Vipimo Muhimu vya Kufanya Kabla ya Kupata Ujauzito

Sote tunajua umuhimu wa kufanya vipimo na matibabu husika ili kuhakikisha afya njema kwa mama mjamzito mtarajiwa na usalama wa mtoto wake anayekuja. Wataalamu wengi kwa sasa wanashauri wanawake waanze kumuona mkunga wao kabla hata ya kuanza kupata ujauzito.

Inawezekana ikashangaza kwa nini uanze kuwa na wasiwasi wa ujauzito kabla ya hata kuwa nao, ila daktari wako au mkunga anaweza kukufanyia vipimo na kuwa na uhakika wa kuwa wewe na mwenza wako hamna matatizo yaliyojificha yanayoweza kuleta madhara kwenye ujauzito au uwezo wenu wa kupata ujauzito. Daktari wako anaweza pia kukupa ushauri kuhusu mazoezi, lishe, mfumo wa maisha na virutubisho vya asidi ya foliki. Utafiti unaonyesha wanawake wanaomuona daktari au mkunga kabla ya kupata ujauzito wanaongeza uwezo wao wa kupata ujauzito na kupunguza matukio ya mimba kuharibika au mtoto kuzaliwa na matatizo.

Kinachotokea wakati wa uchunguzi

Wakati wa uchunguzi wa awali kabla ya ujauzito, daktari wako au mtoa huduma ya afya atafanya uchunguzi na vipimo mbalimbali kujua kama upo tayari kwa ujauzito. Baadhi ya uchunguzi utakaofanyika ni kama ifuatavyo:

1. Uzito

Kupima uzito ni muhimu ili kujua kama uzito wako ni sahihi kwa urefu wako na aina ya mwili wako. Kama sivyo, daktari wako atashauri mabadiliko mbalimbali kwenye lishe yako, mazoezi au madawa ili kuweza kurudisha uzito wako kuwa kawaida. Uwiano wa mwili na uzito (BMI) kati ya 18.5 na 22.9 ndio sahihi kwa wanawake.

2. Kipimo cha mkojo

Kipimo cha mkojo kugundua kama kuna maambukizi kwenye njia ya mkojo au figo ni mojawapo ya vipimo muhimu kabla ya kupata ujauzito.

3. Vipimo vya magonjwa mfumo wa uzazi wa wanawake

Vipimo hivi hufanywa kuchunguza uwepo wa uvimbe kwenye mfuko wa uzazi (uterine fibroids), uvimbe wenye maji (cysts) au uwepo wa maambukizi kwenye nyonga (PID). Pia kipimo hiki kinaangalia uwepo wa matatizo ya hedhi ikiwemo hedhi zisizo na utaratibu na pia uwepo wa matatizo yoyote yanayoweza kuleta shida kwenye ujauzito.

4. Uchunguzi wa matiti, nyonga na tumbo

Uchunguzi wa nyonga na njia ya uzazi yanaangalia uwepo wa fangasi au trichomona (trichomoniasis) ambayo yanaweza kuleta matatizo kwenye ujauzito. Tumbo linafanyiwa uchunguzi kuangalia kama kuna matatizo yoyote yanayoweza kuleta shida kwa uwezo wa ukuaji wa ujauzito. Matiti yanachunguzwa kama kuna uwepo wa uvimbe utakaohitaji ufuatiliaji wa karibu.

5. Kipimo cha Shinikizo la Damu (Blood Pressure)

Shinikizo la damu linapimwa ili kugundua uwepo wa shinikizo la juu au la chini kwani zote zinaweza kuleta matatizo kwenye ujauzito.

6. PAP Smear test (Kipimo cha ute wa mlango wa uzazi)

Uchunguzi wa ute wa mlango wa uzazi ni kipimo kimojawapo kitakachofanywa ukikutana na daktari kabla ya ujauzito. Kipimo hiki kinafanywa kwa daktari kuingiza kifaa maalumu kwenye uke (speculum) ili aweze kuona mlango wa mfuko wa uzazi (cervix). Daktari baada ya hapo hupanguza mfuko wa uzazi kwa kutumia pamba maalumu ili kupata ute ute uliopo kwenye mlango wa uzazi. Pamba hii na ute ute uliopatikana hutumwa maabara ili kuweza kufanyiwa uchunguzi. Kipimo hiki huchunguza kama umepata maambukizi ya magonjwa ya ngono kama kisonono, kaswende, HIV au Hepatiti B.

7. Vipimo vya damu

Vipimo vifuatavyo vya damu vinafanywa ili kugundua uwepo wa magonjwa mbali mbali:

  • Upungufu wa vitamini D
  • Wingi wa damu (Himoglobini)
  • Glucose (Kipimo cha sukari kwenye damu)
  • Aina ya damu (Rh factor)
  • Rubella
  • Varicella
  • Kifua kikuu (TB)
  • Hepatiti B
  • Toxoplasmosis
  • Thyroid
  • Maambukizi ya Ngono.

8. Magonjwa ya kurithi (Genetic conditions)

Zungumza na daktari wako kama kwenye familia yako kuna historia ya magonjwa ya Thalassemia, Cystic Fibrosis au Down`s Syndrome ili uweze kufanyiwa uchunguzi zaidi.

9. Matumizi ya uzazi wa mpango

Mtarifu daktari kuhusu njia ya uzazi wa mpango uliyokuwa unatumia. Njia nyingi za uzazi wa mpango haziathiri ni muda gani utachukua mpaka kupata ujauzito baada ya kuacha kuzitumia. Ijapokuwa, kama umekuwa ukitumia njia ya uzazi wa mpango ya sindano, inaweza kuchukua hadi mwaka mmoja kuweza kurudisha uwezo wako wa kupata ujauzito kuwa wa kawaida.

10. Mimba zilizopita

Inashauriwa kuzungumza na daktari wako kuhusu mimba zilizopita, zilizotoka na zile zilizotungwa nje ya mfuko wa uzazi. Ijapokuwa inaweza kuwa ni mazungumzo magumu kwako ila itamsaidia daktari wako kuweza kukupa msaada bora kuelekea kwenye ujauzito wako unaokuja.

Hitimisho

Pamoja na vipimo mbali mbali kama vilivyoelezwa hapo juu, tegemea pia daktari wako kuzungumza na wewe kuhusu lishe, afya yako kwa ujumla, mfumo wa maisha wa kufuata, utaratibu wa mazoezi wa kufuata na aina ya kazi yako na inavyoendana na ujauzito. Mueleze matatizo yoyote unayoyapata kuhusu mzunguko wako wa hedhi, pia matatizo yoyote ya kiafya uliyo nayo kama pumu, kisukari au shinikizo la juu la damu kwani yatamsaidia kukupa ushauri sahihi zaidi.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.