Mazoezi kipindi cha ujauzito.
Je ni salama?
Kufanya mazoezi ni jambo ambalo binadamu wengi hulifanya mara kwa mara ikiwa ni mpango wa kimaisha au hulifanya mara moja moja. Mazoezi ni kitendo cha kuushughulisha mwili kwa njia mbalimbali. Mazoezi yaliyojipatia umaarufu ni kama kutembea, kukimbia, kushiriki michezo mbalimbali na hata watu hutumia vifaa maalumu vya mazoezi kuishughulisha miili yao. Hivi karibuni vituo vingi vya mazoezi ambavyo vilikuwa maarufu kwenye nchi zilizoendelea vinaanza pia kuonekana barani Afrika.
Mazoezi ni mazuri kwa afya ya mwili na akili. Pia mazoezi ni njia nzuri kupata afya bora. Ikiwa ni kawaida kabisa watu wa umri wowote ule kushiriki katika mazoezi, huwa inazua mjadala mara kwa mara ni kwa namna gani wajawazito wafanye mazoezi. Kwanza kabisa je wanaruhusiwa kisayansi kufanya mazoezi?
Waandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya DW waliwahi kuyasema haya kuhusu mabadiliko ya mtazamo wa kisayansi kuhusu kufanya mazoezi wakati wa ujauzito
Nukuu
Miaka 20 iliyopita, madaktari wangemuambia mama mjamzito kupumzika kadiri awezavyo, kwa kuhofia kuathiri ukuaji wa kiumbe aliye tumboni, na kusababisha uchungu wa mapema au hata mimba kutoka. Hata hivyo chuo cha wakunga na madaktari wa wanawake cha nchini Marekani ACOG, kinasema kujishughulisha kimwili kuna hatari ndogo sana na kunawasaidia wanawake wengi zaidi.
Miongozo ya hivi karibuni ya chuo cha ACOG, kuanzia mwishoni mwa mwaka 2015, ambayo inatazamwa kama alama teule duniani kote, inabainisha kuwa wasiwasi kuhusu uzazi wa njiti, kutoka kwa mimba au kudumaa kwa kijusi kutokana na mazoezi haujathibitishwa. Kwa mujibu wa ACOG, wanawake wanatakiwa kuhimizwa kushiriki katika mazoezi ya viungo na kuimarisha misuli kabla na baada ya ujauzito.
Nicole Goebel/Iddi Ssessanga – DW
Aina za Mazoezi Kipindi cha Ujauzito
Mazoezi ya dakika kati ya 20 hadi 30 yanapendekezwa kwa siku nyingi za wiki kwa mwenye ujauzito usio na matatizo yoyote – wakiwemo wale walio na uzito uliopitiliza au wasio na shughuli za kutosha. Haijalishi pia wewe ni mtu wa umri gani. Inapendekeza baadhi ya michezo, kama vile kuogelea au kutembea, ambayo ni rahisi kwa viungo.
Faida za Mazoezi
Mazoezi yanaweza kukusaidia kuwa mwenye afya na kukuepushia kisukari cha ujauzito, ambacho kinaweza kukidhuru kiumbe tumboni na kinachohitaji mlo makhsusi, na katika wakati mwingine sindano za insulini hata kama kwa kawaida hauna ugonjwa wa kisukari. Kulingana na ACOG, mazoezi yanaweza pia kupunguza hatari ya tatizo linalosababishwa na kupanda kwa shinikizo la damu na vilevile kujifungua kwa njia ya upasuaji.
Wakati watafiti wakiendelea kutafuta njia za kuzuia uzito uliopitiliza hasa miongoni mwa watoto wadogo, faida za mazoezi wakati wa ujauzito zimevutia usikivu wa wanasayansi. Wakati hakuna ushahidi kuonyesha kuwa mtoto wako atakuwa na umbo la kimichezo kwa sababu umekuwa ukifanya mazoezi wakati wa ujauzito, mazoezi yanaweza kuathiri ukuaji wa viungo vya mtoto huyo, na hivyo kuwa na faida katika utoto wake na kuendelea.
Ikiwa mazoezi laini ni jambo usilotegemea kufanya, mazoezi yalioboreshwa ya yoga yanaweza kukusaidia kubakia mnyumbufu na kukusaidia pia dhidi ya maumivu ya mgongo – ambayo ni tatizo la kawaida wakati wa ujauzito, kwa sababu kina mama wanakuwa na kawaida ya kuumwa mgongo kutokana na uzito ulioongezeka.
Hivyo hakuna kisingizio cha kutokufanya mazoezi- lakini unapaswa kuchagua mazoezi yako kwa umakini. Michezo ya kugusana kama vile soka, ndondi, mpira wa kikapu/pete haishauriwi. Pia jiepushe na michezo ya kujitupa majini, kupanda, kupanda juu ya zaidi ya mita 2,000, na jambo lolote linaloweza kukuweka katika hatari ya kuanguka. Pia jihadhari sana wakati wa joto kali, vilevile pumzike ukiwa na dalili zozote za mafua, maumivu ya kichwa au kizunguzungu.
IMEPITIWA: OKTOBA,2021.