Ugonjwa wa Kichocho

Kichocho ni nini?

Kichocho ni ugonjwa unaosababishwa na minyoo midogo aina ya Schistosoma au Bilhazia. Minyoo ambayo huingia katika mwili wa binadamu kwa njia ya vitundu vya ngozi na kusababisha mwasho katika viungo mbalimbali vya mwili. Hivyo kupelekea homa, mwili kudhoofu, kupungukiwa kinga mwilini na hatimaye mtu kupoteza maisha.
Pamoja na binadamu kuonekana kuugua ugonjwa wa kichocho pia wanyama wafugwao kama vile Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo hupatwa pia na ugonjwa huu wa kichocho wanapotumia maji yaliyo na vijidudu vya maradhi hayo.

Kichocho kinaenezwaje?

Minyoo aina ya Schistosoma ambayo hueneza Kichocho cha mkojo hasa kwa binadamu inatokea katika Konokono waishio katika maji. Kichocho cha mkojo kwa binadamu husambazwa na konokono wajulikanao kama Bulinus africanus, Bulinus tropicus na Bulinus forskalli, konokono hawa pia husambaza kichocho cha ng’ombe. Kichocho cha matumbo cha binadamu husambazwa na konokono waitwao Biomphalaria pfeiferi.
“Schistosoma lava wakiwa katika maji hutoboa ngozi ya binadamu au mnyama aliyeingia katika maji hayo na kuingia hadi kwenye mishipa ya damu mpaka kufika kwenye maini ambapo hapo hubadilika na kuwa minyoo ambayo itaendelea kukua na kuelekea katika sehemu mahsusi ya mwili ambapo minyoo wakubwa hukaa ” anasema Dkt. Jahashi Nzalawahe kutoka idara ya Vetenari Microbaiolojia na Parasaitolojia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA.

Aina za kichocho

“Kuna aina kuu mbili za kichocho ambazo ni kichocho cha mkojo na kichocho cha tumbo, Kichocho cha mkojo (Urinary schistosomiasis) husababishwa na minyoo inayoitwa Schistosoma haematobium ambao huishi katika mishipa ya damu ya kibofu cha mkojo cha binadamu na Kichocho cha matumbo (Intestinal schistosomiasis) ambacho husababishwa na minyoo iitwayo Schistosoma mansoni ambao hupatikana katika mishipa ya damu ya utumbo”
“Dalili kuu za Kichocho cha mkojo ni kuwepo kwa damu katika mkojo, kujisikia hali ya mwili kuchoka, kuwa na kikohozi kikavu na maumivu ya misuli, pia dalili za Kichocho cha tumbo ni kuharisha kinyesi chenye damu, maumivu ya tumbo na kuvimba tumbo” anaeleza Dkt. Nzalawahe.
Kama nilivyoeleza awali Kichocho huwapata binadamu pamoja na wanyama wafugwao kama Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo kiitwacho (Bovine Schistosomiasis) ambacho husababishwa na minyoo iitwayo Schistosoma bovis waishio katika mishipa ya damu ya utumbo wa wanyama na kupelekea mnyama kupunguza hamu ya kula, kuharisha damu, upungufu wa damu, mnyama kukonda na asipopata tiba mnyama hufa.

Jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa kichocho.

Ugonjwa wa kichocho unaweza kuzuiwa kwa urahisi iwapo kanuni za kiafya zitazingatiwa. Hata hivyo hadi sasa hakuna chanjo iliyopatikana ya kudhibiti ugonjwa huo. Si maji yote ni salama kwenye maeneo yaliyo na ugonjwa huu. Sehemu hatari zaidi za ugonjwa huo ni maeneo kama vile kingo za maziwa, mito na mabwawa ambapo maji yametuama na kuna uoto wa mimea. Sehemu salama ni kama vile katika fukwe za bahari na zile zenye mawimbi ambazo si rahisi kukuta konokono wa majini. Mabwawa ya kuogelea ni salama iwapo yatanyunyiziwa dawa ya klorini.

1. Kuacha kujisaidia haja kubwa au ndogo kwenye mabwawa, mito, maziwa na mifereji ya maji. Kwa mtu mwenye kichocho (cha mkojo (Bilhazia) anapokojoa mkojo hutoka na mayai ya kichocho, na kwa kichocho cha tumbo, haja kubwa huwa na mayai ya kichocho ambayo huanguliwa mara tu yanapogusana na maji na vijidudu vilivyo anguliwa huingia mwilini mwa konokono na kuendelea kukua, baada ya wiki tano hutoka na kurudi kwenye maji, ambako huogelea kutafuta mtu aliyepo ndani ya maji na huingia kwenye mwili wa mtu kupitia kwenye ngozi.

2. Kuacha kuoga, kuchota, kufua nguo kwenye maji yaliyotuama kama vile katika mabwawa, mito, maziwa na mifereji ambayo mingi inakuwa na konoko wanaosambaza kichocho. Badala yake watu wawekewe maji ya bomba ambayo huwekewa dawa za kuua vimelea vya maradhi.

3. Kuondoa majani yaliyoota kwenye maji sehemu ambazo watu huenda kuchota maji, kufua, na kuoga katika mabwawa, mito, maziwa, mifereji lengo likiwa ni kuharibu makazi ya konono.

4. Kusafisha mifereji ya umwagiliaji vizuri muda wote ili kupunguza uzalianaji wa konono, na bora zaidi ni kuijenga mifereji kwa mawe na sementi, ili kuharibu kabisa makazi ya konokono.

5. Kwa wakulima wanaofanya kilimo cha umwagiliaji yafaa wavae mabuti na gloves kujikinga na vijidudu vya kichocho kujipenyeza kwenye ngozi. Njia nyingine ni kunyunyizia dawa za kuua konokono kwenye maji (ziwa, mto, bwawa, mfereji), wenye konokono waenezao kichocho.

6. Bila kusahau maji ya kunywa yachemshwe na kuchujwa ili kuuwa vijidudu vya maradhi mbalimbali ikiwemo wadudu wa kichocho.

Ni vyema tujue kuwa, mtu anapaswa kumuona daktari baada ya kuwa na dalili za ugonjwa na yeye ndiye atakayemuainishia dawa za kutumia. Ni matarajio yetu kuwa iwapo tutafuata kanuni na misingi yote hiyo ya kiafya hapo juu, basi tutafanikiwa kushinda vita dhidi ya maradhi ya kichocho. Kwa kufanya hivyo maambuki ya kichocho yanawezwa kuzuiliwa na hatimaye ugonjwa huu kuweza kuteketezwa kabisa

Programu ya AfyaTrack

Programu ya kwanza nchini Tanzania ya kufuatilia maendeleo ya ujauzito na ukuaji wa mtoto kwa lugha ya Kiswahili.