Zingatia mambo haya kujikinga na malaria
Malaria ni moja ya magonjwa yanayoongoza kwa vifo nchini Tanzania. Ila ni ugonjwa ambao vilevile kwa maamuzi na bidii za binadamu ugonjwa huu unaweza kukwepeka. Fuatilia zaidi makala nzima kuhusu Ugonjwa wa Malaria.
Zifuatazo ni namna mbalimbali za kujikinga na malaria:
1. Kutumia chandarua kilicho wekwa dawa ya kuua mbu. Kutumia tu chandarua haitoshi. Ni muhimu kulala kwenye chandarua kilicho na dawa. Chandarua nyingi zinazouzwa madukani kwa muda huu zimeshawekwa dawa tayari, lakini unashauriwa kuuliza na kuwa na uhakika kuwa chandarua unachonunua kimewekwa dawa.
2. Kuweka mazingira safi kwa kufukia madimbwi na mashimo yasababishayo maji kutuama. Maji yanayotuwama huzalisha sana mbu. Mayai ya mbu hupendelea maeneo yenye majimaji lakini yasiyokuwa na kusogea (yaliyotuama), mfano madimbwi ya maji ya mvua yaliyokaa muda mrefu bila kukauka, unyevunyevu vichakani na kwenye nyasi ndefu, makopo yenye uwazi yaliyotelekezwa na kujaa maji ndani yake, magari mabovu yaliyonyeshewa mvua na kukusanya maji ndani, mabwawa madogomadogo kama ya kufugia samaki n.k. Hivyo ni vyema kufukia madimbwi, kufyeka nyasi, kuchoma au kusafisha makopokopo na magaloni na pia kuondoa magari mabovu na chochote kinachoweza kukusanya maji kwa muda mrefu kwa eneo lote linalozunguka nyumba yako. Ukifanya hivi utakuwa umesababisha hatua muhimu ya kisababishi cha malaria (mbu) asizaliwe.
3. Kuteketeza mazalia ya mbu kwa kunyunyuzia dawa ya DDT. Baada ya kufanikisha namba mbili hapo juu, na kuna sehemu ambazo mazalia ya mbu yanaweza kutokea na hakuna jinsi ya kuepuka maji haya yaliyotuama inashauriwa kunyunyuzia dawa ya DDT. Dawa hii ni sumu ambayo pia inaweza ikamdhuru binadamu. Hivyo shughuli ya kunyunyizia dawa hii hufanywa na wataalamu wa afya na mazingira.
4. Kufukuza na kuzuia kung`atwa na mbu. Ni ukweli kwamba pamoja na juhudi zote hapo juu bado kuna uwezekano wa kung`atwa nambu kwani tupo kwenye eneo la tropiki ambalo ndio makazi yao. Hivyo basi njia nyingine za ziada zinahitajika kujikinga using`atwe na mbu waliofanikiwa kuzaliwa.
• Kuua mbu – Kutumia dawa za kupuliza au kufukiza ndani na nje ya nyumba. Kuna baadhi ya kampuni wanafanya kazi ya kuua vimelea (fumigation) maeneo mbalimbali.
• Kufukuza mbu – Kutumia dawa za kupuliza au kufukiza ndani na nje ya nyumba (Ifahamike kuwa kuna dawa ambazo zina uwezo wa kufukuza pekee na kuna ambazo zinaua kabisa hivyo unavyonunua dawa dukani elewa unanunua dawa ya aina gani ili uitumie kama inavyoelekezwa)
• Kuzuia mbu – Dawa za kupaka. Kwa wakati ambao haupo nyumbani inawezekana ukawepo kwenye sehemu yenye mbu, mfano baa, mpirani au hata kazini katika ule muda ambao mbu hung`ata, ni vyema ukajikinga nao kwa kujipaka dawa mbalimbali za kuwafukuza au kuwaua mbu pale wanapokukaribia au kuanza kukung`ata. Dawa hizi zinatoa harufu ambayosio rafiki kwa mbu hawa au zina uwezo wa kuwaua pindi wanapoanza kukuchoma.
5. Kujikinga na ugonjwa wa malaria kwa kina mama wajawazito ni muhimu. Wajawazito wana hatari kubwa zaidi ya kung`atwa na mbu kutokana na mabadiliko yao ya kimwili, mfano joto la mwili kuongezeka, hivyo mbu huweza kuwafikia kwa urahisi zaidi. Inapendekezwa na wizara ya afya kwamba wanawake wajawazito watumie dawa ya malaria aina ya “SP” kabla ya kujifungua. Hii itawasaidia kama kinga dhidi ya malaria kwao na kwa watoto wao tumboni. Dozi ya dawa hizi hutolewa katika vituo vya afya vinavyo toa huduma kwa mama na mtoto.
6. Ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya dawa za malaria kwa wagonjwa. Kuzingatia dozi sahihi inaweza ikawa kinga kwa maambukizi mengine yanayokuja. Vilevile kutokumaliza dozi kunamaanisha kuviacha baadhi ya vimelea mwilini ambavyo havikufa tayari mpaka kipindi ulipoacha dozi.
7. Usitumie dawa bila kumuona daktari kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unaongeza usugu wa dawa mwilini mwako bila sababu ya msingi na pia unahatarisha maisha yako. Usugu wa dawa za malaria ni hatari na inamaanisha ukipata malaria na vimelea ulivyonavyo vimeshakuwa sugu kwa dawa zilizopo za malaria, maisha yako yanakuwa hatarini kwani madaktari watashindwa kukutibu.
Wito
Malaria ni ugonjwa hatari unaoua kwa haraka hivyo pindi unapohisi una dalili za malaria kama zilivyoorodheshwa hapo awali, wahi katika kituo cha kutoa huduma za afya kilichokaribu na wewe ili upatiwe uchunguzi na kupata tiba sahihi.
Imepitiwa: July 2017