Jifunze Namna ya Kumuogesha Mtoto Mchanga

Muda wa kuoga unaweza kuwa wa furaha sana kwa mtoto wako. Inaweza ikawa ni tukio la kufurahisha hata kwenu wazazi. Lakini pia kumuogesha mtoto inaweza ikawa ni tukio gumu pale ambapo usalama wa mtoto wako ni wa kuzingatiwa. Jifunze namna ya kumuogesha mtoto wako kwa usalama zaidi na wakati huo huo kiwe kitendo cha kufurahia kwako na mtoto wako.

Unapomuogesha mtoto wako kwa mara ya kwanza hakikisha mwenza wako yupo. Kama mwenza hayupo ni vyema kuwe na mtu wa pili wa kukusaidia.

Weka maji ya vuguvugu kwenye beseni au sehemu utakayomuogeshea mtoto wako. Kabla hujamuweka mtoto wako kwenye beseni hakikisha tena joto la maji likoje kwa kutumia mkono wako. Wakati ukiendelea kumuogesha pia uwe makini na maji yanavyoendelea kuwa ya baridi, ukiona mikoni yako imeanza kuyasikia ni ya baridi basi yatakuwa ni ya baridi zaidi kwa mtoto wako, hivyo ni vyema kumaliza kumuogesha haraka zaidi.

Weka kila kitu utakachohitaji karibu yako, sabuni, kitambaa cha kuoshea, taulo, nepi na nguo za kubadilisha kabla hata hujaanza kumuogesha. Hii itakusaidia mkono mmoja uwe umemshikilia mtoto wako muda wote na mkono mwingine ukifanya kazi. Ukishamaliza kumuogesha mfunike haraka kwa taulo ili asipoteze joto lingi. Mkaushe vizuri, ukihakikisha unafuta majimaji yote kwenye sehemu zenye mikunjo kabla ya kumvalisha nepi na nguo.

Watoto wengine huhisi kama maji yanawasisimua, hivyo ni vyema kumuogesha mapema asubuhi. Wengine husinzia wakati wa kuogeshwa, hivyo kumuogesha wakati wa jioni inapendeza zaidi. Mtoto wako hahitaji kuogeshwa kila siku, mara mbili hadi tatu kwa wiki inatosha ilimradi tu kila siku unaosha uso wake, shingo, mikono na eneo linaloguswa na nepi.

Mara tu baada ya kuoga watoto hupenda kula. Unaweza ukamfunika mtoto wako kwa taulo kavu baada ya kumkausha na kumnyonyesha mkiwa mmegusana ngozi kwa ngozi.

Hakikisha umeyamwaga maji uliyotumia kumuogeshea mtoto, kwani ajali ikitokea na mtoto wako akaanguka kwenye maji hayo ukiwa haupo anaweza akazama hata kwenye maji yenye kina kidogo tu cha inchi 1.

.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.