Kwanini mtoto wako ana hasira za kuhamaki?
Watoto wenye umri wa mwaka mmoja mpaka miaka mitatu wanakabiliwa na hali hii. Ni hali ya kihisia inayofananishwa na kimbunga wakati wa kiangazi. Dakika moja mwanao anafurahia biskuti yake na dakika mbili baadae analia, analalamika na kupiga kelele kwa sauti ya juu kwasababu biskuti yake imevunjika mara mbili.
Kuwa mvumilivu, mara nyingi watoto wanaokabiliana na hali hii wanakua wamekatishwa tamaa na kitu. Mtoto wako katika umri huu anasikia kila anachoambiwa lakini anakasirika pale anaposhindwa kujielezea anavyojisikia au anachotaka na kwasababu hii anavunjika moyo zaidi.
Jinsi ya kukabiliana na ghadhabu ya mwanao:
1. Usipoteze Uelekeo
Ghadhabu ya mwanao sio muonekano mzuri. Pamoja na kupiga mateke, kupiga kelele au kujiburuza sakafuni, ghadhabu ya mwanao inahusisha kutupa vitu, kujipiga na wakati mwingine kujiumiza kwa kubana pumzi yake. Mwanao akiwa katika hali hii ni vigumu kukusikiliza japo atakujibu kwa kupiga kelele na kukutishia.
Kaa na mwanao wakati wa matukio kama haya inaweza kumsaidia, kushuhudia ghadhabu ya mwanao inaweza kukushtua, lakini anaweza kujisikia salama akikuona uko karibu nae. Wataalamu wanashauri kumbeba mtoto na kumshika kama inawezekana. Wengine wanashauri kumpuuzia mwanao mpaka hasira zitakapoisha kuliko kutetea tabia hiyo mbaya. Kwa kujaribu na kukosea utajua mbinu gani ni sahihi kwa mwanao.
2. Kumbuka wewe ni mtu mzima
Usiwe na wasiwasi watu wengine wanafikiria nini- mtu yeyote ambaye ni mzazi alishapitia hili. Kubaliana na hali halisi. Mwanao atakuwa na wasiwasi kwa alichokitenda. Kitu ambacho hatafurahia kuona ni wewe umekasirishwa zaidi na jambo hili. Ikiwa hasira za mwanao zimefika hatua ya kupiga wenzake na wanyama(paka au mbwa kama unafuga), mtoe kwenye eneo la tukio mpeleke chumbani kwake, mwambie kwanini umempeleka chumbani kwake, na mjuze kwamba utakaa nae mpaka atakapoacha kuhamaki. Ukiwa sehemu yenye umati wa watu wengi kuwa tayari kuondoka na mwanao mpaka atakapoacha kuhamaki.
3. Ongea nae baadae
Anapomaliza kuhamaki, mshike mwanao na ongea nae kuhusu kilichotokea. Kuwa tayari kumuelezea unafahamu kwanini amefanya hivyo na utamsaidia kujifunza kuelezea anavyojisikia wakati mwingine.
4. Jaribu kuepuka hali ya kuleta hamaki
Jaribu kulifanyia kazi tatizo linalosababisha mwanao kuhamaki kabla halijatokea. Kwa mfano kama mwanao anahamaki akiwa na njaa, beba vitafunio na vyakula vyake zaidi kwenye begi wakati unatoka, bila kusahau maji ya kunywa.
Jiangalie mara ngapi unasema HAPANA kwa maombi yake, inaweza kuwa sababu nyingine ya mwanao kuhamaki, jaribu kumruhusu baadhi ya mambo ili kumsaidia mwanao na wewe .