Maumivu ya Tumbo na Kukakamaa kwa Fumbatio Wakati wa Ujauzito

Ujauzito unakuja na baadhi ya hali ambazo zinaweza kumkosesha utulivu mama mjamzito kama vile matiti kuongezeka ukubwa au maumivu ya mgongo na kiuno.  Maumivu ya tumbo na kukakamaa kwa fumbatio (abdominal cramping) kunaweza kukufanya upate wasiwasi haswa kama wewe ni mjamzito.

Baadhi ya maumivu haya wakati wa ujauzito ni kawaida, lakini wakati mwingine yanaweza ashiria tatizo linalohitaji matibabu haraka iwezekanavyo. Maumivu haya yanaweza kutokea wakati wowote katika ujauzito. Kupitia makala hii utaweza kufahamu kama maumivu ya tumbo na kukakamaa kwa fumbatio wakati wa ujauzito ni kawaida au ni ishara unahitaji matibabu na ushauri wa daktari haraka.

Je, mikakamao hii wakati wa ujauzito ni kawaida?

Baadhi ya maumivu ya tumbo na kukakamaa kwa fumbatio wakati wa ujauzito ni kawaida na hayana madhara kipindi cha ujauzito. Maumivu yanayosababishwa na ukuaji wa uterasi,maumivu ya ligameti zinazoshikilia uterasi,kukosa choo au kuvimbiwa na mikazo ya leba ya uwongo (Braxton Hicks contractions).

Maumivu ya tumbo yanayosababishwa na ujauzito kutungwa nje ya uterasi,kutoka au kuharibika kwa mimba changa (miscarriage), uchungu wa kujifungua kabla ya wiki 37 za ujauzito (preterm labor),tatizo la kondo la nyuma kuachia kabla mtoto hajazaliwa (placenta abruption), kifafa cha mimba (preeclampsia), maambukizi katika njia ya mkojo (UTI) na ugonjwa wa kidole tumbo(appendicitis) wakati wa ujauzito ni hatari. Siku zote ni salama kuwasiliana na mtaalamu wa afya anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako ikiwa utapata dalili zinazokupa wasiwasi.

Chanzo cha maumivu ya tumbo na mikakamao ya fumbatio wakati wa ujauzito

Zifuatazo ni sababu za kawaida za maumivu na mikakamao ya fumbatio wakati wa ujauzito ambayo inaweza kutokea kipindi chochote cha miezi mitatu ya ujauzito:

Tumbo kujaa gesi

Gesi na kuvimbiwa ni malalamiko ya kawaida kipindi cha ujauzito yanasababishwa na ongezeko la viwango vya homoni ya projesteroni, homoni inayohusika na kutuliza misuli laini ndani ya njia ya mmeng’enyo.

Matokeo yake ni kuvimbiwa ikiambatana na kukosa choo kwasababu mmeng’enyo wa chakula unafanyika taratibu- hali zote hizi zinaweza kusababisha kuhisi fumbatio lako kukakama.

Tatizo lako la kiafya linahusishwa na mmeng’enyo wa chakula iwapo utakuwa unatoa hewa nje ya mwili kwa kujamba au baada ya kujisaidia haja kubwa unapata unafuu. Unaweza kuzuia kupata shida hizi zinazohusiana na mfumo wa umeng’enyaji wa chakula kwa kula vyakula vya nyuzinyuzi (fiber), kula milo midogo midogo badala ya kula milo mitatu mikubwa, chukua muda wako kutafuna vizuri na taratibu chakula. Ikiwa mabadiliko haya madogo hayatasaidia, wasiliana na daktari au mhudumu wa afya anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako kila miadi kwa ushauri na matibabu zaidi.

Mikakamao ya fumbatio inayotokea baada ya kufika kileleni(orgasm) wakati wa tendo la ndoa

Wakati mwingine mikakamao hii inafuatwa na maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo, ambayo ni kawaida na una hatari ndo kwa ujauzito ulio salama. Sababu ya maumivu haya baada na wakati mama anapofika kileleni ni ongezeko la mtiririko wa damu kwenye nyonga na mikazo ya kawaida ya uterasi inayotokea kila mama anapofika kileleni.

Usiwe na hofu ya mtoto wako kuumia kila unapofika kileleni, yuko salama. Jaribu kufurahia tendo hili ikiwa daktari au mtoa huduma wako atakuruhusu kufanya tendo la ndoa wakati wa ujauzito. Kutuliza mikakamao na maumivu haya, jaribu kujilaza kitandani au kulala kidogo baada ya tendo.

Mtiririko wa damu kwenye uterasi

Wakati wa ujauzito, mwili wako unatuma damu nyingi zaidi ya kawaida kwenye uterasi. Hii inapelekea kuhisi mgandamizo eneo hilo. Jilaze kitandani upate kupumzika au oga kwa maji ya moto inaweza kusaidia kutuliza maumivu haya.

Maambukizi katika njia ya mkojo (UTI)

UTI inaweza isiwe na dalili, lakini mara nyingi inasababisha maumivu au mgandamizo eneo la nyonga. Dalili nyingine ni kama harufu mbaya, rangi tofauti au damu kwenye mkojo, maumivu na kuungua wakati wa kukojoa, homa au kutaka kukojoa kila mara. UTI ni hatari isipo tibiwa vizuri na mapema. Bahati nzuri matumizi mazuri mpaka mwisho ya antibiotiki yanatibu maambukizi haya.

Ukosefu wa maji mwilini

Ukosefu wa maji ya kutosha mwili unaweza kusababisha leba ya uwongo au mikazo ya uterasi katikati ya ujauzito ambayo ni kawaida. Kunywa maji ya kutosha kila unaposikia kiu, baadhi ya tafiti zinaonyesha ukosefu wa maji uliokithiri unaweza ongeza hatari za kupata uchungu na kujifungua kabla ya muda.

Lenga kunywa angalau glasi 8 mpaka 10 za maji kwa siku. Mkojo kuwa na rangi ya njano iliyopauka ni moja ya ishara una maji ya kutosha mwilini.

Maumivu tumbo na mikakamao kwenye fumbatio miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito

Upandikizaji

Mapema baada ya kujua una ujauzito, unaweza kupatwa maumivu ya tumbo la uzazi kama yale ya siku za hedhi. Maumivu haya hutokea siku ambayo hedhi yako ilitarajiwa kutokea, kabla hata hujapata uhakika umepata ujauzito.

Vichomi vya mbali na kuona damu kidogo kwenye nguo zako za ndani ni matokeo ya yai lililorutubishwa kujipandikiza kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi (uterasi), hali hii inatokea siku ya 6 mpaka 12 baada ya urutubishaji wa yai na inadumu kwa siku moja.

Mimba kutungwa nje ya mfuko wa uzazi (Ectopic pregnancy)

Wakati yai lililorutubishwa linajipandikiza sehemu tofauti, mara nyingi katika mirija ya falopia-inaweza kusababisha maumivu na mikakamao sehemu ya chini ya fumbatio.

Maumivu haya yanaweza anza taratibu na kuongezeka kadiri muda unavyoenda. Mara nyingi ujauzito wa aina hii unasababisha maumivu ya mabega, kutoka damu ukeni,kizunguzungu na kuzimia.

Ikiwa unahisi una dalili za ujauzito huu, tafadhali onana na daktari mapema. Uchunguzi wa aina hii ya ujauzito unafanywa kwa kipimo cha ultrasound na vipimo vya damu wiki ya 5 mpaka 6 ya ujauzito.

Kutoka au kuharibika kwa mimba changa (miscarriage)

Kukakamaa kwa fumbatio na maumivu ya tumbo miezi ya kwanza ya ujauzito inahusishwa na mimba kutoka au kuharibika, maumivu haya yanaweza fananishwa na yale ya kipindi cha hedhi. Mara nyingi hutokea kwenye fumbatio, sehemu ya chini ya mgongo na eneo la nyonga, huambatana na kutoka damu ukeni.

Inaweza kuwa ngumu kugundua kama maumivu unayoyapata mwanzoni wa ujauzito ni dalili ya mimba kutoka, upandikizwaji wa yai lililorutubishwa au kupanuka kwa uterasi. Njia pekee itakayokusiaidia ni kuangalia kwa makini damu inayotoka ukeni. Mimba kutoka au kuharibika inaambatana na utokwaji wa damu ukeni kwa siku kadhaa na mara nyingi inaongezeka uzito kadiri siku zinavyoongezeka ukilinganisha na upandikizwaji wa yai. Ikiwa una wasiwasi wasiliana na mtoa huduma za afya, ikiwezekana tembelea kituo cha afya kilicho karibu na wewe.

Maumivu tumbo na mikakamao kwenye fumbatio miezi mitatu ya pili ya ujauzito

Maumivu ya ligamenti zinazoshikilia uterasi

Ujauzito unavyoendelea kukua, ligamenti hizi huvutika na kusababisha maumivu ya ghafla ambayo hutokea upande mmoja au pande zote za eneo la chini la fumbatio.

Mara nyingi maumivu haya huanza kipindi cha pili cha miezi mitatu ya ujauzito, hutokea wakati wa mazoezi, baada ya kuamka kitandani, ukipiga chafya, ukikohoa/ukicheka au ukiasogea ghafla. Maumivu haya hukoma baada ya dakika chache. Kusugua kwa taratibu au kuweka kitambaa chenye joto kwenye fumbatio kunaweza kusaidia. Jaribu pia kupumzika na kugeuka taratibu kila unapobadili mkao wako.

Leba ya uwongo (Braxton Hicks contractions)

Zinaweza kutokea kuanzia wiki ya 20 ya ujazuito, ni njia za mwili wako kukutaarifu ujio wa siku ya kweli ya kujifungua. Mikazo hii hudumu kwa sekunde chache na haina mpangilio.

Kama utapatwa na mikakamao hii kipindi cha pili cha miezi mitatu ya ujauzito na kuendelea, jaribu kubadili mkao wako. Lala au kaa kitako kama ulikua umesimama mpaka maumivu yatakapotoweka.

Kumbuka: tatizo la kondo la nyuma kuachia kabla ya mtoto kuzaliwa (placenta abruption), kifafa cha mimba na mama kujifungua kabla ya wiki ya 37 vinaweza kutokea katika kipindi cha pili cha miezi mitatu ya ujauzito.

Maumivu tumbo na mikakamao kwenye fumbatio miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito

Tatizo la kondo la nyuma kuachia kabla mtoto kuzaliwa (placenta abruption)

Ikiwa kondo la nyuma litatengana (kidogo au lote) na ukuta wa uterasi kabla mtoto kuzaliwa, inaweza kusababisha maumivu makali na yanayo jirudiarudia, vilevile maumivu ya mgongo na kutokwa damu ukeni.

Tatizo hili linatokea sana miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, lakini pia linaweza tokea miezi mitatu ya pili ya ujauzito. Ikiwa unapatwa na mikakamao ya fumbatio inayoambatana na kutokwa damu ukeni, wasiliana na daktari au mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako haraka kupata huduma za kitabibu.

 Kifafa cha mimba

Mara nyingi hali hii hutokea kipindi cha mwisho cha ujauzito na inajulikana kupitia dalili kama shinikizo la ghafla la damu na uwepo wa protini katika mkojo.

Inaweza sababisha maumivu ya sehemu ya juu ya fumbatio yanayoambatana na kuumwa kichwa sana ambacho hakitulizwi kwa dawa, mikono na uso kuvimba sana, mabadiliko ya uwezo wa kuona, ongezeko la uzito ambao hauhusiani na ulaji wako, kichefuchefu au kutapika na kupumua kwa shida.

Ni muhimu kumuona daktari au mkunga wako ikiwa unapitia dalili zilizotajwa hapo awali. Kumbuka kifafa cha mimba ambacho hakitatibiwa vizuri ni hatari kwako na mtoto wako, kwasababu kinapunguza kiasi cha oksijeni na lishe inakwenda kwa kijusi tumboni. Pia inaongeza nafasi ya kupata tatizo la kondo la nyuma kuachia kabla mtoto kuzaliwa. Ikigundulika mapema na kutibiwa una uwezekano mzuri wa kuwa na ujauzi wenye afya.

Kubana na kuachia kwa misuli wakati wa kujifungua (Labor contractions)

Uchungu wa uzazi hutokana na kubana na kuachia (tena kwa kurudiarudia) kwa misuli katika tumbo la uzazi. Misuli hii inavyobana na kuachia taratibu husababisha kufunguka kwa mlango wa tumbo la uzazi. Kubana na kuachia kwa misuli hutokea taratibu na yenye mpangilio maalumu,idadi ya marudio ya mikazo ya uterasi ni mara 3-4 kila dakika 10 na kila mkazo huchukua sekunde 40-60

Mkazo au mbano wa tumbo la uzazi mwanzoni hauchukui muda mrefu. Huachia mama anapopumzika. Unapokaribia kujifungua hapo ndipo uchungu wa uzazi wa kweli huja kwa nguvu, haupungui hata ukibadili mkao wako. Dalili nyingine za kujifungua ni pamoja na mgandamizo eneo la nyonga (kama mtoto anasukuma kushuka chini) na mabadiliko ya uchafu unaotoka ukeni (damu nyepesi au uvujaji wa majimaji ya ukeni).

Katika miadi yako daktari au mkunga wako alikutaarifu kuwasiliana nae ikiwa utapatwa dalili za mikakamao ya fumbatio kipindi hiki cha mwisho cha ujauzito ikiwa utahisi ni uchungu wa uzazi. Ukipatwa na dalili kama kupasuka kwa chupa ya uzazi, kutokwa damu ukeni au kama una dalili zozote za ghafla za kifafa cha mimba ghafla wasiliana na daktari au mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako.

Ikiwa unapata dalili hizi kabla ya wiki ya 37 ina maanisha utajifungua kabla ya muda, wasiliana pia na mkunga wako hata kama hauna uhakika au tembelea hospitali unayotarajia kujifungulia mara moja.

Jinsi ya kupunguza maumivu ya ujauzito

Utulizaji wa maumivu ya tumbo na mikakamao kwenye fumbatio wakati wa ujauzito hutegemea sababu ya maumivu unayoyapata. Vidokezo hivi vinaweza kusaidia kutuliza sababu za kawaida zinazopelekea maumivu ya tumbo na mikakamao ya fumbatio wakati wa ujauzito:

  • Laza mwili wako na pumzika kwa muda, itasaidia kutuliza maumivu yanayohusiana na upandikizaji, kufika kilele wakati wa ujauzito, ongezeko la mtiririko wa damu kwenye uterasi na maumivu ya ligameti zinazoshikilia uterasi.
  • Kunywa maji ya kutosha, itasaidia kutuliza maumivu yanayohusiana na ukosefu wa maji ya kutosha mwilini, kukosa choo au kuvimbiwa.
  • Oga kwa maji ya moto kutuliza maumivu yanayohusiana na ongezeko la mtiririko wa damu kwenye uterasi.
  • Badilisha mkao kama unapatwa na mikazo ya leba ya uwongo
  • Tumia mikanda maalum kusaidia kupunguza maumivu ya tumbo wakati wa ujauzito yanayohuisana na ligameti zinazoshikilia uterasi.

Lini niwasiliane na daktari au mkunga wangu

Wakati gani inakupasa upate wasiwasi kuhusu maumivu na mikakamo kama wewe ni mjamzito?

Hakikisha unawasiliana na daktari au mkunga wako anayesimamia maendeleo ya ujauzito ikiwa utapatwa na dalili zifuatazo:

  • Maumivu makali ya sehemu ya chini ya fumbatio katikati au pande zote, maumivu ambayo hayapungui (hata kama hayaambatani na kutoka damu)
  • Ongezeko la ghafla la kiu, inayoambatana na kupungua kwa kukojoa au kutokojoa kabisa siku nzima.
  • Maumivu makali ya kichwa yasiyoisha, mabadiliko katika kuona, kuvimba au ongezeko la uzito usioelezeka
  • Homa au kutetemeka
  • Kutokwa damu nzito au kutoka damu kunakoambatana na maumivu au maumivu makali chini ya fumbatio.
  • Kuharisha damu
  • Maumivu au kuungua wakati wa kukojoa, au kukojoa kwa shida au damu kwenye mkojo
  • Kubanana kuachia misuli ya uterasi zaidi ya mara nne ndani ya saa moja (haswa kama inatokea kabla ya wiki ya 37 ya ujauzito).

UJUMBE

Kumbuka kuna nafasi nzuri kwamba maumivu ya tumbo wakati wa ujauzito ni kawaida kabisa. Lakini ni busara kujua sababu kubwa zaidi ya mibano ya fumbatio na maumivu ya tumbo wakati wa ujauzito ili uweze kupata huduma ya matibabu ambayo unaweza kuhitaji.

IMEPITIWA: APRIL,2021.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.