Kama mama mpya utaanza kugundua ishara na milio ya mwanao inayomaanisha anataka kunyonya, kubembelezwa, kubadilishwa nepi au hitaji lingine. Kwa wakati huu kulia ni njia kuu ya mawasiliano ya mwanao (njia ya kufikisha ujumbe). Angalia ishara hizi ili upate kugundua kama mtoto wako atakuwa na njaa hivi karibuni:
- Mtoto akiweka mikono mdomoni,kufanya kama anayonya,kutoa ulimi nje,akilamba mdomo,kutoa udenda.
- Mtoto akijisogeza na kugeukia upande wa mtu aliyembeba.
- Mtoto akitoa milio na miguno ya kitoto, akijinyoosha, kuamka usingizini.
- Kulia ni ishara ya mwisho- mtoto akifikia hatua hii ya kulia inaweza kuwa ngumu kumnyonyesha mtoto wako. Kugundua ishara za awali za mtoto wako akiwa na njaa itasaidia kumfanya mtoto ashibe na maziwa mengi kutoka.
Kunyonyesha usiku
Unaweza kugundua mwanao kunyonya zaidi usiku, mara nyingi kila saa kuanzia saa kumi na mbili jioni mpaka saa tano usiku. Mchana na jioni maziwa yanakua na fati nyingi zaidi kuliko asubuhi, hivyo mtoto atahitaji aidi maziwa yenye fati nyingi kumsaidia kukua zaidi kwaajili ya siku inayofuata. Mara nyingi baada ya muda huu wa kunyonya usiku mtoto atalala vizuri masaa 3-4. Mara mtoto wako atakapofikisha mwezi mmoja akiwa na uzito mzuri sio lazima kumuamsha katikati ya usiku.