Hatua za Ukuaji kwa Mtoto: Kutembea

Kujifunza kutembea ni moja ya mafanikio makubwa katika maisha ya mtoto, ni hatua kubwa katika maisha yake huru. Mara mtoto atakapoanza kutembea atakua mchunguzaji sana.

Lini mwanangu ataanza kutembea?

Katika mwaka wa kwanza wa mwanao, mwili wake na misuli yake inakuwa na nguvu zaidi. Atajifunza kukaa, kuviringika na kutambaa.

Mtoto wako ataweza kusogea kwa kujiinua. Kati ya miezi saba na mwaka mmoja ataweza kusimama kwa kushika vitu kwa mda mchache. Atapata shida kusimama mda mrefu,hivyo ataishia kudondoka na matako mara anapochoka.

Watoto wengi wanazunguka sana wakikaribia mwaka mmoja. Wanazunguka wakishika vitu kama samani na ukimshika mkono anaweza kutembea hatua chache. Watoto wengi wanaanza kutembea wenyewe wakifika miezi 12 na 17.

Jinsi gani mwanangu atajifunza kutembea?

Mchanga mpaka miezi miwili

Ukimbeba mwanao kwa kumsimamisha na kumshika kichwa chake, utahisi mwanao akijaribu kutumia miguu yake. Kwa sasa miguu yake haina nguvu ya kutosha kumsaidia kusimama.

Miezi mitano mpaka 10

Ifikapo miezi sita mtoto ataweza kuhimili uzito wake na kujiinua kwa kusimama. Ukimsimamisha kwenye mapaja yako ataanza kuruka juu na kutua,kuruka itakua shughuli yake anayoipenda katika umri huu. Ikiwa mwanao hajaweza kuhimili uzito wake kwenye miguu yake akifika miezi nane ongea na mshauri wako wa afya.

Mwanao anapoendelea kujifunza kujiviringisha, kukaa na kutambaa misuli yake inaendelea kunyooka.

Kati ya mwezi wa saba na miezi 12 mwanao atajitahidi kuinuka na kuanza kusimama akiwa anashika samani au mguu wako. Mwanao akianza kusimama vizuri ataanza kuzunguka kwa kushika vitu. Anaweza kuwa jasiri na kuachia na kusimama bila msaada. Mara baada ya mwanao kuwa tayari kuachia kushika samani ataanza kupiga hatua chache ukumshika mkono. Anaweza kuinama akitaka kuokota mdoli wake.

Mwaka mmoja

Mtoto wa mwaka mmoja anaanza kujaribu kukunja magoti na kujifunza kukaa chini baada ya kusimama. Hii ni hatua ngumu zaidi kuliko unavyofikiria.

Mwanao anaweza kuzunguka ndani ya nyumba, kusimama mwenyewe bila msaada na kupiga hatua chache. Lakini watoto wengine wanachukua muda mrefu zaidi kutembea. Kutembea ni jambo la kutatiza! Inahitaji usawa, uratibu na nguvu za misuli.

Mwanao atahitaji mazoezi mengi na atalega mwanzoni. Watoto wengi wanafanikiwa kutembea awali kwa kupanua miguu yao na vidole vyao kuelekezwa ndani au njee. Pia anaweza akaanguka sana.

Nawezaje kumsaidia mwanangu kutembea?

Unaweza kumsaidia mwanao kwa kumpa mazoezi mengi. Mtoto wako anahitaji kuweza kusimama, kutoka kwenye kukaa na kuzunguka kwa kutambaa kabla ya kuanza kutembea kwa ujasiri mwenyewe.

Unaweza kuhifadhi midoli yake mbali na yeye juu ya meza fupi, kwa kufanya hivi kutamsaidia kujivuta na kuifikia. Unaweza kufanya hivyo pia wakati akisimama ili kumpa motisha ya kusonga mbele na kuifuata.

Mwanao akianza kusimama anaweza kuhitaji msaada wa kushuka chini kukaa, hivyo basi mfundishe kukunja magoti ili aweze kukaa kwa urahisi zaidi.

Muhamasishe mwanao kutembea zaidi kwa kuchuchuma au kusimama mbele yake na kumshika mikono yake na kumsaidia kutembea kukuelekea wewe.

Unaweza mtengenezea kigari cha kujifunza kutembelea au kununua vya dukani kama unaweza, kitakachomsaidia kujishika na kusukuma.

Mruhusu mwanao ajifunze kutembea akiwa pekuu (bila viatu) na katika eneo salama(barazani) kama unaweza. Akitembea bila viatu itamsaidia kuimarisha usawa na uwezo wa kusogeza miguu yake kwa urahisi. Mtoto akibanwa na viatu au soksi huku anatembea hawezi kujinyoosha na kukua vizuri.

Hakuna haja ya kumvalisha mwanao viatu, mpaka atakapoweza kutembea kwa ujasiri nje mwenyewe.

Nawezaje kuhakikisha mwanangu anakua salama, sasa ameanza kutembea?

Mara mwanao anapoanza kutembea atazunguka haraka sana! Hakikisha kuna nafasi ya kutosha na sakafu ni tupu itamsaidia kutembea kwa urahisi. Hakikisha ana mazingira salama ya kujifunza kutembea. Hakikisha unaweka usalama ndani ya nyumba yako kama jikoni, bafuni na kwenye nyaya za umeme za televisheni au jokofu. Usimuache mwanao mwenyewe.

Vifuatavyo ni vidokezo vinavyoweza kusaidia nyumba yako ikawa salama kwa mtoto wako:

  • Kama hujatengeneza, weka milango ya usalama jikoni.
  • Hakikisha vitu hatarishi unavitoa kwenye droo anazoweza kufikia sebuleni au jikoni,kama kabati yenye visu,mikasi,dawa na sabuni za maji za kufulia na kudekia.
  • Funika kona zote zilizochongoka kama meza zilizo chini ili kumlinda mwanao asijiumize.

Je, ni sahihi mimi kuwa na wasiwasi mtoto wangu ana miezi 15, na hajaanza kutembea bado?

Watoto wanatofautiana uwezo, baadhi wanakua kwa haraka zaidi ya wengine. Baadhi ya watoto wanatambaa mapema na kuchelewa kutembea, wengine wanatamba na kisha kutembea, wengine hawatambai kabisa. Watoto kukua tofauti ni kawaida kabisa na hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.

Kama mwanao atafikisha umri wa miezi 18 na hajanza kutembea na una wasiwasi ongea mara moja na daktari au nesi.

Mara nyingi kasi ya mtoto wako kujifunza kusogea inarithiwa kutoka kwa wazazi wake. Ikiwa wewe au mwezi wako mlichelewa kutembea,kuna nafasi mwanao atafanya hivyohivyo.

Kumbuka kama mwanao alizaliwa kabla ya miezi 37 ya ujauzito, anaweza kufikia hatua hii ya kutembea kwa kuchelewa.

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.