Begi la Hospitali Unapokwenda Kujifungua

Nini cha kufungasha kwenye begi la hospitali?

Sasa ni wakati wa kukusanya vitu muhimu utakavyohitaji wakati wa uchungu na kujifungua na baada ya mtoto kuzaliwa, hivyo andaa begi lako wakati unakaribia wiki ya 36 ya ujauzito. Hospitali zinaweza kutofautiana kanuni na sheria za kipi unapaswa kubeba na kipi hakiruhusiwi,wasiliana na mkunga wako kufahamu mambo muhimu ya kuongeza kwenye orodha ya mahitaji ya begi la hospitali.

Ni nini nifungashe kwaajili ya uchungu?

Mpango wa kujifungua na kumbukumbu za uzazi ulizoandika pembeni. Mfuko wenye vifaa vya kujifungulia mama unaopatikana kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya serikalini nchini kwa bei ya shilingi 21000/=. Mfuko huo una:

  • Mipira ya mikono (surgical gloves 4 pairs)
  • Taulo ya kike ya uzazi (maternanity pad)
  • Pamba kubwa (cotton wool gm.500)
  • Nguo ya mtoto (cloth material for new born)
  • Vibana kitovu (2 umbilical cord clamp)
  • Mpira wa kuzuia uchafu
  • Nyembe za kupasulia(surgical blades0
  • Nyuzi za kushonea
  • Bomba la sindano
  • Dawa ya kuongeza uchungu (Misoprostol)

 

Pia ni vyema kufungasha vitu vifuatavyo: 

  • Gauni (dera) ambalo litakusaidia wakati unaugulia uchungu ukiwa unazunguka korido za hospitali. Pia utahitaji lingine baada ya kujifungua, na vema likawa lepesi.
  • Kandambili au malapa rahisi kuvaa na kuvua.
  • Soksi, amini usiamini unaweza hisi baridi miguuni wakati wa uchungu.
  • Gauni lililochakaa kidogo(kuukuu) ya kuvaa wakati wa kujifungua. Haina haja ya kununua gauni jipya wakati wa kujifungua maana unaweza kuchafuka sana wakati uko chumba cha kujifungulia.
  • Mafuta laini(mafuta ya nazi au nyonyo) ya kupaka mwilini ikiwa utapendelea kukandwa wakati wa uchungu.
  • Mafuta maalum(lip balm) ya kupaka midomo, midomo yako inaweza kukauka haraka wakati uko chumba cha kujifungulia.
  • Vinywaji au vitafunio kwaajili yako wakati uko kwenye uchungu. Vinywaji vya kuongeza nguvu ni vizuri au unaweza kutumia glukosi kukusaidia kuendelea.
  • Vitu kama jarida, kitabu au kompyuta ndogo vya kukusaidia kujiburudisha au kukusaidia muda kwenda.
  • Kama una nywele ndefu, vibanio maalumu vya kubana nywele ni muhimu.
  • Mito,ikiwa hospitali inaruhusu, ni vyema kubeba mito ya ziada kutoka nyumbani itakayokusiadia kusikia nafuu.
  • Kama muziki ni moja ya kiburudisho chako ni vyema kubeba simu yenye chaji ya kutosha au “MP3 player”.

 

Mwenza wangu wakati wa kujifungua afungashe nini?

  • Kimiminika cha kupunguza joto (water spray) au feni ya mkononi ya kupunguza joto wakati ukiwa kwenye chumba cha kujifungulia.
  • Viatu salama na vyepesi vya kuvaa wakati mnazunguka kwenye korido.
  • Nguo za kubadilisha.
  • Mirija ya kusaidia kukunywesha maji au kinywaji chochote wakati wa uchungu.
  • Simu na chaja. Simu yenye “stopwatch” au “timer” inaweza kusaidia kujua baada ya muda gani mibano ya misuli ya uterasi (contractions) itaatokea. Mibano ya misuli ya uterasi (contractions) hutokea kwa muda na kurudia tena baada ya muda wakati wa kujifungua. Au kama simu ni ya kupapasa kuna “app” maalumu za kuweza kufanya kazi hii.
  • Kamera ya kidigitali au kamera ya simu, kwaajili ya kuchukua picha au video fupi kama utapendelea wakati wa kujifungua au mda mchache baada ya mtoto kuzaliwa.
  • Vitafunwa na vinywaji. Hutapendezwa msaidizi wako wa kujifungua akiwa na njaa au kiu mbele yako. Akifungasha kinywaji na kitu cha kula ataweza kukaa na wewe zidi kuliko kutoka na kutafuta chakula

Ni nini nifungashe kwaajili ya baada ya kujifungua?

  • Nguo ya kwenda nyumbani. Utahitaji nguo nyepesi na isiyobana kuvaa wakati ukiwa hospitalini na safari ya kwenda nyumbani. Itachukua mda tumbo lako kurudi kama awali, hivyo utahitaji kuvaa nguo za uzazi kwa muda.
  • Muongozo jinsi ya kuanza kunyonyesha,ambayo utaupata wakati wa kliniki za awali na mkunga wako.
  • Sidiria za kunyonyeshea, fungasha mbili au tatu.
  • Vitambaa malumu vya kukinga maziwa yasimwagike.
  • Pedi za uzazi au vitambaa maalumu ambavyo vinaweza kusaidia.
  • Gauni la kulala ambalo linafunguka mbele,litakusaidia siku za kwanza wakati wa kunyonyesha.
  • Mahitaji ya kuoga na usafi wa mwili kama sabuni, mafuta, mswaki na dawa ya mswaki, manukato mapole ya makwapani(deodorant).
  • Taulo na chanuo.
  • Chupi za zamani au chupi za kutupwa baada ya kutumika. Chupi mpya na nzuri zinaweza kuchafuka sana wakati wa kujifungua. Chupi kubwa za pamba ni nzuri hasa kama utafanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua, hazitasugua na kutonesha kidonda.

Nifungashe nini kwaajili ya mtoto?

  • Nguo tatu au nne za kulala na vesti.
  • Blanketi la mtoto, jaokua hospitali inaweza kuwa na joto, mtoto wako atahitaji blanketi kama kutakua na baridi wakati wa kuondoka.
  • Vitambaa vya kumfuta mtoto akicheuwa.
  • Jozi moja ya soksi.
  • Nguo moja kwaajili ya kusafiria kurudi nyumbani.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.