Asidi ya foliki ni shujaa katika mimba! Kumeza vitamini kabla ya kupata ujauzito kwa kiwango kinachokubalika cha mikrogramu 400mcg kabla na wakati wa ujauzito huweza kusaidia matatizo ya kuzaliwa nayo kwenye ubongo, mgongo na uti wa mgongo wa mtoto wako. Ni vyema kumeza kidonge cha asidi ya foliki kila siku kama unategemea au wewe ni mjamzito tayari.
Asidi ya foliki (Folic acid) ni nini?
Asidi ya foliki ni aina ya vitamini B inayoitwa “folate” inayotengenezwa na mwanadamu maabara (inajulikana kama vitamini B9). “Folate” inafanya kazi muhimu kwenye utengenezaji wa chembe damu nyekundu na pia husaidia katika kukinga dhidi ya kasoro katika neva za fahamu na hivyo kuepusha dosari za kimaumbile katika ubongo, mgongo na uti wa mgongo. Chakula bora chenye wingi wa asidi ya foliki ni “fortified cereals”. Folati hupatikana zaidi kwenye mbogamboga zenye rangi kijani iliyokolea na matunda jamii ya chungwa.
Ni lini uanze kutumia asidi ya foliki?
Matatizo ya kuzaliwa nayo (dosari katika neva za fahamu) huanza kutokea ndani ya wiki ya 3-4 ya ujauzito (siku 28) baada ya mimba kutungwa, kabla hata mama kujua kuwa ni mjamzito. Hivyo ni muhimu kuwa na “folate” tayari kwenye mzunguko wa mwili wako kwenye kipindi hiki muhimu cha mwanzoni ambapo ndio ubongo na uti wa mgongo wa mtoto wako unajijenga.
Kama ulizungumza na daktari wako kipindi ulichokuwa unataka kupata ujauzito, inawezekana alishakushauri tayari kuanza kutumia vitamini na asidi ya foliki. Tafiti moja ilionesha wanawake waliotumia asidi ya foliki kwa kuanzia mwaka kabla ya kupata ujauzito walipunguza uwezekano wa kujifungua mapema kabla ya muda (kabla ya wiki 37) kwa asilimia 50 au zaidi.
Tafiti zinaonesha nusu ya mimba zote hazikuwa zimepangwa hivyo inapendekezwa kuwa mwanamke yeyote anayetarajia kupata ujauzito atumie mickrogramu 400 za vidonge vya foliki asidi kila siku, akianza kabla ya kupata ujauzito na kuendelea namna hiyo kwa wiki 12 za ujauzito. Muda huu wa wiki 12 za mwanzo wa ujauzito ndiyo muda ambao ubongo na mfumo wa neva unajengwa na kukua
Shirika la kuzuia magonjwa la Marekani (CDC) linashauri Vilevile shirika wanawake wote walio kwenye umri wa kuweza kuwa wajawazito kutumia asidi ya foliki kila siku. Hivyo hata ukiamua kuanza kutumia asidi ya foliki mapema zaidi ni vyema zaidi.
Kama utaamua kununua nyongeza ya vitamini wewe mwenyewe, ni vyema ukazungumza pia na daktari wako baada ya kupata ujauzito ili kuwa na uhakika kuwa nyongeza hiyo ya vitamini ina mjumuisho wa kila kitu unachotakiwa ukipate kwa ujauzito wako ikiwemo asidi ya foliki.
Kiasi gani cha asidi ya foliki nitumie?
Dozi inayoelekezwa kwa wanawake wote waliopo kwenye umri wa kuweza kupata ujauzito ni mikrogramu 400 au 400mcg za folati kila siku. Ikiwa wewe ni mjamzito au unajaribu kupata ujauzito unashauriwa kutumia foliki asidi mapema kadiri uwezavyo na ndani ya wiki 12 za kwanza za ujauzito. Kufanya hivi kutamsaidia mtoto kukua vizuri na kawaida.
Daktari anaweza kukushauri kutumia dozi kubwa zaidi ya foliki asidi ikiwa uko katika hatari kubwa ya kupata dosari katika neva za fahamu (neural tube defects) wakati wa ujauzito.
Huu ndio mchanganuo wa kiasi cha asidi ya foliki kinachoelekezwa kwa wanawake wajawazito kwa siku
- Ukiwa unataka kupata ujauzito – 400mcg
- Miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito – 400mcg
- Kuanzia mwezi wa 4 hadi wa 9 wa ujauzito – 600mcg
- Ukiwa unanyonyesha – 500mcg.
Mama ambaye tayari amepata mtoto mwenye dosari katika neva za nyuroni (mfumo wa fahamu) anahitaji ajadiliane na daktari wake kama atahitaji vidonge vya foliki na dozi yake itakuwa ni ipi. Tafiti zinaonesha kwamba matumizi ya mikrogramu 4,000 kwa mwezi mmoja kabla na katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito zinaweza kusaidia kutatua tatizo hili. Tafadhali usitumie dawa hizi mwenyewe bila kujadiliana na daktari kwanza.
Asidi ya foliki ina faida gani?
Bila kuwa na asidi ya foliki ya kutosha, dosari katika neva za fahamu na hivyo kuepusha kasoro za kimaumbile katika ubongo, mgongo na uti wa (neural tube defects). Magonjwa haya ni kama:
- Spina bifida: Kutokukamilika ukuaji wa uti wa mgongo au pingili za uti wa mgongo.
- Anencephaly: Kutokukamilika kwa ukuaji wa sehemu kubwa ya ubongo.
Watoto wenye “Anencephaly” mara nyingi hawaishi muda mrefu na wale wenye “spina bifida” huwa na ulemavu maisha yao yote. Habari njema ni kwamba kutumia nyongeza ya asidi ya foliki kipindi cha ujauzito inaweza kumuepusha mtoto wako kupata magonjwa haya kwa zaidi ya asilimia 50.
Kama utatumua kabla na wakati wa ujauzito, asidi ya foliki inaweza kumkinga mtoto wako dhidi ya:
- Mdomo sungura
- Kuzaliwa kabla ya muda (Njiti)
- Kuzaliwa na uzito mdogo
- Mimba kutoka
- Ukuaji dhaifu tumboni
Asidi ya foliki pia inahusishwa na kupunguza hatari ya kupata:
- Matatizo kwenye ujauzito
- Magonjwa ya moyo
- Kiharusi
- Aina baadhi ya saratani
- Ugonjwa wa “Alzheimer”
Je, kuna vyanzo vingine vya folati?
Vyakula vilivyo na foliki asidi katika kiwango kiubwa ni kama:
- Mboga za majani kama spinachi, kabichi, loshu, broccoli
- Mimea jamii ya kunde kama maharage, mbaazi, njegere, njugu
- Karanga, njugumawe, nazi na korosho
- Matunda jamii ya sitrusi kama machungwa, machenza, limao n.k
- Nafaka zisizokobolewa
- Maini na samaki
- Vyakula vilivyoongezwa foliki asidi.
Kumbuka
- Kichefuchefu, kupoteza hamu ya kulan a kuvimbiwa ni madhara yanayoweza kutokea kwa mjamzito kama matokeo ya kutumia vidonge hivi. Ulaji wa chakula kidogo kidogo badala ya kula milo mikubwa mitatu kwa siku, kula na kunywa taratibu na kufanya mazoezi mepesi mara kwa mara yanaweza kusaidia dalili hizi unazoweza kupata kama matokeo ya kutumia asidi ya foliki. Ikiwa dalili hizi zinaendelea kuwa mbaya, wasiliana na daktari/mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wako mara moja.
- Mtoto tumboni yuko katika hatari ya kupata dosari katika mfumo wa fahamu ikiwa: mama mjamzito aliwahi kupata ujauzito ulipata dosari katika mfumo wa neva za fahamu, wewe au mwezi wako ana kasoro katika neva za fahamu aliyozaliwa nayo,katika familia yako au mwezi wako kuna historia ya watu kuzaliwa na dosari katika neva za fahamu, mjamzito ana kisukari,mjamzito ana uzito mkubwa uliopitiliza na mjamzito ana ugonjwa wa siko seli.
- Mama ambaye hakutumia foliki asidi kabla au miezi ya awali ya ujauzito ajadiliane na daktari/mkunga anayesimamia maendeleo ya ujauzito wake, wataweza kukushauri nini kifanyike na dozi kiasi gani itumike kuokoa maisha ya mtoto tumboni. Tafadhali usitumie dawa hizi mwenyewe bila kujadiliana na daktari kwanza.
IMEPITIWA: JUNI,2021.