Miadi ya Kliniki ya Mtoto

 Baada ya kuzaliwa

Daktari wa watoto atampima mtoto ndani ya masaa 24 baada ya kuzaliwa, na atapima mwili mzima wa mtoto kuangalia kama mwili unafanya kazi ipasavyo. Baadhi ya vipimo utakavyoona mwanao akifanyiwa kwanza:

  • Daktari atampima mwanao urefu,uzito na mzunguko wa kichwa chake. Vipimo hivi vitaandikwa kwenye chati ya ukuaji.
  • Uwezo wake wa kusikia
  • Kipimo cha damu kuchunguza magonjwa ya kurithi, seli mundu na mengineyo.
  • Pia katika kipindi hichi mtoto atapewa chanjo ya kifua kikuu (sindano bega la kulia) na polio (matone ya mdomoni).

Mwezi wa 1

Katika miadi hii ya kwanza ya mtoto wako, mtaalamu wa watoto atafanya vipimo vya muhimu kama urefu,uzito na mzunguko wa kichwa chake, fuatilia ukuaji wa mtoto,atauliza maswali ili kufanya tathmini ya hali ya kisaikolojia/tabia ya mtoto ambayo utaifahamu kwa kuangalia matendo na mwitikio wa mtoto wako katika  mazingira mapya. Mwisho kabisa daktari atafanya vipimo vya mwili kuanzia kichwani mpaka kwenye vidole-masikio, macho, mdomo, ngozi, moyo na mapafu, tumbo, mapaja na sehemu zake za siri zitapimwa kuhakikisha zina afya.

Mwezi wa 2

Katika miadi hii ya mwezi wa pili, daktari atampima mtoto vipimo muhimu urefu, uzito, na mzunguko wa kichwa chake, pamoja na tabia na ukuaji wa mwili wake. Jambo la tofauti katika miadi hii ni mtoto atachomwa sindano nyingi za chanjo.

Mtoto atapewa chanjo ya ugonjwa wa kupooza(matone mdomoni),dondaakoo,kifaduro,pepopunda na hepatiti B(sindano paja la kushoto) chanjo ya nimonia(sindano paja la kulia) na kuhara(matone mdomoni).

Mwezi wa 3

Katika miadi hii, daktari atampima mtoto vipimo muhimu urefu,uzito,na mzunguko wa kichwa chake, pamoja na tabia na ukuaji wa mwili wake. Pamoja na chanjo za mara ya pili ya ugonjwa wa kupooza(matone mdomoni),dondaakoo,kifaduro,pepopunda na hepatiti B(sindano paja la kushoto) chanjo ya nimonia(sindano paja la kulia) na kuhara(matone mdomoni).

Mwezi wa 4

Mtoto anakua mkubwa! Ana miezi minne sasa na muda wa kliniki nyingine. Katika miadi hii ya nne tegemea vipimo vya kawaida kama kupima mwili wake urefu,uzito na mzunguko wa kichwa chake, fuatilia ukuaji wa mtoto,atauliza maswali ili kufanya tathmini ya hali ya kisaikolojia/tabia ya mtoto ambayo utaifahamu kwa kuangalia matendo na mwitikio wa mtoto wako katika  mazingira mapya. Mwisho kabisa daktari atafanya vipimo vya mwili kuanzia kichwani mpaka kwenye vidole-masikio, macho, mdomo, ngozi, moyo na mapafu,tumbo,mapaja na sehemu zake za siri zitapimwa kuhakikisha zinaafya.

Mtoto anaweza kufanyiwa kipimo cha haemoglobini kuangalia kama ana anemia na chanjo ya mwisho ya magonjwa ya  kupooza(matone mdomoni),dondaakoo,kifaduro,pepopunda na hepatiti B(sindano paja la kushoto) chanjo ya nimonia(sindano paja la kulia) na kuhara(matone mdomoni).

Mwezi wa 6

Mtoto kafika nusu mwaka tangu amezaliwa, miadi ya kliniki atafanyiwa vipimo vya kawaida

Miezi 9

Tegemea vipimo vya kawaida. Mtoto atapewa chanjo ya kwanza ya surua(sindano bega la kushoto)

Miezi 12

Mtoto ana umri wa mwaka mmoja, ikiwa mtoto hajapata shida yoyote ile, tegemea vipimo vya kawaida kwa mtoto wako. Kama mtoto hajapata chanjo ya surua ni wakati mzuri wa mwanao kupata.

Miezi 15

Kama kawaida mtoto atapimwa vitu muhimu, pamoja na chanjo ya pili ya surua.

Miezi 18

Miezi michache imebaki mwanao kufikisha miaka miwili. Kama mtoto wako hana tatizo lolote la kiafya, katika miadi hii atafanyiwa vipimo vya kawaida kama siku zote.

 Miezi 24

Hongera mwanao ana miaka 2 sasa! Mtoto atapitia vipimo muhimu kama kawaida na kipimo cha mwili kuangalia kama ogani zake zinafanya kazi vizuri. Kama ana tatizo la kiafya ni wakati mzuri wa kumpeleka kwa daktari maalumu wa tatizo husika.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.