Tatizo la Kukosa Choo Kipindi cha Ujauzito

Tumbo kujaa gesi, kuvimbiwa, hali ya kujisikia umebanwa na haja kubwa ni malalamiko ya kawaida kipindi cha ujauzito.

Tatizo la kukosa choo ni hali isiyopendeza, kwa bahati mbaya ni hali ya kawaida sana wakati wa ujauzito- baadhi ya ripoti zinasema karibia asilimia 40 ya wanawake wanapitia hali hii. Kadiri tumbo linavyozidi kukua ndivyo mkandamizo wa mfuko wa mimba unavyoongezeka katika eneo la haja kubwa na kuzidisha tatizo hili.

Lini tatizo la kukosa choo linaanza wakati wa ujauzito?

Tatizo la kukosa choo linaanza mapema kadiri viwango vya projesteroni vinavyoongezeka, karibu na mwezi wa pili hadi wa tatu wa ujauzito. Inaweza kuwa mbaya zaidi wakati ujauzito unavyoendelea na uterasi yako inavyokua.

Ni moja ya matatizo ambayo yamekuwa yakiwasumbua wajawazito wengi hasa katika miezi ya awali ya ujauzito na miezi ya mwisho ya ujauzito.

Nini chanzo cha tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito?

Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito, nazo ni pamoja na:

Viwango vya homoni ya projesteroni: homoni hii huzalishwa kwa wingi wakati wa ujauzito,homoni hii hujulikana kulegeza misuli ya tumbo la chakula hivyo kusababisha chakula kupita taratibu katika utumbo. Mabaki ya chakula hukaa kwa muda mrefu tumboni bila ya kutolewa nje kama taka,kadiri mabaki hayo yanavyo zidi kubaki tumboni ndivyo maji yaliyo katika mabaki hayo huendelea kufyonzwa na utumbo hivyo kusababisha kukosa choo kwa muda na vilevile kupata choo kigumu.

Matumizi ya vidonge vya kuongeza madini ya chuma mwilini: ijapokuwa madini ya chuma ni muhimu wakati wa ujauzito kwa ukuaji wa mtoto, kukosa choo kwa mjamzito inaweza kuwa athari ya kutumia sana vidonge hivi. Ni vema kuongea na mkunga wako kuhusu jambo hili, anaweza kukushauri kubadilisha vidonge hivi, dozi yake au mara ngapi uvitumie. Hakikisha unafuata maelekezo kwasababu ukosefu wa damu ya kutosha (anemia) hutokea sana wakati wa ujauzito na inaweza kusababisha matatizo ya kiafya kwa mama na mtoto.

Ukosefu wa maji ya kutosha mwilini: wakati wa ujauzito mama anakabiliwa na tatizo la upungufu wa maji mwilini, kwasababu mwili unatumia maji zaidi kusaidia kutengeneza plasenta na “amniotic sac” (kifuko cha amnion-mfuko wa maji yanayomlinda mtoto na hupasuka kabla mtoto hajazaliwa. Ikiwa utakuwa na upungufu wa maji mwilini, mwili wako utashindwa kufanya kazi muhimu na kupelekea kupata shida kubwa sana za kiafya.

Msongo wa mawazo: ujauzito unaweza kuleta msongo wwa mawazo hasa unapokaribia siku ya kujifungua. Epuka kuwa na wasiwasi sana, hali hii inaweza kuathiri mfumo wa umeng’enyaji wa chakula na utoaji taka (kukosa choo).

Ukuaji wa tumbo la uzazi: kuongezeka kwa ukubwa wa tumbo la uzazi hutokea zaidi katika miezi ya mwisho ya ujauzito,ukubwa wa tumbo la uzazi kutokana na kuongezeka kwa ukubwa wa mtoto tumboni husababisha mkandamizo mkubwa kwenye tumbo la chakula,hivyo kupunguza kasi ya usafirishwaji wa mabaki ya chakula nje ya tumbo,hivyo kusababisha mwili kufyonza maji katika mabaki hayo na kuleta choo kigumu.

Mwili kutofanyishwa kazi na mazoezi: kadiri tumbo linavyozidi kuwa kubwa, inakuwa ngumu kwa mama kuwa imara katika ufanyaji kazi na mazoezi. Ufanyaji wa mazoezi huchochea misuli ya tumbo kufanya kazi yake ya kutoa taka nje ya mwili, mjamzito anavyo kuwa hafanyi mazoezi misuli ya tumbo nayo hushindwa kufanya kazi yake vizuri na kusababisha mama kukosa choo.

Wakati mwingine kukosa choo kunasababishwa na ulaji wa bidhaa za maziwa sana (dairy products), dawa mpya unayotumia au ulaji mdogo wa vyakula vyenye nyuzi nyuzi (fibre) kama matunda na mboga mboga za majani. Fiber hupatikana katika vyakula vya mimea: mboga, matunda, mboga, nafaka, karanga.

Baadhi ya vyakula unavyotakiwa kuacha ikiwa unasumbuliwa na tatizo la kukosa choo ni pamoja na ndizi, vyakula vya kukaangwa, viazi vya kukaanga, nyama nyekundu, mkate mweupe, wali mweupe, pasta na vyakula vya maziwa kama jibini.

Je, nini unapaswa kufanya ukipata tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito?

Hakuna haja ya kuteseka miezi yote tisa kwa tatizo hili. Zipo mbinu nyingi zitakazo kusaidia kupambana na tatizo la kukosa choo, nazo ni pamoja na:

  • Kula vyakula vyenye nyuzi nyuzi kwa wingi, vyakula hivi vinasaidia kutoa mabaki ya chakula kwenye utumbo kwa urahisi zaidi. Hakikisha unakula nafaka zisizokobolewa, vyakula jamii ya kunde, matunda safi na mboga za kijani za majani (mboga mbichi au iliyopikwa kidogo).
  • Kunywa maji ya kutosha. Maji mengi yatakusaidia kutoa mabaki ya chakula nje ya mwili kwa haraka zaidi. Hakikisha unakunywa angalau glasi 8 za maji kwa siku. Maji yanaweza kusaidia tatizo la kukosa choo lililosababishwa na matumizi ya vidonge vya madini chuma. Ikiwa unaishi eneo lenye hali ya hewa ya joto, kunywa zaidi maji (zaidi ya glasi 8)
  • Fanya mazoezi. Kutembea, kuogelea na yoga ni mazoezi mazuri kwa mwili wa mwanamke mwenye ujauzito. Mwili unapofanyishwa mazoezi unasaidia utembeaji wa mabaki ya chakula kuelekea nje ya mwili.
  • Oga kwa maji ya moto. Maji ya moto yanasaidia kupumzisha misuli na kuhamasisha taka kutoka nje ya mwili. Kama una bafu la kulala (bathtub) jiloweke kwa lisaa moja au zaidi.
  • Kunywa maji yenye limao. Chukua juisi ya limao nusu, changanya kwenye glasi ya maji, kisha kunywa kabla ya kwenda kulala. Maji yatasaidia kulainisha kinyesi, limao lina kiwango kikubwa cha asidi kitakachosaidia kusafirisha kinyesi.
  • Kula vyakula vyenye magnesiamu ya kutosha. Magnesiamu yanasaidia kuelekeza maji kwenye utumbo na kusaidia kinyesi kulainika na kusafirishwa nje kwa urahisi. Hakikisha unapata miligramu 350 kwa siku kwa kula vyakula kama samaki, spinachi, karanga na chokoleti nyeusi.
  • Epuka nafaka zilizokobolewa kila unapoweza, nafaka hizi zinachangia kukosa choo. Kwa mfano badala ya kula mkate mweupe, kula mkate wa kahawia (broen bread).
  • Jaribu kula milo sita midogo midogo kwa siku badala ya milo mitatu mikubwa, kwa kufanya hivi unaweza kuepuka kuvimbiwa na tumbo kujaa gesi.
  • Jisaidie haja kubwa kila unapoisikia, kubana haja kubwa mara kwa mara kunafanya misuli ya kuzuia utokaji wa kinyesi kuwa hafifu na kusababisha tatizo la kukosa choo.
  • Zingatia virutubisho na dawa zako. Jambo la kushangaza ni kwamba, virutubisho na dawa nyingi ambazo hufanya mwili wa mjamzito kuwa na afya kwa mfano; vitamini za kutumia kabla ya kuzaa, virutubisho vya kalsiamu na chuma zinaweza kuzidisha tatizo la kukosa choo. Kwa hivyo jadiliana na daktari wako kuhusu njia mbadala au marekebisho ya dozi za virutubisho hivi hadi hali itakapoboreka. Muulize pia daktari wako juu ya kutumia zaidi virutubisho vyenye madini ya magnesiamu kusaidia kupambana na tatizo la kukosa choo.
  • Ongea na daktari wako. Pale ambapo mbinu hizi za nyumbani hazifanyi kazi vizuri, mshirikishe daktari wako anaweza kukusahauri dawa au mbinu nyingine za kidaktari.

Je, naweza kuzuia kupata tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito?

Tabia ya kula kiafya na mazoezi ya kawaida huhimiza mfumo wa haraka wa kumeng’enya chakula, ambao unaweza kusaidia kuzuia tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito.

Kutumia vyakula vingi vyenye nyuzi nyuzi (kama; matunda, mboga, nafaka nzima, dengu), kunywa maji ya kutosha na kuupa mwili mazoezi vyote kwa pamoja vinazuia tatizo la kukosa choo.

Lini nitarajie tatizo la choo kuisha nikiwa mjamzito?

Kwa wanawake wengine, tatizo la kukosa choo hudumu katika kipindi chote cha ujauzito kadri viwango vya projesteroni vinapopanda. Walakini, ukibadilisha tabia yako ya kula na kuwa na tabia ya kufanya mazoezi kila mara, mambo huanza kusonga vizuri. Na unaweza kuchukua hatua za kupambana na tatizo hili la kukosa choo wakati wowote wa ujauzito.

Kumbuka

Utafurahi kujua kwamba vitamini unazotumia kabla ya kujifungua pia zinaweza kusaidia tatizo la kukosa choo, haswa asidi ya folic. Manufaa ya “vitamini B complex” na “vitamini B5” sio tu kutatua tatizo la kukosa choo wakati wa ujauzito, bali inasaidia kupunguza maumivu ya miguu wakati wa ujauzito. Unaweza kuipata kutoka kwa viini vya mayai, nafaka nzima, parachichi, viazi vitamu, mbegu za alizeti, broccoli.

IMEPITIWA: JUNI,2021.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.