Hatua za Uchungu Wakati wa Kujifungua

Hatua ya kwanza ya uchungu ni ile ambayo wanawake wengi wanasema “kuwa kwenye uchungu”. Katika hatua hii mlango wako wa uzazi hutanuka na kupungua unene. Hatua hii ya uchungu ndio yenye maumivu makali kwani kubana kwa misuli “contractions” huongezeka na kuwa karibu zaidi mpaka mlango wa uzazi utakapokuwa umefunguka vizuri. Katika hatua hii utakuwa unatumia mbinu zote za kupambana na uchungu ulizojifunza ukisaidiwa na mkunga au mwenza wako.

Kama utachagua kutumia dawa mbalimbali za kupunguza maumivu, utapatiwa dawa hizi katika hatua hii ya kwanza ya uchungu. Dawa zingine haziwezi kutolewa ukiwa umekaribia kabisa kujifungua. Pale upana wa mlango wako wa uzazi utakapofikia sentimeta 10, utakuwa tayari kuanza kusukuma.

Hatua ya pili ya uchungu ni pale utakapokuwa unamsukuma mtoto wako apite katika njia ya kujifungulia na kuja duniani. Utasikia aina tofauti ya kubana kwa misuli katika hatua hii, itakuwa ni aina fulani ya kubana inayokufanya utamani kusukuma. Katika hatua hii kubana na kuachia kwa misuli yako kutakuwa ni kati ya dakika 2 hadi 4 kutoka mbano mmoja kwenda mbano mwingine na huchukua hadi sekunde 90 kwa mbano mmoja. Urefu wa hatua hii unaweza kuwa mfupi sana au ukachukua hadi lisaa limoja. Ila haitakiwi hatua hii ichukue zaidi ya masaa mawili.

Hatua ya tatu ya uchungu, utajifungua kondo la nyuma (placenta). Wakati mwingine utachomwa sindano ila kuweza kuharakisha hatua hii. Hatua hii haina maumivu ila utashauriwa kusukuma kidogo kusaidia kutoka kwa kondo hili.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.