vingi
- Ulaji wa chakula kingi wakati mmoja
- Kula chakula masaa machache kabla ya kwenda kulala
- Kuvaa mavazi yakubana wakati wa ujauzito inaweza kuchangia kiungulia kutokea
- Matumizi ya kahawa au vinywaji vyenye kahawa
- Unywaji wa pombe wakati wa ujauzito
- Uvutaji sigara wakati wa ujauzito.
Ishara na Dalili za Kiungulia Wakati wa Ujauzito.
Kawaida dalili zinatokea baada ya kula au kunywa, vilevile unaweza kupata dalili hizi wakati wowote kipindi cha ujauzito lakini mara nyingi zinatokea sana wiki ya 27 ya ujauzito na kuendelea. Miongoni mwa dalili hizo ni pamoja na:
- Kujisikia kuungua, kuchoma au maumivu kifuani kutokana na tindikali za tumboni kurudi kwenye umio (esophagus)
- Tumbo kujaa gesi
- Uchachu mdomoni
- Kujisikia kuumwa
- Kubeua mara kwa mara
- Kukohoa mara kwa mara
- Kupata malengelenge kwenye mdomo
- Kujisikia kutapika.
Mambo Muhimu ya Kuzingatia Kufanya Nyumbani ili Kupunguza Kiungulia Wakati wa Ujauzito
- Kuwa makini na chakula unachokula. Hakikisha unaepuka vyakula vyenye tindikali na pilipili kama vile nyanya, vitunguu maji, vitunguu swaumu, kahawa, soda, chokoleti. Kaa mbali na vyakula vyenye mafuta mengi na viungo vingi, aina hii ya vyakula vinachelewesha umeng’enyaji wa chakula tumboni.
- Kula milo midogo midogo badala ya milo mikubwa mitatu ya kawaida. Hii inasaidia kuepuka tumbo kujaa sana
- Kaa wima kila unapokula, inasaidia chakula kutulia tumboni.
- Hakikisha usile mlo mkubwa (mfano:chakula cha usiku) masaa matatu kabla ya kwenda kulala. Unaweza kula mlo mwepesi ambao utalifanya tumbo lako kuwa tupu na kuepusha kiungulia.
- Usivute sigara na kunywa pombe wakati wa ujauzito. Kemikali zinazopatikana katika sigara na pombe zinasababisha kiwambo (valvu) kulegea, valvu hii inafanya chakula chote kilicho tumboni kutulia, lakini mara baada ya kulegea chakula ambacho hakijameng’enywa na tindikali inayopatikana tumboni zinapata uhuru wa kurudi kwenye koromro la chakula na kusababisha kiungulia.
- Vaa nguo zisizobana wakati wa ujauzito. Nguo za kubana huongeza mkandamizo tumboni hivyo kuwa rahisi kwa tindikali za tumboni kurudi kwenye koromeo la chakula (oesophagus).
- Unapoenda kulala hakikisha sehemu za juu za mwili zimeinuliwa juu kidogo kwa kuweka mto.
- Kunywa maji dakika 30 baada ya kumaliza kula siyo katikati ya mlo.
- Ongea na daktari au mkunga wako juu ya dawa sahihi kwaajili ya kiungulia. Hali ikiwa mbaya hakikisha unaenda hospitali, kulingana na hali yako ya ujauzito daktari atapendekeza dawa sahihi za kutumia. Usitumie dawa bila kupata ushauri wa daktari maana zinaweza kukudhuru wewe na mtoto tumboni.
- Unapohisi kiungulia kunywa glasi ya maziwa au kunywa maji moto yaliyowekwa kijiko kimoja cha asali.
- Mjamzito alale kwa ubavu wa kushoto, tafiti zinaonyesha kulala kwa ubavu wa kulia kunasababisha kiungulia kwasababu ni rahisi tindikali za tumboni kurudi kooni.
- Kula papai au nanasi mara kwa mara kwa sababu matunda haya yana enzaimu (kemikali maalum) zinazosaidia tumbo kumeng’enya chakula.
IMEPITIWA: NOVEMBA, 2021.